Sura ya 19 — “Mtawatambua kwa matunda yao”
GSAM 299.1“Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, kwa kazi ya huduma, kwa kuujenga mwili wa Kristo; hata sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na wa kumjua Mwana wa Mungu, kufikia mtu mkamilifu, kufikia kipimo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”1
GSAM 299.2Mwokozi alipoweka karama za Roho wake katika kanisa, ili kutimiza kazi ya Bwana “kama alivyopenda yeye,” mpaka siku kamilifu itakapofika, hakuwaacha watu wake wakisie kama udhihirisho fulani ulitoka mbinguni au kwa pepo wabaya, bali anatoa kanuni ambazo kwazo tunaweza kujua kama roho hiyo ni ya Mungu au sivyo. Hata katika siku hizi za mwisho, ambapo, kama nabii Yoeli alivyotabiri, Bwana angemimina Roho wake juu ya wote wenye mwili, na wana na binti wangetabiri,2 Paulo anasema watu wasidharau unabii, bali “wajaribu mambo yote,” na “walishike lililo jema.”3
GSAM 299.3Udhihirisho wa namna hiyo unaweza kujaribiwa kwa njia gani nyingine isipokuwa kwa kuulinganisha na kanuni za Maandiko za kutambua kazi ya Roho wa Mungu? Si kila jambo linalopita ufahamu wa akili zenye mipaka hutoka kwa Mungu, kwa maana Biblia inasema kwamba katika siku za mwisho Shetani atatenda miujiza ili kuudanganya ulimwengu, apate kuwakusanya watu kwenye vita vya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.4 Basi karama ya kweli ya kiroho inaweza kutambuliwa kwa kulinganisha kwa makini udhihirisho wake na kanuni za Biblia. Katika jambo hili inahitajika tahadhari ileile wanayotumia watu wa ulimwengu katika kutambua fedha bandia.
GSAM 300Kutambua Fedha Bandia
GSAM 300.1Katika gazeti la Mtoa Habari za Noti za Benki la Detroit la Aprili, 1863, Bwana Preston alitoa kanuni tano za kutambua fedha bandia, naye akasema kwamba mtu yeyote ambaye angekagua kwa uangalifu mkubwa kila noti aliyoipata, kwa kufuata kanuni hizo, hangehitaji kamwe kuogopa kudanganywa.
GSAM 300.2Hakuna njia ya hakika zaidi ya kujaribu karama ya unabii kuliko kuilinganisha na maelezo ya karama za namna hiyo zilizodhihirishwa katika nyakati za Maandiko, na kuijaribu kwa kanuni zilizotolewa humo. Maandiko hutukamilisha kwa kila kazi njema (2 Timotheo 3:16, 17), na hutupa kumbukumbu sahihi ya udhihirisho wa karama ya unabii, na jinsi kazi ya kweli ya Roho wa Mungu inavyoweza kutofautishwa na matendo ya Shetani pamoja na karama zake bandia.
GSAM 300KANUNI ZA KUTAMBUA KARAMA ZA KWELI
GSAM 300.3Bwana ametoa katika neno lake angalau kanuni saba tofauti, ambazo kwazo udhihirisho wa kweli wa Roho wa Mungu unaweza kutofautishwa na kazi ya Shetani.
GSAM 300Kanuni ya Kwanza—Maagizo Maalumu
GSAM 300.4Nabii Isaya, akisema juu ya mambo yaliyopo katika siku za mwisho, anasema: “Uufunge ushuhuda, uitie muhuri sheria kati ya wanafunzi wangu. Nami nitamngojea Bwana, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia.... Na watakapowaambia, Tafuteni habari kwa wenye pepo wa utambuzi na kwa wachawi waliao kama ndege na kunong’ona; je! haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! watafute habari kwa wafu kwa ajili ya walio hai? Waende kwa sheria na kwa ushuhuda; wasiposema sawasawa na neno hili, ni kwa sababu hamna nuru ndani yao.”5
GSAM 301.1Katika andiko hili, fikira zinaelekezwa kwa watu wanaojishughulisha na kurudisha muhuri katika sheria ya Mungu—watu wanaomngojea Bwana, wakijishughulisha na huduma yake. Wanamtazamia; yaani, wanatazamia kuja kwake—tena katika wakati ambapo roho zinazodai kuwa ni roho za wafu zinawaomba watu watafute habari kwao. Wengine wanaitikia wito wao na kutafuta maarifa kwa wafu; lakini Bwana anawaalika watu wake wamtafute yeye. Kwa kweli, hiyo ni kusema kwamba wakimtafuta atawapa maagizo maalumu. Hawana haja ya kutafuta habari kwa wafu, ambao hawawezi kuwapa habari yoyote; kwa maana “wala hawana tena sehemu milele katika jambo lolote linalofanyika chini ya jua;” na “wafu hawajui neno lolote.”6
GSAM 301.2Katika andiko lililo juu imetolewa kanuni ambayo kwayo ujumbe wote unapaswa kujaribiwa,—“wasiposema sawasawa na neno hili, ni kwa sababu hamna nuru ndani yao.” Ujumbe wote unaotoka kwa Bwana utasema kwa kupatana na neno lake na sheria yake.
GSAM 301.3Nikiitumia kanuni hii kwa maandishi ya Bibi White, ningesema kwamba katika miaka hamsini na miwili iliyopita nimesoma shuhuda zake kwa makini, nikizilinganisha na sheria ya Mungu na ushuhuda wa Biblia, nami naona upatano ulio kamili kabisa kati ya hivi viwili. Maagizo yake hayaji kutoa ufunuo wowote mpya utakaoshika nafasi ya Maandiko, bali yanatuonyesha ni wapi na jinsi gani, katika nyakati hizi, watu wanavyoweza kupotoshwa na kuongozwa mbali na neno. Nafasi ya shuhuda za Bibi White inaweza kuelezwa vizuri zaidi kwa yale ambayo yeye mwenyewe ameandika kuzihusu:—
GSAM 301.4“Neno la Mungu linatosha kuangaza akili iliyotiwa giza kupita zote, nalo linaweza kueleweka na wale wenye tamaa yoyote ya kulielewa. Lakini, pamoja na hayo yote, wengine wanaodai kulifanya neno la Mungu kuwa somo lao wanaonekana wakiishi kinyume kabisa na mafundisho yake yaliyo wazi zaidi. Basi, ili wanaume na wanawake wasiwe na udhuru, Mungu hutoa shuhuda zilizo wazi na zinazolenga jambo lenyewe, akiwarudisha kwenye neno ambalo wamepuuza kulifuata.
GSAM 302.1“Neno la Mungu limejaa kanuni za jumla za kujenga mazoea sahihi ya maisha, na shuhuda, za jumla na za mtu mmoja mmoja, zimekusudiwa kuelekeza fikira zao hasa kwenye kanuni hizi.... Hamfahamu Maandiko vizuri. Kama mngelifanya neno la Mungu kuwa somo lenu, mkiwa na tamaa ya kufikia kipimo cha Biblia na kuufikia ukamilifu wa Kikristo, msingezihitaji shuhuda....
GSAM 302.2“Bwana anakusudia kuwaonya, kuwakemea na kuwashauri kupitia shuhuda zilizotolewa, na kuzikazia akili zenu umuhimu wa ukweli wa neno lake. Shuhuda zilizoandikwa hazikusudiwi kutoa nuru mpya, bali kukazia kwa nguvu mioyoni ukweli uliofunuliwa tayari kwa uvuvio.... Hakuna ukweli wa ziada unaotolewa, bali Mungu, kupitia shuhuda, amerahisisha kweli kuu zilizokwisha kutolewa, na kwa njia aliyoichagua mwenyewe ameziweka mbele ya watu, ili kuamsha akili zao na kuzikazia kweli hizo, wapate wote kuwa bila udhuru....
GSAM 302.3“Shuhuda hazikusudiwi kulidharau neno la Mungu, bali kulitukuza na kuzivuta akili kwalo, ili uzuri wa ukweli ulio rahisi kueleweka uwaguse wote.... Kama watu wanaodai sasa kuwa hazina ya pekee ya Mungu wangetii matakwa yake kama yalivyoelezwa katika neno lake, shuhuda maalumu zisingetolewa ili kuwaamsha watimize wajibu wao, na kuwakazia hali yao ya dhambi na hatari yao ya kutisha katika kupuuza kulitii neno la Mungu.”7
GSAM 302Kanuni ya Pili—Manabii wa Kweli
GSAM 302.4Tumekwisha kujifunza kwamba manabii wote wa kweli watasema kwa kupatana na sheria ya Mungu na ushuhuda wa neno lake. Mtume Yohana anatoa kanuni nyingine inayoeleza mafundisho ya manabii wa kweli. Anasema: “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu: Kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili ni ya Mungu; na kila roho isiyokiri kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili si ya Mungu; na hiyo ndiyo roho ya mpinga Kristo, ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwapo duniani.”8
GSAM 303.1Liangalieni kwa makini andiko lililotangulia. Halisemi kwamba yeyote akiriye kwamba Yesu Kristo “alikuja katika mwili,” bali “amekuja katika mwili;” yaani, kwamba huja kwa Roho wake na kukaa ndani yetu, akiitikia imani yetu. Kwa kweli, huu ndio ukweli mkuu wa injili, “Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.”9
GSAM 303.2Fundisho linalohusu maisha yetu linalopatikana katika maandishi yote ya Bibi White ni kwamba ni lazima Kristo awe Mwokozi anayekaa ndani yetu ikiwa tunataka kufanya maendeleo yoyote katika njia ya mbinguni. Maandishi yake hufundisha kwamba Kristo anahitajika kwanza, mwisho, na wakati wote. Ili kutoa mfano wa jambo hili, tunaelekeza fikira kwenye kitabu chake, Hatua za Kumwendea Kristo, ambacho zaidi ya nakala laki moja zimeuzwa katika lugha ya Kiingereza, bila kutaja maelfu ya nakala katika lugha kumi na nane za kigeni ambamo sasa kinachapishwa. Mchungaji wa Kanisa la Kipresbiteri, baada ya kukisoma kitabu hicho, aliagiza nakala zaidi ya mia tatu kwa washiriki wa kanisa lake na rafiki zake, naye akasema, “Kitabu hiki kimeandikwa na mtu anayemjua vizuri Bwana Yesu Kristo.”
GSAM 303Kanuni ya Tatu—Manabii wa Uongo
GSAM 303.3Yohana anatoa kanuni ya kutambua manabii wa uongo: “Hao ni wa ulimwengu; kwa hiyo hunena ya ulimwengu, na ulimwengu huwasikia.”10 Mafundisho ya manabii wa uongo yatapendeza moyo wa kimwili, badala ya kuitukuza njia ya kujikana nafsi na kuubeba msalaba. Manabii wa uongo watafundisha “mambo ya kupendeza,” badala ya kumtukuza “Mtakatifu wa Israeli.”11 Yeyote anayesoma hata kurasa chache za maandishi ya Bibi White anaweza kuona kwamba yanaelekeza katika kujikana nafsi na kuubeba msalaba, wala si ya namna ya kuupendeza moyo wa kidunia na wa kimwili.
GSAM 304Kanuni ya Nne—Mateso na Uvumilivu
GSAM 304.1Katika kufuatilia somo hili zaidi, tutayachukua kuwa kanuni ya nne maneno ya mtume Yakobo: “Ndugu zangu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana kuwa mfano wa kustahimili mateso na wa uvumilivu.”12 Tunaposoma habari za maisha ya manabii wale wa zamani, tunajifunza kwamba mojawapo ya majaribu yao makubwa zaidi lilikuwa kuona Israeli wakikataa au wakitenda kinyume na shuhuda zilizo wazi walizopewa. Uchunguzi mfupi wa nyakati hizo utaonyesha mara moja tabia ya manabii wa kweli na wa uongo pia. “Bwana wa majeshi asema hivi, Msiyasikilize maneno ya manabii wanaowatabiria; wanawafanya kuwa watu wa ubatili; hunena njozi ya mioyo yao wenyewe, wala si yatokayo katika kinywa cha Bwana.”13
GSAM 304.2Hakuna kitu katika maandishi ya Bibi White cha kumfanya msomaji kuwa mtu wa ubatili; bali, kama mtu mwingine alivyosema, “Nimepata faida kubwa ya kiroho mara zisizohesabika kutokana na shuhuda. Kwa kweli, sizisomi kamwe bila kujisikia nimekemewa kwa kukosa imani kwa Mungu, kukosa kujitoa kwake, na kukosa bidii katika kuokoa roho.” Basi, kwa hakika, matokeo ya shuhuda za Bibi White yanatofautiana sana na yale ya mafundisho ya manabii wa uongo, kama yalivyoelezwa na Yeremia.
GSAM 304.3Nabii anatuambia pia jinsi manabii wa uongo watakavyofundisha: “Huwaambia daima wale wanaonidharau, Bwana amesema, Mtakuwa na amani; na kila mtu aendaye kwa kufuata mawazo ya moyo wake mwenyewe humwambia, Hakuna mabaya yatakayowapata.”14
GSAM 304.4Kuhusu jinsi yalivyo mafundisho ya Bibi White katika shuhuda zake, nitanukuu maneno yafuatayo kutoka kwa msomaji mwenye makini:
GSAM 304.4“Nimesoma shuhuda zake zote tangu mwanzo hadi mwisho, nyingi kati yake mara nyingi, nami sijawahi kuweza kupata sentensi hata moja isiyo ya maadili katika shuhuda hizo zote, wala kitu chochote kisicho safi kabisa na cha Kikristo; hakuna kinachomwongoza mtu yeyote mbali na Biblia au mbali na Kristo; bali humo napata miito yenye bidii kubwa zaidi ya kumtii Mungu, kumpenda Yesu, kuyaamini Maandiko, na kuyachunguza daima. Ukaribu wa namna hiyo na Mungu, kujitoa kwake kwa bidii ya namna hiyo, na miito mizito ya namna hiyo ya kuishi maisha matakatifu, vinaweza tu kuchochewa na Roho wa Mungu.”
GSAM 305.1Mtu aliyezichunguza shuhuda zake kwa makini tangu mwanzo anaandika:
GSAM 305.1“Katika jambo la kushughulikia watu kwa uwazi na uaminifu, bila hofu wala upendeleo, nataka kushuhudia kwamba hakujakuwa na upungufu. Kama nia duni na mbaya ndizo zilizokuwa nguvu inayoongoza kazi hii, maneno ya kujipendekeza yangeshika nafasi ya shuhuda zinazochunguza mioyo na makemeo ya uaminifu. Uwazi wa kusema, makemeo ya uaminifu kwa mabaya, maneno ya huruma na kutia moyo kwa roho zinazotetemeka zinazohisi kumhitaji Mwokozi, na kwa wakosaji wanaotafuta kwa unyenyekevu kuyaacha makosa yao,—haya ndiyo mambo yaliyokuwa sehemu kubwa ya kazi zake. Ushuhuda wa Bibi White, ukikemea mabaya ya watu wengi aliowaona katika njozi, umetolewa kwa uaminifu mkubwa na kwa matokeo bora sana.”15
GSAM 305Kanuni ya Tano—Unabii wa Kweli Hutimia
GSAM 305.2Kuna kauli iliyotolewa na Musa kuhusu manabii wa kweli na wa uongo, inayopatikana katika sura ya kumi na nane ya Kumbukumbu la Torati. Anasema: “Tutalijuaje neno ambalo Bwana hakulisema? Nabii anenapo kwa jina la Bwana, ikiwa jambo hilo halifuati wala halitokei, hilo ndilo neno ambalo Bwana hakulisema, bali nabii huyo amelinena kwa kujikinai; usimwogope.”16
GSAM 305.3Jambo hilo hilo linapatikana pia katika maandiko yafuatayo: “Ni nani asemaye neno likatokea, ikiwa Bwana hakuliagiza?”17 Kuhusu nabii Samweli ilisemwa, “Yote ayasemayo hutimia hakika.”18 “Neno la nabii litakapotimia, ndipo nabii huyo atajulikana kwamba Bwana amemtuma kweli.”19
GSAM 306.1Sasa imepita miaka zaidi ya hamsini na mitatu tangu mwandishi alipomwona kwa mara ya kwanza Bibi E. G. White akiwa katika njozi ya unabii. Katika miaka hii ametoa kauli nyingi za unabii kuhusu mambo ambayo yangetokea. Baadhi ya matabiri haya yanahusu matukio yaliyokwisha kutimia, na baadhi yanaendelea kutimia, ilhali mengine bado ni ya wakati ujao. Kwa yale yanayohusu matukio yaliyopita au ya sasa, sijui hata mfano mmoja wa kutotimia. Baadhi ya matabiri yake yamekwisha kutajwa. Mengine yataonekana katika sura zinazofuata tunapoendelea na simulizi letu.
GSAM 306Kanuni ya Sita—Miujiza Si Kipimo cha Nabii wa Kweli
GSAM 306.2Waandishi wengi wa mambo ya dini wamesisitiza, na maelezo ya Maandiko yamesema, kwamba ishara ya nabii wa kweli ni kutenda miujiza. Hatujaona bado katika Maandiko kanuni ya namna hii.
GSAM 306.3Ikiwa kutenda miujiza ni uthibitisho wa nabii wa kweli, basi yule “nabii wa uongo” aliyetajwa katika Ufunuo 19:20 angetangazwa hatimaye kuwa nabii wa kweli; kwa maana imesemwa, “Mnyama akakamatwa, na pamoja naye yule nabii wa uongo aliyefanya miujiza mbele yake, ambayo kwa hiyo aliwadanganya wale walioipokea chapa ya mnyama.” Mamlaka hiyo hiyo inatajwa tena katika Ufunuo 13:14 kuwa inawadanganya “wale wakaao juu ya nchi kwa miujiza ile aliyopewa uwezo wa kuifanya mbele ya mnyama.” Kwa kuitumia kanuni hii vivyo hivyo, tungelazimika kukata shauri kwamba hata Shetani ni nabii wa kweli. Roho fulani zitakazofanya kazi maalumu wakati wa pigo la sita kati ya mapigo saba ya mwisho zinaitwa “roho za mashetani, zifanyazo miujiza, ziwaendeazo wafalme wa dunia na wa ulimwengu wote, kuwakusanya kwenye vita vya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.”20
GSAM 306.4Ikiwa uthibitisho wa nabii wa kweli unapatikana katika miujiza anayoifanya wakati hayumo katika njozi, tungepata manabii wachache tu wa Biblia ambao wangeweza kuthibitika kwa kipimo hicho, hasa ikiwa uamuzi utategemea yale yaliyoandikwa kuhusu matendo yao. Ni kweli kwamba imeandikwa kuwa baadhi ya manabii walitenda miujiza, kama vile Eliya, Elisha, na Paulo. Lakini ni nani aliyepata katika Biblia kumbukumbu ya miujiza ya Isaya, Yeremia, Danieli, Hosea, Yoeli, Amosi, na wengineo? Hata hivyo, hawa walikuwa manabii wa kweli wa Bwana, nao wanathibitishwa kuwa hivyo kwa kanuni ambazo Bwana ametoa kuwa kipimo cha nabii wa kweli.
GSAM 307.1Kwamba kutenda miujiza si kipimo cha nabii wa kweli kunaonekana wazi kwa kusoma habari za Yohana Mbatizaji zilizo katika Maandiko. Kwamba alikuwa nabii kunaonyeshwa na unabii wa baba yake, Zekaria, alipokuwa akieleza njozi ambayo Mungu alikuwa amempa kuhusu mwana ambaye angezaliwa kwake: “Nawe, mtoto, utaitwa nabii wa Aliye Juu; kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana kumtengenezea njia zake.”21 Mwokozi wetu mwenyewe alimtambua Yohana kuwa ndiye nabii yule ambaye angemtengenezea njia mbele yake; kwa maana alisema juu ya Yohana: “Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii. Huyu ndiye aliyeandikiwa, Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Kwa maana nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna nabii aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji?”22
GSAM 307.2Basi hapa tuna kauli iliyo wazi ya Mwokozi kwamba Yohana alikuwa nabii. Na tutumie kipimo cha kutenda miujiza tuone matokeo yake. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohana mwinjilisti, tuna maneno haya: “Na wengi wakamwendea [Kristo], wakasema, Yohana hakufanya muujiza wowote; lakini mambo yote aliyoyasema Yohana juu ya mtu huyu yalikuwa kweli.”23 Kauli hii peke yake inabatilisha kabisa dai kwamba ishara ya nabii wa kweli ni kutenda miujiza.
GSAM 307.3Kanuni hii iliyotolewa katika Kumbukumbu la Torati 13:1-3, ambayo tunaiita kanuni ya sita katika hesabu yetu ya sasa, inatukinga tusikimbilie kufuata jambo lolote la ajabu au la miujiza mpaka tuwe tumechunguza kwanza kwa makini kama linaelekea kutusogeza karibu zaidi na Bwana au kutuvuta mbali naye. Kwa kweli, andiko hili linatuambia tutumie kanuni zote, hasa tuangalie kama jambo hilo linapatana na Mungu na sheria yake.
GSAM 308.1Kanuni hii ya sita inafundisha kwamba muujiza ukitendwa na mtu anayejifanya kuwa mtumishi wa Mungu, utakapoangaliwa kwa makini, itaonekana kwamba pamoja nao kuna kuziacha kweli takatifu za neno la Mungu, na kushusha kipimo ili kuuridhisha moyo unaoelekea kuikwepa njia ya kujikana nafsi. Bwana humruhusu mtu wa namna hiyo atokee, na mwenendo wake ni jaribu kwa mtoto wa kweli wa Mungu, ukimpa nafasi ya kupima kwa makini mwelekeo au nia ya huyo mtenda miujiza. Wale wanaolishikilia neno la Mungu, badala ya kuvutwa na mtenda miujiza huyo wa uongo, hutoka katika hali hiyo wakiwa na nguvu katika Mungu kutokana na jambo hilo walilopitia.
GSAM 308.2Katika siku hizi mbaya, ambapo wengi wanadai kuwa “waponyaji kwa imani,” “waponyaji kwa uwezo wa Mungu,” “waponyaji wa Sayansi ya Kikristo,” na wengineo, ingefaa kutumia kanuni za Maandiko kwa uangalifu mkubwa; kwa maana zitahitajika kanuni za Mungu na mwangaza wa Roho Mtakatifu ili tuweze kutambua wazi nia na kusudi la baadhi ya “waponyaji” hawa, jinsi kazi yao ilivyo ya hila nyingi; na kwa upande mwingine wapo wale wanaopuuza waziwazi sheria ya Mungu na ukweli wake kwa wakati huu. Katika visa fulani “waponyaji” hawa wa kujifanya wamewaka hasira kama watu waliojaa wazimu hata sheria ya Mungu inapotajwa tu. Kama ilivyo hakika kwamba Bwana ana ujumbe unaoitangaza sheria yake takatifu, ndivyo ilivyo hakika kwamba watu wanaoitukana sheria yake, na kuwafukuza mbele yao wale wanaoitaja tu, hawana uvuvio wa Roho Mtakatifu.
GSAM 308Kanuni ya Saba—Matunda Yao
GSAM 308.3“Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, lakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika michongoma? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; bali mti mbaya huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Basi mtawatambua kwa matunda yao.”24
GSAM 309.1Maneno haya ya Mwokozi wetu yanatambua ukweli kwamba karama ya unabii ingekuwapo katika nyakati za injili. Kama hakuna manabii wa kweli ambao wangehusika na kazi hiyo, na kila udhihirisho wa unabii ungetoka katika chanzo kiovu, je! asingesema, “Jihadharini na manabii”? Kwamba anatuambia waziwazi namna kila aina inavyoweza kutambuliwa ni ushahidi bora kabisa kwamba katika kazi ya Mfariji, Roho Mtakatifu, ya kuonyesha “mambo yajayo” (Yohana 16:13), kungekuwapo karama ya kweli ya unabii. Kanuni hii, ambayo katika hesabu yetu tumeiita kanuni ya saba, ni ya hakika isiyokosea. Kristo hakusema mnaweza kuwatambua kwa matunda yao, bali alisema kwa hakika, “mtawatambua kwa matunda yao.”
GSAM 309.2Tunauliza, Ni matunda gani yatakayoonekana katika kazi ya karama za kweli za Roho wa Mungu? Jibu linapatikana katika kauli ya Paulo kuhusu kusudi la Bwana katika kuliwekea kanisa karama: “Kwa hiyo asema, Alipopaa juu, aliteka mateka, akawapa wanadamu karama.... Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, kwa kazi ya huduma, kwa kuujenga mwili wa Kristo; hata sisi sote tutakapoufikia umoja [“kuingia katika umoja,” pambizoni] wa imani na wa kumjua Mwana wa Mungu, kufikia mtu mkamilifu, kufikia kipimo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”25
GSAM 309.3Itumie kanuni hii kwa karama ya unabii ambayo imehusishwa na ujumbe wa malaika wa tatu tangu mwanzo wake, na matokeo ni nini?—Tunaona kwamba maagizo yaliyotolewa daima kupitia Bibi White yameelekeza kwenye umoja na upatano, yakihimiza “kushauriana,” na “kushikamana,” ili kuwa katika upatano na Kristo, na hivyo kuhakikisha ushirika wa kweli na umoja kati ya mtu na mwenzake.
GSAM 310.1Baadhi ya wapinzani wa kazi hii wamesema kwa dhihaka, “Kama si njozi za Bibi White, mlizo nazo kati yenu, kazi yenu ingesambaratika zamani.” Jibu ni kwamba, “Hiyo ni kweli; kwa sababu kupitia chanzo hicho Bwana ametoa mashauri, maonyo, na nuru, na hivyo mafarakano yameondolewa, na kazi imesitawi.” Kwa hiyo walichokusudia kuwa shambulio dhidi ya karama hiyo, kwa kweli ni ushuhuda kwamba matunda yake ni yale ya karama ya kweli ya unabii.
GSAM 310.2Kwa miaka sitini na zaidi udhihirisho wa karama ya unabii kupitia Bibi White umejaribiwa kwa kanuni hizi saba, na katika kila jambo umetimiza masharti yanayotakiwa kwa unabii wa kweli.
Maelezo ya chini ya ukurasa
- Waefeso 4:11-13. ↩
- Yoeli 2:28, 29. ↩
- 1 Wathesalonike 5:20, 21. ↩
- Ufunuo 16:14. ↩
- Isaya 8:16-20. ↩
- Mhubiri 9:6, 5. ↩
- Shuhuda kwa Kanisa, Juz. 5, kur. 663-667. ↩
- 1 Yohana 4:1-3. ↩
- Waefeso 3:17; Wakolosai 1:27. ↩
- 1 Yohana 4:5. ↩
- Isaya 30:10, 11. ↩
- Yakobo 5:10. ↩
- Yeremia 23:16. ↩
- Mstari wa 17. ↩
- J. N. Andrews, katika Mapitio na Mbiu la Desemba, 1867. ↩
- Kumbukumbu la Torati 18:21, 22. ↩
- Maombolezo 3:37. ↩
- 1 Samweli 9:6. ↩
- Yeremia 28:9. ↩
- Ufunuo 16:14. ↩
- Luka 1:76. ↩
- Luka 7:26-28. ↩
- Yohana 10:41. ↩
- Mathayo 7:15-20. ↩
- Waefeso 4:8-13. ↩