Sura ya 7 — Kuenea kwa kasi kwa ujumbe
GSAM 126.1“Nami nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua ulikuwa juu ya kichwa chake, na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto; naye alikuwa na kitabu kidogo kilichofunguliwa mkononi mwake; akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi, akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo; naye alipolia, ngurumo saba zikatoa sauti zao.... Na yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi akainua mkono wake kuelekea mbinguni, akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hakutakuwa na wakati tena; lakini katika siku za sauti ya malaika wa saba, atakapoanza kupiga baragumu, siri ya Mungu itatimizwa, kama alivyowatangazia watumishi wake manabii.”1
GSAM 126Malaika ni Ishara ya Wajumbe Wanadamu
GSAM 126.2Kama ilivyokwisha kuonyeshwa, kazi ya kuhubiri injili imekabidhiwa kwa mwanadamu, na Bwana ameahidi kuibariki njia hiyo ya utendaji hadi “mwisho wa ulimwengu.”2 Kwa hiyo malaika anayeleta ujumbe huu lazima awe ishara ya ujumbe unaohusu wakati, utakaohubiriwa kwa wakaaji wa dunia. Ujumbe huo unatangazwa kutoka katika kitabu “kilichofunguliwa,” jambo linaloonyesha wazi kwamba wakati mmoja kilikuwa kimefungwa. Wajumbe hawa wanathaminiwa na Mungu; kwa maana “upinde,” ishara ya agano la Mungu, uko juu yao, nao wamesimama wakiwa wamevikwa nuru ya utukufu wa Mungu, na wanatangaza ujumbe kwa mamlaka ya Muumba wa vitu vyote. Kinachotangazwa hapa ni ujumbe unaohusu wakati, ambao hapo kwanza ulikuwa “umetiwa muhuri,” lakini sasa unatangazwa kutoka katika kitabu “kilichofunguliwa.”
GSAM 127.1Katika sura zilizotangulia imethibitishwa kwamba Bwana aliweka wakati ambapo nuru ingetolewa kuhusu mwisho wa kile kipindi kikuu cha unabii—siku 2300—kinachoongoza kwenye hukumu ya upelelezi; kwamba utabiri wa kuongezeka kwa maarifa ulitimizwa kwa usahihi kwa kuinuliwa kwa watu wengi ambao aliwafunulia nuru hiyo; na kwamba pia aliweka wakati ambapo “mfano wa mtini” ulipaswa kujifunzwa, kwa kuwainua walimu wake wakati huo na mahali hapo ili watoke na kuutangaza mfano huo kwa ulimwengu. Kwa usahihi huohuo ameweka wakati ambapo ujumbe unaohusu wakati ungeongezeka na kuwa kilio chake kikuu, na jambo hilo lilitimizwa kwa usahihi huohuo.
GSAM 127Kilio Kikuu cha Ujumbe wa Kwanza
GSAM 127.2Wakati ambapo kilio kikuu cha tangazo hili kingetolewa ni jambo linalovutia kuchunguzwa. Hapa umewekwa kati ya kupigwa kwa baragumu la sita na la saba, kama inavyoonekana kwa mahali lilipo katika maandiko ya Biblia, na pia kwa ujumbe wenyewe, unaosema: “Katika siku za sauti ya malaika wa saba, atakapoanza kupiga baragumu, siri ya Mungu itatimizwa, kama alivyowatangazia watumishi wake manabii.” Huu ni ushahidi wa kukata shauri kwamba wakati unaotangazwa katika ujumbe huu unaendelea hadi kupigwa kwa baragumu la saba.
GSAM 127Wakati wa Kilio Kikuu
GSAM 127.3Malaika wa saba anapopiga baragumu, tunasoma kwamba “hekalu la Mungu likafunguliwa mbinguni, na ndani ya hekalu lake likaonekana sanduku la agano lake.”3 Katika huduma ya patakatifu pa duniani, chumba kilichokuwa na sanduku—patakatifu pa patakatifu—kilifunguliwa mara moja tu kwa mwaka; ilikuwa katika siku ya upatanisho, kwa kusudi la kufuta dhambi—kutakaswa kwa patakatifu. Wakati ulionenwa na manabii, ambapo kazi hii ya utakaso, inayofanywa na Kristo, ingefanyika, ni mwisho wa siku 2300.4 Pia imeelezwa kwamba malaika wa saba anapopiga baragumu, sauti mbinguni zinasema kwamba wakati wa wafu kuhukumiwa umefika.5
GSAM 128.1Ishara hii ya unabii katika Ufunuo 10 inaonyesha wakati ambapo ujumbe huu utatoka “kwa sauti kuu,” na hatimaye, “kama simba angurumavyo.” Wakati ambapo, kulingana na unabii huu, ujumbe ungeongezeka na kuwa “kilio kikuu” ni tangu mwisho wa baragumu la sita hadi mwisho wa kile kipindi cha unabii kinachoongoza kwenye kutakaswa kwa patakatifu, yaani, hadi mwisho wa siku 2300. Baragumu manne ya kwanza yalitimizwa katika vita vya Wagothi, Wavandali, Wahunni, na wengineo, ambavyo viliigawanya Roma ya Magharibi katika sehemu au falme kumi.
GSAM 128Baragumu la Tano
GSAM 128.2Baragumu la tano linaonyesha kutokea kwa Uislamu pamoja na wingu lake la mafundisho ya uongo, lakini hasa kipindi cha “miezi mitano,” au miaka mia moja na hamsini halisi tangu wakati ambapo “walikuwa na mfalme juu yao.” Tarehe 27 Julai, 1299, Othman, mwanzilishi wa Milki ya Waosmani, alivamia eneo la Nikomedia. Tangu wakati huo Waosmani waliisumbua na “kuitesa” milki ya Roma ya Mashariki hadi tarehe 27 Julai, 1449, ile miaka mia moja na hamsini ya kupigwa kwa baragumu la tano. Wakati huo Waturuki walikuja na majeshi yao dhidi ya mji wenyewe wa Konstantinopoli, wakitumia baruti katika vita vyao; na kwa mzinga mzito, ambao mwanahistoria Gibbon anasema ulihitaji maksai sitini kuuvuta, walifyatua mawe makubwa dhidi ya kuta za Konstantinopoli.
GSAM 128Mwisho wa Baragumu la Sita
GSAM 128.3Karibu na wakati huu John Palleologus, ambaye wanahistoria wanamtaja kuwa kaizari wa mwisho wa Kigiriki, alikufa. Constantine Decozes ndiye aliyekuwa mrithi halali wa kiti cha enzi, lakini inasemekana kwamba hofu yake kwa Amurath, sultani wa Waturuki aliyekuwa akipigana vita hivi dhidi yake, ilimfanya aombe ruhusa kwa Amurath ya kukalia kiti cha enzi. Tendo kama hilo karibu lingeonekana kuwa kuwakabidhi Waturuki kiti cha enzi. Kwa kweli, baada ya muda mfupi sana Waosmani waliumiliki mji wa Konstantinopoli na milki ya Roma ya Mashariki. Kwa hiyo wao “waliiua” milki hiyo kisiasa, ambayo hapo awali walikuwa “wameitesa.” Walipaswa “kuiua” kwa muda wa “saa moja, na siku moja, na mwezi mmoja, na mwaka mmoja.”
GSAM 129.1Tukichukulia huu kuwa wakati wa unabii, siku moja kwa mwaka mmoja, ungekuwa muda gani? Hesabu yake ni rahisi: mwaka mmoja, siku 360, au miaka; mwezi mmoja, siku 30, au miaka; na siku moja, mwaka mmoja—kwa jumla, siku 391, au, kwa uhalisi, miaka 391. Saa moja, ikiwa sehemu ya ishirini na nne ya siku, kama ishara ingekuwa nusu mwezi, au siku kumi na tano. Kwa hiyo muda wote wa utawala huru wa Waislamu katika eneo la Roma ya Mashariki ungekuwa miaka 391 na siku 15. Tukiongeza muda huu kwa tarehe 27 Julai, 1449, tunafikia tarehe 11 Agosti, 1840, kuwa mwisho wa kipindi cha uhuru wa Waturuki, kama kilivyoelezwa chini ya baragumu la sita.
GSAM 129Daktari Josiah Litch Anatabiri Kuanguka kwa Milki ya Waosmani
GSAM 129.2Mwaka 1838 Daktari Josiah Litch, wa Philadelphia, Pennsylvania, baada ya kuukubali ukweli uliotolewa na William Miller, alijiunga na kazi ya kuutangaza ujumbe kwa watu wengi zaidi. Aliandika makala kwa ajili ya magazeti kuhusu baragumu saba za Ufunuo. Alisema bila kusita kwamba baragumu la sita lingekoma kulia na mamlaka ya Waosmani ingeanguka tarehe 11 Agosti, 1840, na kwamba jambo hilo lingeuthibitishia ulimwengu kuwa siku moja katika unabii wa ishara inawakilisha mwaka mmoja wa wakati halisi.
GSAM 129.3Baadhi ya ndugu, hata wale waliokubaliana naye katika jambo hili, walitetemeka kwa kuogopa matokeo “ikiwa halingetimia” kama alivyosema. Hata hivyo, hili halikumvunja moyo, bali aliendelea kufanya yote aliyoweza ili kutangaza maoni yake kuhusu suala la Waturuki. Magazeti yalisambaza kauli aliyokuwa ametoa kuhusu jambo hilo. Vyama vya wasioamini vilijadili suala hilo katika mikutano yao, vikisema, “Huyu ni mtu anayethubutu kuhatarisha jambo, na ikiwa suala hili litatokea kama anavyosema, litathibitisha bila shaka madai yake kwamba siku moja katika unabii inaashiria mwaka mmoja, na kwamba siku 2300 ni miaka ya idadi hiyo hiyo, na kwamba itaisha mwaka 1844.”
GSAM 130.1Kuchapishwa kwa hotuba ya Daktari Litch kulizua msisimko mkubwa, na hivyo maelfu mengi ya watu walielekezwa kutazamia mwisho wa matatizo yaliyokuwa yamezuka kati ya Mehemet Ali, pasha wa Misri, na sultani wa Waturuki. Mamia walisema, “Ikiwa jambo hili litaisha kama daktari alivyosema, litathibitisha kanuni ya ‘siku kwa mwaka’ ya kutafsiri wakati wa ishara, nasi tutakuwa Waadventista.”
GSAM 130Sultani wa Waturuki Katika Vita na Pasha wa Misri
GSAM 130.2Kwa miaka kadhaa kabla ya 1840, sultani alikuwa ameingia katika vita na Mehemet Ali, pasha wa Misri. Mwaka 1838 matatizo kati ya sultani na mtawala wake wa Misri aliyekuwa chini yake yalizuiwa kwa muda kwa ushawishi wa mabalozi wa nchi za kigeni. Hata hivyo, mwaka 1839 mapigano yalianza tena na kuendelea hadi, katika pambano kuu kati ya majeshi ya sultani na ya Mehemet, jeshi la sultani lilipovunjwavunjwa na kuangamizwa kabisa, na kundi lake la meli za kivita lilipotekwa na Mehemet na kupelekwa Misri. Nguvu za sultani zilikuwa zimepungua sana kiasi kwamba, vita vilipoanza tena mwezi Agosti, alikuwa na meli mbili tu kubwa za kivita za daraja la kwanza na meli tatu nyepesi za kivita, masalio ya kusikitisha ya kundi la meli za Waturuki lililokuwa na nguvu hapo awali. Mehemet alikataa katakata kuliachilia kundi hili la meli na kulirudisha kwa sultani, akatangaza kwamba ikiwa mataifa yenye nguvu yangejaribu kulinyang'anya kutoka kwake, angelichoma moto. Mambo yalikuwa katika hali hii wakati, mwaka 1840, Uingereza, Urusi, Austria, na Prussia zilipoingilia kati na kuamua kutatua tatizo hilo; kwa maana ilikuwa wazi kwamba, kama angeachwa afanye atakavyo, Mehemet angekitwaa upesi kiti cha enzi cha sultani.
GSAM 131Kuingilia Kati kwa Mataifa Yenye Nguvu Yaliyoungana
GSAM 131.1“Sultani alikubali kuingilia kati huku kwa mataifa yenye nguvu yaliyoungana, na hivyo akalikabidhi suala hilo mikononi mwao kwa hiari. Mkutano wa mataifa haya ulifanyika London, shehe Effendi Bey Likgis akiwapo kama mwakilishi mwenye mamlaka kamili wa Waosmani. Masharti ya mwisho yaliandaliwa ili kuwasilishwa kwa pasha wa Misri, ambayo kwa hayo sultani angempa utawala wa kurithi wa Misri, na utawala wa maisha yake yote juu ya sehemu yote ya Siria inayoanzia Ghuba ya Suez hadi Ziwa la Tiberia, pamoja na jimbo la Akko; naye, kwa upande wake, alipaswa kuondoka katika sehemu nyingine zote za nchi za sultani alizokuwa akizikalia wakati huo, na kurudisha kundi la meli za Waosmani. Ikiwa angekataa pendekezo hili la sultani, mataifa hayo manne yenye nguvu yangelichukua suala hilo mikononi mwao wenyewe, na kutumia njia nyingine ambazo yangeona zinafaa ili kumfanya akubali masharti.
GSAM 131.2“Ilikuwa wazi kwamba mara tu masharti haya ya mwisho yangekabidhiwa mikononi mwa Mehemet Ali, suala hilo lingekuwa milele nje ya uwezo wa yule wa kwanza [sultani], na tangu wakati huo maamuzi kuhusu mambo yake yangekuwa mikononi mwa mataifa ya kigeni yenye nguvu.
GSAM 131Unabii Watimizwa—Mwisho wa Uhuru wa Waturuki
GSAM 131.3“Sultani alimtuma Rifat Bey kwa meli ya mvuke ya serikali kwenda Aleksandria, ili kumjulisha pasha masharti hayo ya mwisho. Yalikabidhiwa mikononi mwake, naye akayapokea tarehe kumi na moja Agosti, 1840! Siku hiyohiyo sultani aliwaandikia mabalozi wa mataifa manne yenye nguvu, akiuliza ni mpango gani ambao ungetumika ikiwa pasha angekataa kutimiza masharti hayo ya mwisho; nao wakajibu kwamba maandalizi yalikuwa yamefanywa, na hakukuwa na haja ya yeye kuwa na hofu kuhusu jambo lolote ambalo lingeweza kutokea. Siku hii kipindi cha miaka mia tatu na tisini na moja na siku kumi na tano kilichowekwa kwa ajili ya kuendelea kwa mamlaka ya Waosmani kikaisha; nao uhuru wa sultani ulikuwa wapi?—Ulikuwa umetoweka!”6
GSAM 132.1Tangu siku hiyo hadi leo sultani amelazimika kutenda kulingana na maagizo ya mataifa yenye nguvu, na kutazama ufalme wake ukigawanywa, huku sehemu zake zikitwaliwa moja baada ya nyingine kwa matumizi yao wenyewe.
GSAM 132Hamu ya Watu Kuhusu Unabii Yaamshwa
GSAM 132.2Kutimia huku kwa unabii kwa namna ya kushangaza kuliathiri sana mawazo ya watu. Kuliongeza hamu ya watu ya kusikia kuhusu unabii uliotimizwa na unaotimizwa. Daktari Litch alisema kwamba katika miezi michache baada ya tarehe 11 Agosti, 1840, alikuwa amepokea barua kutoka kwa watu mashuhuri zaidi ya elfu moja wasioamini, baadhi yao wakiwa viongozi wa vyama vya wasioamini, ambamo walisema kwamba walikuwa wameacha vita dhidi ya Biblia, na wameikubali kuwa ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu. Baadhi yao walimgeukia Mungu kikamilifu, na kadhaa wakawa wanenaji hodari katika vuguvugu kuu la ujio wa pili. Baadhi walimweleza Daktari Litch hivi: “Tumesema kwamba wafafanuzi wa unabii hunukuu kurasa za historia zilizochakaa ili kuthibitisha madai yao ya kutimia kwa unabii; lakini katika jambo hili tuna mambo halisi yanayotendeka mbele ya macho yetu wenyewe.”
GSAM 132.3Ili kuonyesha jinsi ambavyo, wakati uleule wa mwisho wa baragumu la sita, ujumbe wa ujio wa pili ulianza kutangazwa “kwa sauti kuu,” nitataja tukio kama nilivyosimuliwa na mmoja wa wale walioshiriki katika kuutangaza ujumbe huu.
GSAM 132.4Mwaka 1840, E. C. Williams, mtengenezaji mkubwa wa mahema na matanga ya meli, wa Rochester, New York, aliukubali ujumbe, akawaalika Wachungaji Miller na Himes waje Rochester ili kuzungumza na maelfu ya watu wa mji huo. Walijibu kwamba hawakuwa na fedha zilizohitajika kupata ukumbi mkubwa wa kutosha kuwatosha watu. Akajibu, “Nina hema la mviringo lenye kipenyo cha futi 120. Nitalisimamisha, nitaweka viti ndani yake, na kulitunza, bila malipo. Njoni mtangaze ujumbe.” Aliniambia, “Walikuja, lakini hema halikutosha hata nusu ya wale waliokuja kusikia, kwa hiyo nikaongeza kipande cha futi arobaini, likawa hema lenye ukubwa wa futi 160 x 120. Hema hili lilijaa watu kila siku, na mamia wakasongamana karibu nalo kwa nje, wote wakiwa na shauku ya kulisikia neno.”
GSAM 133Mamia Wakitangaza Ujumbe
GSAM 133.1Ili kukidhi hamu iliyokuwa ikiongezeka, mahema makubwa yalitumiwa, na mikutano ilifanywa katika vijisitu wakati wa majira ya kiangazi. Baadhi ya majengo makubwa zaidi ya makanisa na kumbi za umma zilitumiwa wakati wa majira ya baridi, na sehemu hizo zote zilijaa kabisa wasikilizaji wenye hamu. Badala ya Mchungaji Miller kusimama “karibu peke yake” katika kutangaza ujumbe, kama alivyokuwa kabla ya 1840, sasa watu wapatao mia tatu waliungana naye kutangaza hadharani mwisho wa kipindi cha siku 2300, na kutoa kilio, “Hakutakuwa na wakati tena,” na, “Saa ya hukumu yake imekuja.” Hivyo tunaona jinsi ambavyo, wakati wa Bwana ulipofika wa ujumbe kuenea ulimwenguni kote, neno lake lilitimizwa, na mamilioni ya watu wakaguswa na hamu ya kuusikia mwito.
GSAM 133.2Yaliyokuwa kweli kuhusu vuguvugu hilo huko Amerika yalikuwa kweli pia katika nchi nyingine. Tangu mwaka 1840, badala ya watu wachache kusambaza machapisho yao, makumi mengi ya watu walijitokeza, kana kwamba wakisonga mbele kutangaza kilio. Huko Uingereza kulikuwa na wachungaji mia saba wa Kanisa la Uingereza pekee waliokuwa wakitangaza ujumbe, bila kuhesabu makumi mengi ya wengine waliokuwa wakifanya kazi hiyo hiyo. Katika zaidi ya mataifa ishirini kati ya mataifa mbalimbali makubwa ya dunia ujumbe ulikuwa ukienea kwa bidii iliyomfanya mtazamaji aseme, “Watu hawa wamejitoa kwa dhati kwa kiwango cha ajabu.”