Sura ya 6 — Ujumbe na wajumbe
GSAM 108.1“Iandike njozi, uiweke wazi juu ya mbao, ili aisomaye apate kukimbia. Kwa maana njozi hii bado ni kwa wakati uliowekwa, lakini mwisho wake itanena, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa maana hakika itakuja, haitakawia.”1
GSAM 108.2“Nami nikamwona malaika mwingine akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubirie hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa, na kabila, na lugha, na jamaa, akisema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumpa utukufu; kwa maana saa ya hukumu yake imekuja; nanyi msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.”2
GSAM 108.3Wale waliotangaza ujio wa pili walidai kwamba “njozi” hii pamoja na wakati wake “uliowekwa,” uliotajwa na nabii Habakuki, ilijumuisha njozi za unabii wa Danieli na za mwandishi wa Ufunuo. Walizieleza wazi sana kwa kuzionyesha katika chati zao za unabii, hata kwamba aliyesoma tafsiri yake angeweza kweli “kukimbia” na kuwajulisha wengine.
GSAM 108Ujumbe Bayana
GSAM 108.4Tangazo la Waadventista halikuwa tu lile alilotoa Paulo mbele ya Feliksi, “Haki, kiasi, na hukumu itakayokuja;” wala halikuwa lile alilotoa Martin Luther baada ya kumaliza kutafsiri Biblia, aliposema, kama ilivyoripotiwa, muda mfupi kabla ya kifo chake, “Nimesadiki kwamba hukumu haiko mbali; naam, kwamba Bwana mwenyewe hatakawia zaidi ya miaka mia tatu mingine.” Wala halikuwa lile alilosema John Wesley, kwamba “alidhani ile miaka elfu ingeweza kuanza baada ya karibu miaka mia moja.” Waadventista walidai kwamba walikuwa wakitoa ujumbe uliowakilishwa kwa mfano katika Ufunuo 14:6, 7, “Saa ya hukumu yake imekuja,” na kilio cha Ufunuo 10:6, “Wakati hautakuwapo tena.” Unabii kama huo usingeweza kutimizwa kwa tangazo la tukio ambalo “lingekuja,” likija “baada ya miaka mia tatu,” au “baada ya miaka mia moja,” bali kwa wakati ulio wazi, “imekuja.” Ujumbe wa namna hiyo hasa, ukiweka wakati wazi kama unabii huo ulivyotaka, ulitangazwa na Waadventista kwa ulimwengu wote.
GSAM 109Hukumu Wakati wa Kuja kwa Kristo
GSAM 109.1Wakati ujumbe huu ulipotangazwa kwa mara ya kwanza, kila dhehebu la Kikristo liliamini kwamba hukumu ingetokea wakati wa kuja kwa Kristo mara ya pili. Basi, watu waliokuwa katika hali hizo, wakitoa ujumbe kwamba saa ya hukumu imekuja huku wakiwa na imani hiyo, bila shaka wangetangaza kuja kwa Kristo mara ya pili. Kwa kweli, kilichoupa ujumbe nguvu na kuigusa mioyo ya watu kwa nguvu kubwa zaidi kilikuwa tangazo la wakati uliowekwa wazi. Kwanza walidai kwamba mwisho wa dunia ungekuja wakati fulani katika “mwaka wa Kiyahudi” wa 1843, na kwamba huo ulikuwa muda kati ya Machi 21, 1843, na Machi 21, 1844. Baada ya muda huo kupita, tunasoma katika Kilio cha Usiku wa Manane cha mwaka wa 1844 kwamba siku hususa iliwekwa kwa ajili ya mwisho wa nyakati za unabii. Hii ilikuwa siku ya kumi ya mwezi wa saba wa Kiyahudi, iliyolingana na Oktoba 22, 1844.
GSAM 109Kuhesabu Siku 2300
GSAM 109.2Msingi wa wakati huo—1843—ulikuwa siku 2300 za Danieli 8. Ilidaiwa kwamba, kwa kuwa “siku” hizi zilihusiana na unabii ambao ndani yake wanyama walichaguliwa kuwakilisha falme, “siku” lazima zitumike kwa mfano kuwakilisha miaka, kulingana na tafsiri ya Bwana ya wakati wa mfano, kama ilivyotolewa katika Hesabu 14:34 na Ezekieli 4:5, 6; kwamba yale majuma sabini—siku 490—ya Danieli 9 yangekuwa sehemu ya kwanza ya siku 2300, na kwamba vipindi hivyo viwili vilianza pamoja. Tukio lililotajwa katika Danieli 9, lililoonyesha mwanzo wa majuma sabini, lilikuwa “kutolewa kwa amri ya kuutengeneza upya na kuujenga Yerusalemu.” Amri hiyo ilitolewa katika mwaka wa saba wa Artashasta Longimanus, mwaka wa 457 K.K., kama ilivyoandikwa katika Ezra 7.
GSAM 110.1Kwamba hiyo ilikuwa tarehe ya kweli ya mwanzo wa majuma sabini kulithibitishwa na jambo hili: baada ya majuma sitini na tisa hasa—miaka 483—tangu mwaka wa 457 K.K., yaani mwaka wa 27 B.K., Kristo alibatizwa na Yohana na kuanza huduma yake, akisema, “Wakati umetimia,”3 na kadhalika. Mwanzo wa huduma ya Kristo, mwaka wa 27 B.K., kusulubiwa kwake miaka mitatu na nusu baada ya tarehe hiyo, “katikati [kwenye nusu] ya juma [la sabini],” mwisho wa kazi maalumu miongoni mwa Wayahudi, mwaka wa 34 B.K., na kuongoka kwa Sauli upesi baada ya hapo, yule mtume kwa Mataifa, vilithibitisha kwamba majuma sabini yaliishia kweli katika tarehe hiyo, na kwa hiyo kwamba yalianza mwaka wa 457 K.K. Walihesabu hivi: Ukiondoa 457 kutoka 2300, hubaki 1843. Na kwa kuwa ile miaka 457 ilikuwa kabla ya Kristo, tunafikia mwisho wa 1843 kuwa mwisho wa siku 2300.
GSAM 110Mambo Waliyokiri Wapinzani
GSAM 110.2Imesemwa kwa kweli kwamba “mambo yanayokiriwa kwa kuunga mkono ukweli na wale walio katika safu za wapinzani wake hutoa ushahidi ulio bora kuliko wote.” Hakuna mpinzani yeyote wa ujumbe wa ujio wa pili aliyewahi kudokeza kwamba hukumu ya upelelezi ya watu wa Bwana ilikuwa tukio ambalo lingetokea kabla ya kuja kwa Kristo; bali katika jambo hili walifikiri kwa kupatana na Waadventista. Ili kuthibitisha kauli hii tunanukuu wapinzani wawili mashuhuri.
GSAM 110.3Bwana N. Colver, akihubiri katika Kanisa la Mtaa wa Marlboro, Boston, mwaka wa 1842, kwa kuwapinga Waadventista, alisema:—
GSAM 111.1“Ikiwa siku hizi ni miaka, dunia itaisha mwaka wa 1843; mtoto yeyote wa shule anaweza kuliona hilo; kwa maana ikiwa ile 490 iliishia katika kifo cha Kristo, siku 2300 zingeishia mwaka wa 1843; nayo dunia lazima iishe, isipokuwa kama inaweza kuonyeshwa kwamba tukio jingine litafanyika, nami sioni jinsi hilo linavyoweza kufanywa.”
GSAM 111.2Profesa Stuart, karibu na wakati huohuo, alisema:
GSAM 111.2“Ni jambo la ajabu kwamba wafafanuzi walio wengi sana katika Uingereza na Marekani wamezoea kwa miaka mingi kuzifahamu siku zilizotajwa katika Danieli na Ufunuo kuwa viwakilishi, au mifano, ya miaka. Nimeona kuwa vigumu kutafuta chimbuko la desturi hii iliyoenea sana, ambayo karibu naweza kusema inafuatwa na wote.”
GSAM 111Ushuhuda wa Profesa Bush
GSAM 111.3Profesa Bush alisema: “Yeyote anayempinga Bwana Miller katika hoja yake ya wakati, humpinga katika hoja yake iliyo na nguvu zaidi. Wakati wake ni sahihi; lakini amekosea kuhusu tukio litakalotokea.” Bush aliamini kwamba ulimwengu wote ungeongoka kabla ya kuja kwa Kristo. Wazo lake lilikuwa kwamba ile miaka elfu ingeanza mwaka wa 1844.
GSAM 111.4Wachungaji wa imani ya ujio wa pili walifundisha katika hotuba zao za hadharani kwamba historia ya ulimwengu ilionyesha mataifa mbalimbali yakiwa katika hali ileile iliyowakilishwa na sanamu ya Danieli 2, wakati jiwe lingepiga sanamu miguuni, naye Mungu wa mbinguni angesimamisha ufalme wake; na katika sura ya 7, wakati “ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme chini ya mbingu zote vitapewa watakatifu wa Aliye Juu.” Pia walielekeza fikira za watu kwenye jambo hili: ishara—katika maumbile, katika siasa, na katika maadili—zilikuwa sawasawa na zile ambazo Maandiko yalitabiri kwamba zingeonekana wakati Bwana alipokuwa karibu kuonekana.
GSAM 111Maajabu Mbinguni
GSAM 111.5Bwana asema kwa njia ya nabii Yoeli: “Nami nitaonyesha maajabu mbinguni na duniani, damu, na moto, na nguzo za moshi. Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja ile siku ya Bwana iliyo kuu na yenye kutisha.”4 Waadventista waliamini na kufundisha kwamba nuru ya anga la kaskazini ya karne za hivi karibuni (kwa kawaida huitwa mianga ya kaskazini) ilikuwa ule “moto na nguzo za moshi” unaopatana na maelezo ya nabii; na kulingana na habari bora zaidi zilizoweza kupatikana katika historia (tunarejelea Ensiklopidia ya Edinburg kuwa ushahidi), ilikuwa imeonekana mara chache sana kabla ya kipindi hicho.
GSAM 112.1Hivyo, wakati ujumbe wa kuja upesi kwa Bwana ulipokuwa ukienda kwenye sehemu za mbali kabisa za dunia, ishara zilionyeshwa mbinguni ambazo ziliupa ukweli nguvu na kuvuta fikira za watu.
GSAM 112.2Mnamo Januari 25, 1837, kulikuwa na mwonekano mzuri ajabu wa nuru ya anga la kaskazini yenye mfano wa moto, ambao ulionekana kuelekeza mawazo ya wengi moja kwa moja kwenye utabiri wa nabii Yoeli kuhusu yale ambayo yangetangulia siku kuu ya Bwana. Maelezo yafuatayo ya tukio hilo yametolewa katika Mtangazaji wa Biashara wa New York la Oktoba 22, 1839. Yanapatana kabisa na tukio hilo kama mwandishi alivyolishuhudia huko Victor, Kaunti ya Ontario, N.Y.
GSAM 112Nuru ya Anga Yenye Mfano wa Moto ya 1837
GSAM 112.3“Jioni ya Januari 25, 1837, mwonekano wa ajabu wa matukio hayohayo [yaani nuru ya anga la kaskazini] ulionekana katika sehemu mbalimbali za nchi, kama wasomaji wetu watakavyokumbuka bila shaka. Mahali ambapo ardhi ilikuwa imefunikwa na theluji, mandhari ilikuwa ya kuvutia na ‘ya kutisha’ kwa namna ambayo haikuwa imepata kuonekana. Katika mahali pamoja, karibu na mlima, watu walioshuhudia tukio hilo walitujulisha kwamba lilifanana na ‘mawimbi ya moto yaliyokuwa yakibingirika kuteremka mlimani,’ na kwa ujumla, kadiri ilivyojulikana, theluji iliyofunika ardhi ilionekana kama moto uliochanganyika na damu, huku juu (kama asemavyo mtume), ‘mbingu zikiwaka moto,’ zilifanana sana na maelezo ya unabii kuhusu siku ya mwisho hata wengi wakastaajabu; watoto waliolitazama waliogopa, wakauliza kama hukumu ilikuwa inakuja; na hata wanyama walitetemeka wakionyesha hofu kubwa.”
GSAM 113.1Haikuwa Marekani peke yake ambapo ishara hii ya nabii Yoeli ilionyeshwa, bali mafundisho ya kuja kwa Bwana yalipokuwa yakijulikana zaidi huko Uingereza, ishara hiyohiyo ilionyeshwa mbinguni katika nchi hiyo. Mtangazaji wa Biashara wa New York la Oktoba 22, 1839, linanukuu yafuatayo kutoka magazeti ya London kuhusu tukio la ajabu lililoshuhudiwa katika nchi hiyo usiku wa Septemba 3:—
GSAM 113Nuru ya Anga ya 1839
GSAM 113.2“LONDON, SEPTEMBA 5 [1839].—Kati ya saa nne usiku wa Alhamisi na saa tisa alfajiri ya jana, mbinguni kulionekana mojawapo ya mionekano mizuri ajabu zaidi ya matukio haya ya pekee, nyota zinazoanguka na mianga ya kaskazini, iliyoshuhudiwa katika miaka mingi iliyopita. Dalili ya kwanza ya tukio hili la ajabu ilionekana dakika kumi kabla ya saa nne usiku, wakati kitu cha rangi nyekundu hafifu, kilichoonekana kama mvuke, kilipopanda kutoka upande wa kaskazini wa nusu ya anga, na kuenea polepole hadi katikati ya mbingu; na ilipofika saa nne au saa nne na robo usiku, anga lote, kutoka mashariki hadi magharibi, lilikuwa kama shuka moja kubwa la nuru. Mwonekano wake ulikuwa wa kutisha sana, ukafanana kabisa na ule unaosababishwa na moto mkubwa wa kuogofya. Nuru ilibadilika sana; wakati mmoja ilionekana kushuka, na mara baada ya hapo ikapanda ikiwa na mwangaza mkali. Ndani yake yalionekana mafungu ya moshi yaliyobingirika tena na tena, na kila mtazamaji alionekana kusadiki kwamba ulikuwa ‘moto mkubwa sana.’
GSAM 113.3“Hofu iliyoukumba mji mkuu ilikuwa kubwa sana; maelfu ya watu walikuwa wakikimbia kuelekea kule walikodhani msiba huo wa kutisha ulikuwa umetokea. Mitambo ya kuzimia moto ya vituo vya wazimamoto katika Mtaa wa Baker, Mtaa wa Farringdon, Mtaa wa Watling, Barabara ya Waterloo, na vilevile ile ya vituo vya magharibi mwa London—kwa kweli, kila mtambo wa kuzimia moto katika London—ilifungwa kwa farasi na kupelekwa kwa mbio kuelekea mahali palipodhaniwa kuwa ‘eneo la maangamizi’ kwa juhudi zisizo za kawaida, ikifuatwa na magari, wapanda farasi, na makundi makubwa ya watu. Baadhi ya mitambo hiyo ilifika mpaka High Gate na Halloway [karibu maili nne] kabla ya kosa hilo kugunduliwa. Mionekano hii iliendelea kwa zaidi ya saa mbili, na kulipokaribia kupambazuka mandhari ikawa ya fahari.
GSAM 114.1“Ilipofika saa nane usiku, tukio hilo lilionyesha mandhari nzuri ajabu, ambayo ilikuwa vigumu sana kuieleza. London yote iliangazwa kama wakati wa adhuhuri, na hewa ilikuwa safi ajabu. Nusu ya anga upande wa kusini, katika wakati uliotajwa, ingawa haikuwa na mawingu, ilikuwa na giza sana; lakini nyota, zilizokuwa hazihesabiki, ziling'aa kwa uzuri. Upande wa mbingu ulioelekeana nao ulikuwa na tofauti ya ajabu lakini nzuri sana; ulikuwa safi kupita kiasi, na nuru ilikuwa angavu sana; vimondo vilifuatana bila kukoma, vikitofautiana katika uzuri wa mwangaza—vilionekana kufanyizwa katikati ya mbingu, vikaenea mpaka vikaonekana kupasuka. Mwonekano huo ulisisimua sana. Nyota ndogo zisizohesabika zilichomoka juu ya upeo wa macho na kuruka kwa kasi sana kuelekea duniani hata jicho likashindwa karibu kufuatilia njia yake; nazo pia zilionekana kupasuka na kutandaza mvuke mwekundu uliokolea juu ya nusu yote ya anga. Rangi zilikuwa nzuri ajabu.
GSAM 114.2“Ilipofika saa nane na nusu usiku, mandhari iligeuka kuwa giza, ambalo lilipotawanyika lilifunua upinde wa mvua wenye nuru kwenye kilele cha mbingu, na kuzunguka ukingo wa giza lililoning'inia juu ya sehemu ya kusini ya nchi. Muda mfupi baadaye, nguzo za nuru yenye rangi ya fedha zilienea kutoka humo. Ziliongezeka ajabu, zikichanganyika na mvuke mwekundu uliotokea wakati huohuo, na zilipofikia urefu wake wote, mandhari ilipita yote ambayo mtu angeweza kuwaza. Nyota zilikuwa zikiruka kwa kasi kuelekea kila upande, na zikaendelea mpaka saa kumi alfajiri, wakati vyote vilipotoweka.”
GSAM 114Mionekano ya Ajabu Katika Jua
GSAM 114.3Wakati wahubiri walio hai walipokuwa wakieleza ukweli wa kuja kwa Bwana, maajabu mengi na ya namna mbalimbali yalionekana mbinguni katika sehemu mbalimbali za ulimwengu. Kati ya hayo, nafasi tuliyo nayo itaturuhusu kuonyesha tu mchoro wa mwonekano wa jua huko Norwich, Uingereza, katika Desemba, 1843. Mwonekano wa namna hiyo ulitokea New Haven, Conn., Septemba 9, 1844, kwa saa mbili kabla na baada ya adhuhuri, nao ukashuhudiwa na maelfu ya watu.
GSAM 115Mwonekano wa Ajabu wa Jua
GSAM 115.1Duara dogo la ndani linawakilisha jua. Lilikuwa na rangi hafifu ya machungwa. Sehemu ya nje ya yale maduara mawili yaliyolizunguka jua, yakiwa katika umbali usio sawa kutoka kwake, ilionekana kuwa na rangi hiyohiyo; lakini sehemu ya ndani ya maduara hayo ilikuwa ya manjano iliyokolea, anga ndani ya maduara hayo likionekana kuwa na rangi ya kahawia yenye giza, na yale maduara matatu makubwa yaliyopita kwenye jua na chini yake yalionekana kama nuru angavu iliyo dhahiri.
GSAM 115.2Kuhusu tukio la Uingereza, tunasoma yafuatayo katika barua ya E. Lloyd, London, Januari 3, 1844:—
GSAM 115.3“Kumekuwa na ‘ishara katika jua’ ya ajabu, iliyoonekana na watu mashuhuri wa Norwich na wa maeneo yanayozunguka, ambayo namna yake haijapata kuonekana Uingereza hapo awali. Ilionekana Desemba iliyopita, karibu saa sita mchana, na ikaendelea kwa saa mbili. Iliwatia wakazi hofu kubwa. Ilitokea kabla tu ya Ndugu Winter, Burgess, na Routon kuanza kazi yao ya umishenari katika mji huo. Ilionekana kuandaa njia kwa ajili ya ukweli, hata wakapata mafanikio mazuri huko.”
GSAM 116.1Habari ya tukio hilo kama lilivyotokea New Haven, Conn., imetolewa katika Kilio cha Usiku wa Manane cha Oktoba 10, 1844, nayo ilichukuliwa kutoka gazeti la New Haven Palladium la Septemba 10, 1844. Katika habari iliyo katika Kilio mhariri anasema, “Hakuna mwanafalsafa aliyeweza kutoa maelezo ya sababu ya tukio hili ambayo yanamridhisha yeye mwenyewe.”
GSAM 116.2Habari ya mandhari hii iliyoonekana kuhusiana na jua huko New Haven, Conn., Septemba 9, 1844, ilichapishwa pia katika gazeti la Hartford Courant la Septemba 12, 1844, nayo inasema hivi:—
GSAM 116.3“Pete zilizolizunguka jua Jumatatu, Septemba 9, 1844, kwa saa mbili kabla na baada ya adhuhuri, zaonekana kuwa zilitazamwa kwa hamu kubwa na wakazi wetu kwa ujumla, nazo zimeamsha shauku ya kutaka kufahamu zaidi kuhusu mionekano ya namna hiyo na sababu yake.
GSAM 116.4“Duara hili la nuru lilikuwa la pekee kwa muda lililodumu, na lilitoa nafasi nzuri za kulitazama. Karibu na adhuhuri, lilikuwa hasa na pete mbili kamili, moja yenye upana wa karibu nyuzi arobaini na tano, ikilizunguka jua lililokuwa katikati yake, na nyingine yenye upana wa karibu nyuzi sabini na mbili, ikiwa na kitovu chake kwenye kilele cha anga, huku mzingo wake ukipita kwenye jua. Duara dogo liliambatana na umbo la duaradufu lenye mhimili mrefu na lililokengeuka kidogo tu kutoka umbo la duara. Moja kwa moja upande ulioelekeana na jua, na nyuzi thelathini na sita kaskazini mwa kilele cha anga, duara kubwa lilikatizwa na maduara mengine mawili yenye vipenyo vilivyokaribia au vilivyolingana kabisa na kipenyo chake, yakifanyiza mahali yalipokutana doa angavu, kama ambavyo kwa kawaida lingetokana na nuru ya pete tatu zenye mwangaza iliyoungana. Pete iliyolizunguka jua ilionyesha rangi za upinde wa mvua, mara nyingi zikiwa angavu na nzuri sana. Pete nyingine zilikuwa nyeupe na hafifu zaidi kadiri zilivyokuwa mbali zaidi na jua. Hata hivyo, sehemu ndogo za maduara zenye rangi za mche [za upinde wa mvua] zilionekana nyakati mbalimbali, mashariki na magharibi pia.... Ulinganifu kama huo wa umbo lazima utegemee sheria fulani inayoongoza kufanyizwa kwa maduara ya nuru; lakini namna ya sheria hiyo haijaelezwa kikamilifu.... Hakujawa na ugumu mkubwa katika kueleza kufanyizwa kwa pete inayolizunguka jua, kwa kuwa sababu yake inafanana kwa kiasi fulani na ile inayofanyiza upinde wa mvua, lakini imekuwa vigumu zaidi kueleza chimbuko la pete ambayo mzingo wake unapita kwenye kitovu cha jua.”
GSAM 117Maajabu Yanayotimiza Utabiri wa Maandiko
GSAM 117.1Tunaweza kufahamu jinsi maajabu haya yaliyoonekana mbinguni yalivyotumiwa, huko Uingereza na Amerika, kwa kusoma Ufafanuzi wa Sura ya Ishirini na Nne ya Mathayo, wa Sylvester Bliss, uliochapishwa Boston mwaka 1843. Baada ya kunukuu baadhi ya masimulizi yaliyotajwa hapo juu, anasema hivi:—
GSAM 117.2“Hivyo, ‘ishara kubwa’ na ‘mambo ya kutisha’ yaliyotabiriwa katika Maandiko ya kweli yaonekana kuwa yametimizwa yote, pamoja na yale ambayo Mwokozi alisema yangetangulia kuja kwake.
GSAM 117.3“Kama vile kuchipua kwa majani ya miti kulivyo ishara ya hakika ya majira ya joto, vivyo hivyo, ishara hizi zinapotimia, Wakristo wanapaswa kujua kwa hakika kwamba kuja kwa Kristo kumekaribia, hata milangoni. Si ruhusa tu ya kujua jambo hilo, bali Mwokozi wetu anawaamuru walijue.”5
GSAM 117WAJUMBE
GSAM 117.4Baada ya kuelekeza fikira kwenye baadhi ya mambo makuu ya ujumbe wa ujio wa pili kama ulivyohubiriwa hapo mwanzo, huenda ikapendeza kuwatazama wachache wa wale waliokuwa na sehemu maarufu katika tangazo hilo kuu. Tayari tumetaja majina ya wengi waliokuwa miongoni mwa wachungaji wenye vipawa vikubwa zaidi wa wakati huo katika nchi za nje, waliotoa kilio hicho. Tunapoelekeza fikira kwa baadhi ya wale walioongoza huko Amerika, ambao Bwana aliwatwika mzigo wa kazi, itaonyesha zaidi kwamba mkono wa Bwana ulikuwa kweli katika vuguvugu hilo.
GSAM 118William Miller
GSAM 118.1Kwanza tutamtazama William Miller, ambaye alikuwa maarufu sana katika vuguvugu la ujio wa pili huko Marekani, kiasi kwamba kwa watu wengi vuguvugu hilo linajulikana tu kama “Umilleri.”
GSAM 118.2William Miller alizaliwa Pittsfield, Mass., mwezi Februari, 1782. Tangu utotoni mwake, alionyesha dalili za uwezo na uchangamfu wa akili uliopita kiwango cha kawaida. Kadiri miaka michache ilivyopita, dalili hizo zilizidi kuwa dhahiri kwa wote walioshirikiana naye. Alikuwa na mwili imara, akili changamfu iliyokua vizuri kiasili, na tabia isiyolaumika. Alikuwa amepata manufaa machache yaliyotolewa na shule ya wilaya kwa miaka michache tu, ndipo watu kwa jumla wakakubali kwamba maarifa yake yalizidi yale ya walimu waliokuwa wakiajiriwa kwa kawaida.
GSAM 118.3Bwana Miller alioa mwaka 1802, akakaa Poultney, Vt. Wanaume alioshirikiana nao tangu alipohamia Poultney, ambao pia walikuwa wamemsaidia sana katika mambo ya maisha haya, walikuwa wameathiriwa sana na kanuni za kushuku mambo ya dini na nadharia za udeisti. Hawakuwa watu wenye mwenendo mbaya; kwa ujumla walikuwa raia wema, na kwa kawaida walikuwa watu wenye mwenendo wa kiasi, wenye huruma na ukarimu. Hata hivyo, waliikataa Biblia kuwa kipimo cha kweli ya dini, nao wakajitahidi kufanya kuikataa kwao kuonekane kuwa na msingi, kwa msaada wowote walioweza kupata katika maandiko ya Voltaire, Hume, Volney, Paine, Ethan Allen, na wengine. Bwana Miller aliyasoma maandiko hayo kwa makini, na hatimaye akajitangaza kuwa mdeisti. Yeye mwenyewe amesema kwamba maisha yake ya udeisti yaliendelea kwa miaka kumi na miwili, kuanzia karibu mwaka 1804.
GSAM 118.4Baada ya kupewa cheo cha kapteni, alijiunga na jeshi mwaka 1810. Aliporudi kutoka jeshini, aliihamishia familia yake Low Hampton, N.Y., ili aanze kazi ya kilimo huko mwaka 1812. Akiwa mkulima, alikuwa na nafasi zaidi ya kusoma. Aliona kwamba maoni yake ya udeisti hayakumpa uhakika wowote wa furaha baada ya maisha haya ya sasa. Ng'ambo ya kaburi kila kitu kilikuwa giza na huzuni. Kwa maneno yake mwenyewe:
GSAM 118.4“Wazo la kutoweka kabisa lilikuwa baridi na la kutia hofu, na kuwajibika kulimaanisha maangamizi ya hakika kwa wote. Mbingu zilikuwa kama shaba juu ya kichwa changu, na dunia kama chuma chini ya miguu yangu. Umilele!—ulikuwa nini? Na kifo!—kwa nini kilikuwapo? Kadiri nilivyozidi kufikiri kwa hoja, ndivyo nilivyozidi kuwa mbali na uthibitisho. Kadiri nilivyofikiri, ndivyo mahitimisho yangu yalivyozidi kutawanyika. Nilijaribu kuacha kufikiri, lakini sikuweza kuyadhibiti mawazo yangu. Kwa kweli nilikuwa mwenye taabu, lakini sikuelewa sababu yake.... Muda mfupi baadaye, ghafla tabia ya Mwokozi ilijidhihirisha wazi sana katika akili yangu. Ilionekana kwamba huenda akawapo mmoja aliye mwema na mwenye huruma hata awe tayari kufanya upatanisho yeye mwenyewe kwa makosa yetu, na hivyo kutuokoa tusipate adhabu ya dhambi. Mara moja nilihisi jinsi ambavyo mmoja wa namna hiyo angepaswa kupendeka; nikawaza kwamba ningeweza kujitupa mikononi mwake, na kuitumainia rehema yake.”
GSAM 119Kuongoka kwa William Miller
GSAM 119.1Alisema zaidi:
GSAM 119.1“Niliona kwamba Biblia ilimwonyesha Mwokozi wa namna ileile niliyomhitaji; nami nilishangaa jinsi kitabu kisichovuviwa kingeweza kufunua kanuni zilizofaa kikamilifu mahitaji ya ulimwengu ulioanguka dhambini. Nililazimika kukubali kwamba Maandiko lazima yawe ufunuo kutoka kwa Mungu. Yakawa furaha yangu; na katika Yesu nikampata rafiki.... Sasa Biblia ikawa jambo kuu nililojifunza, nami naweza kusema kwa kweli kwamba niliichunguza kwa furaha kubwa. Niligundua kwamba hata nusu yake sikuwa nimeambiwa. Nilishangaa kwa nini sikuwa nimeona uzuri na utukufu wake hapo awali, na nikastaajabu kwamba niliweza kuikataa wakati wowote.”
GSAM 119.2William Miller mwenyewe anaeleza hivi jinsi alivyojifunza Biblia:
GSAM 119.2“Niliazimia kuweka kando mawazo yangu yote niliyokuwa nayo tayari, kulinganisha kwa makini andiko na andiko, na kuendelea kujifunza kwa utaratibu na mpango.... Kila nilipokuta jambo lisilo wazi, desturi yangu ilikuwa kulilinganisha na vifungu vyote vinavyohusiana nalo; na kwa msaada wa Cruden, nilichunguza maandiko yote ambamo yalipatikana maneno yoyote muhimu yaliyokuwa katika sehemu yoyote isiyo wazi.... Kwa njia hii niliendelea kujifunza Biblia kwa karibu miaka miwili katika kuisoma kwangu yote kwa mara ya kwanza, nami nikaridhika kabisa kwamba yenyewe ndiyo mfasiri wake.
GSAM 120.1“Nilipokuwa nikijifunza hivyo, niliridhika kwamba, ikiwa unabii uliotimizwa zamani ni kipimo chochote cha kuamua namna utakavyotimizwa ule ambao bado ni wa wakati ujao, basi maoni yaliyoenea kuhusu utawala wa kiroho wa Kristo—kipindi cha miaka elfu duniani kabla ya mwisho wa ulimwengu, na kurudi kwa Wayahudi—hayaungwi mkono na neno la Mungu.... Niliona Maandiko yakifundisha wazi kwamba Yesu Kristo atashuka tena katika dunia hii, akija katika mawingu ya mbinguni, katika utukufu wote wa Baba yake.
GSAM 120.2“Nilipata furaha katika kujifunza Maandiko ambayo sikuwahi kudhani ingeweza kupatikana katika mafundisho yake. Nilianza kuyasoma bila kutarajia kupata wakati wa kuja kwa Mwokozi, na mwanzoni nilipata shida kuamini matokeo niliyokuwa nimefikia; lakini ushahidi ulinigusa kwa nguvu sana hata sikuweza kupinga usadikisho wangu. Nikawa karibu nimethibitika kabisa katika mahitimisho yangu, nikaanza kungojea, kukesha na kuomba kwa ajili ya kuja kwa Mwokozi.”
GSAM 120.3Tena anasema:
GSAM 120.3“Niliamini; na mara moja wajibu wa kulitangaza fundisho hili, ili ulimwengu uamini na kujiweka tayari kumlaki Hakimu na Bwana Arusi wakati wa kuja kwake, ukawekwa moyoni mwangu. Sihitaji hapa kutoa maelezo ya kina kuhusu majaribu yangu marefu na makali. Inatosha kusema kwamba, baada ya miaka kadhaa, nililazimishwa na Roho wa Mungu, nguvu ya kweli na upendo kwa roho za watu, kuuchukua msalaba wangu na kuyatangaza mambo haya kwa ulimwengu unaokufa na kuangamia.”
GSAM 120.4Bwana Miller, kama wale waliochochewa na ujumbe huu katika nchi nyingine, alifikiri kwanza kutimiza agizo alilopewa kwa kuandika na kuchapisha katika magazeti ya umma na katika vijitabu. Alichapisha maoni yake kwa mara ya kwanza katika Telegrafu ya Vermont, gazeti la Wabaptisti lililochapishwa Brandon, Vt. Hii ilikuwa mwaka 1831. Alizungumza hadharani kwa mara ya kwanza juu ya jambo hili mwaka 1832. Kuhusu mkutano huu alisema, “Bwana alimimina neema yake juu ya kusanyiko, na wengi wakaamini hata kuokolewa kwa roho zao.”
GSAM 121.1Mwaka 1836 mihadhara yake ilichapishwa katika baadhi ya magazeti ya umma ya wakati huo. Katika majira ya baridi ya 1837-38 mihadhara yake ilitolewa katika kijitabu. Mwaka 1838 kijitabu cha pili chenye kurasa 204 kilichapishwa, na katika kijitabu hicho Bwana Miller alisema kwamba mamlaka ya Waothmani huenda ingeanguka mwaka 1839 au 1840. Mihadhara yake ya kwanza katika miji mikubwa ilikuwa mwaka 1836. Wakati huo alizungumza katika miji ya Randolph, Lowell, Groton, na Lynn, Mass.
GSAM 121.2Hadi mwaka 1840, Bwana Miller alikuwa karibu peke yake kama msemaji wa hadharani juu ya ukaribu wa ujio wa Kristo. Katika mwaka huo, ghafla mamia wakajiunga naye kutangaza ujumbe. Kilicholeta badiliko hili kubwa kitaelezwa katika sura inayofuata. Katika majira ya baridi ya 1839-40, Bwana Miller alitoa mfululizo wa mihadhara huko Exeter, N.H. Huko alikutana kwa mara ya kwanza na Mchungaji J. V. Himes, ambaye wakati huo aliikubali imani hiyo, na tangu siku hiyo akasimama bega kwa bega na Mchungaji Miller akiwa mchapishaji na mhubiri mwenye bidii wa ujumbe mkuu wa ujio wa pili.
GSAM 121Joshua V. Himes
GSAM 121.3Kuhusu mtendakazi huyu mwenye bidii katika vuguvugu hili kuu, jambo bora tunaloweza kufanya ni kunukuu mwandishi wa wasifu wake, anayesema hivi:—
GSAM 121.4“Joshua V. Himes alizaliwa Wickford, R.I., tarehe 19 Mei, 1805. Baba yake alijulikana sana kama mfanyabiashara aliyefanya biashara na Visiwa vya Karibi, naye alikuwa mshiriki maarufu wa kanisa la Kiaskofu la Mtakatifu Paulo huko Wickford. Mama yake alikuwa na tabia ya upole na upendo kwa Mwokozi, ambao aliumimina katika masikio ya mwanawe aliyekuwa tayari kusikiliza.
GSAM 121.5“Baba alikuwa amekusudia kumsomesha mwanawe, Joshua, kwa ajili ya huduma ya kanisa ambalo yeye mwenyewe alishiriki, lakini hali hazikumruhusu. Mungu alikuwa na kazi nyingine ya kumpa mwana huyo, naye alikuwa akipanga mambo kwa namna ambayo ingeleta matokeo yaliyokusudiwa. Mwaka 1817 baba alituma shehena ya thamani chini ya usimamizi wa Kapteni Carter, huku Alexander Stewart akiwa msimamizi wa biashara ya shehena. Watu hawa hawakuwa waaminifu, na walipofika bandari moja ya Visiwa vya Karibi, waliuza meli pamoja na shehena, wakakimbia. Tukio hili lilibadili mipango yote iliyokuwa imefanywa kwa ajili ya maisha ya baadaye ya kijana Joshua, ambaye alitarajiwa kupelekwa Chuo Kikuu cha Brown, huko Providence, R.I. Badala yake, mwezi Aprili, 1821, alipelekwa New Bedford, Mass., akawekwa kwa William Knights kwa mkataba wa uanagenzi ili ajifunze ufundi wa kutengeneza samani.
GSAM 122.1“Alipofika katika makao yake mapya, alianza kwa bidii kazi aliyopewa, akiwa ameazimia kuwa stadi katika ufundi wake. Hata hivyo, upesi aliona kwamba mazingira yake ya kidini hayakulingana kikamilifu na mapendeleo yake. Anasema, ‘Bwana wangu alikuwa mfuasi wa Uyunitariani, naye alinipeleka kanisani kwake. Mchungaji Orville Dewey ndiye aliyekuwa mchungaji. Alikuwa ameiacha imani ya kimapokeo karibuni. Mafunzo niliyopata chini ya Askofu Griswold na Mchungaji William Burge, msimamizi wa kanisa la Mtakatifu Paulo, Wickford, na kumsikiliza mara nyingi Dkt. Crocker, msemaji mwenye ufasaha wa kanisa la Mtakatifu Yohana, huko Providence, R.I., yalinifanya nisiweze kabisa kukubali namna Bwana Dewey alivyokanusha kwa ufasaha mafundisho ya Kristo na mitume wake.’
GSAM 122.2“Kwa kuwa wakati huo hakukuwa na kanisa la Kiaskofu huko New Bedford, aliamua kuhudhuria Kanisa la Kwanza la Kikristo [si la Wanafunzi], na baadaye akajiunga na kundi hilo. ‘Hapa,’ anasema, ‘nilikuta Biblia iliyofunguliwa na uhuru wa kufikiri, nami nikavitumia vizuri vyote viwili.’ Kanisa hili lilikuwa chini ya uchungaji wa Mchungaji Moses Howe. Mchungaji Clough alimbatiza Joshua V. Himes tarehe 2 Februari, 1823. Akiwa na moyo uliowaka kwa bidii kwa ajili ya Bwana wake, alianza mara moja, akiwa na umri wa miaka kumi na minane, kusimulia habari za msalaba na kuwahimiza watu watubu. Anasema hivi kuhusu yeye mwenyewe:—
GSAM 122.3“‘Upesi nikawa mtoa mawaidha, nikapewa kibali cha kuendeleza karama yangu.... Nilimaliza muda wangu wa uanagenzi kwa njia ya kuridhisha, nikapokea pongezi. Lakini kwa miaka mitano au sita nilikuwa na desturi ya kufanya kazi zaidi ya iliyotakiwa, na hivyo nikapata siku moja au mbili kwa juma kwa ajili ya kujifunza na kufanya kazi ya umishenari katika mitaa yenye uhitaji, nami nikamkabidhi mchungaji wangu matunda ya kazi hiyo.’
GSAM 123.1“Mwaka 1825 alitumwa kuwa mmishenari wa konferensi ya makanisa ya Kikristo kusini mwa Massachusetts. ‘Hakukuwa na mpango wala fedha za kuwategemeza wamishenari,’ anasema Mchungaji Himes, ‘nami nikaazimia kufanya biashara ili nijitegemeze, na kuhubiri kadiri nilivyoweza.’
GSAM 123.2“Mwaka 1828 aliondoka New Bedford, akiwa na azimio ambalo bila shaka lingeleta ushindi, bila mashaka wala upungufu wa nguvu, akaenda Plymouth, ambako alihubiri neno la Mungu katika majengo ya shule, katika vyumba vilivyotayarishwa kwa muda, na popote alipoweza kupata watu wa kumsikiliza. Mwaka 1829 aliendelea na kazi ya namna hiyo huko Fall River hadi mwaka 1830, alipohamia Boston akiwa mchungaji wa Kanisa la Kwanza na la Pili la Kikristo; naye akakaa huko kwa miaka thelathini na mitatu. Mwaka 1839 alikubali imani ya ujio wa pili, kama ilivyoelezwa na Mchungaji William Miller aliyekuwa maarufu. Aliingia katika kazi hii mpya kwa shauku yote aliyokuwa nayo, na huduma zake zilijaa moto na nguvu. Mwaka 1840 alianza kuchapisha Ishara za Nyakati, akitetea kazi ambayo alikuwa ameitoa moyo wake wote kuitumikia. Fedha zake zote, kazi yake yote na nguvu zake zote zilitolewa kwa ajili ya kazi hii, na maelfu ya watu wakaongoka.”
GSAM 123Kazi za Pamoja za Miller na Himes
GSAM 123.3Kuanzia mwaka 1840 hadi majira ya kupukutika kwa majani ya 1844, Wachungaji Miller na Himes walifanya kazi kwa pamoja kwa sehemu kubwa, walipokuwa wakitoka mji hadi mji, wakati wa majira ya joto wakiwa na hema lao kubwa sana, na wakati wa baridi katika makanisa na kumbi za umma. Nguvu nyingi za mwili za Mchungaji Himes zilimhifadhi hadi alipoingia mwaka wake wa tisini na mbili. Uwezo wake wa akili ulikuwa imara hadi mwisho. Tarehe 28 Septemba, mwaka 1894, alitoa hotuba iliyogusa mioyo sana kwa kusanyiko la Waadventista Wasabato zaidi ya elfu tatu katika uwanja wa makambi huko Lansing, Michigan. Alionekana kusema kwa bidii na nguvu nyingi kama za siku za zamani. Kwa kweli hili lilikuwa jambo la ajabu kwa mtu ambaye alikuwa ameingia mwaka wake wa tisini na moja miezi mitatu iliyopita, tena aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa usiotibika ambao ulisababisha kifo chake mwaka uliofuata.
GSAM 124.1Wachungaji Miller na Himes walisimama kana kwamba katika “mstari wa mbele wa vita” katika vuguvugu la ujio wa pili huko Amerika, nao walikuwa wawili tu kati ya makumi ya watu waliofanya kazi pamoja nao kutangaza fundisho la ujio wa Kristo, ambao sifa zao kuu zilikuwa uthabiti wa kusudi na uadilifu thabiti. Kwa sehemu kubwa, watu hawa walikuwa wa kundi ambalo ulimwengu huwaita “watu waliojiendeleza kwa juhudi zao wenyewe,”—watu waliokua kwa kukutana na hali ngumu za maisha, waliokuwa wamejifunza kuamua thamani ya jambo kwa kufuata kanuni badala ya kuangalia manufaa yao. Walikuwa wa tabia ile ambayo Mchungaji Miller alisema ilikuwa ya wale waliokuwa kwa kawaida wakiukubali ujumbe kutoka makanisani, “washiriki waliokuwa wacha Mungu zaidi, waliojitoa zaidi, na wenye uzima wa kiroho zaidi.” Jambo hili lilithibitishwa na wachungaji wa makanisa mbalimbali, waliosema, baada ya Waadventista kujitenga nao kabisa, “Hili [fundisho] limewachukua walio bora zaidi katika kundi letu.”
GSAM 124Wahubiri Wengine Maarufu Waadventista
GSAM 124.2Huenda ikapendeza kutaja kwa majina baadhi ya watu waliokuwa na sehemu maarufu pamoja na Wachungaji Miller na Himes katika vuguvugu la siku zile za mwanzo. Anayeongoza orodha ni Charles Fitch, wa Cleveland, Ohio, ambaye mwaka 1842 alipendekeza wazo la kuwa na chati za kueleza njozi za Danieli na Ufunuo. Wazo hili lilitokana na Habakuki 2:2, 3. Charles Fitch alifariki tarehe 10 Oktoba, 1844.
GSAM 124.3Dkt. Josiah Litch, wa Philadelphia, ambaye, kama tutakavyoona katika sura inayofuata, alichochewa na Bwana kutangaza kweli ambayo kutimia kwake kulifanya shauku ya ujumbe wa ujio wa pili ikue ghafla na kwa haraka.
GSAM 124.4Elon Galusha, wa Lockport, N.Y., mchungaji maarufu wa Kibaptisti, ambaye maandiko na huduma zake kuhusu ukaribu wa kuja kwa Bwana ziliamsha mvuto mkubwa katika dhehebu hilo.
GSAM 125.1E. R. Pinney, wa Seneca Falls, N.Y., mchungaji mwingine aliyejitoa wa kanisa la Kibaptisti, ambaye huduma na maandiko yake vilikuwa na nguvu katika kazi. Kwa kufaa angeweza kuitwa “Chumvi ya dunia.”
GSAM 125.2Geo. Storrs, wa Jiji la New York, ambaye kabla ya kuikubali imani ya ujio wa pili alikuwa mhubiri maarufu wa uamsho. Maandiko yake yalikuwa na mvuto mkubwa katika kuwachochea watu wajitoe zaidi, wao wenyewe na mali zao, kwa ajili ya kazi; hasa ilikuwa hivyo katika majuma ya mwisho ya siku 2300. Ni yeye ambaye, baada ya kukatishwa tamaa, aliwasilisha kwa Waadventista na ulimwengu mahubiri yake sita kuhusu asili ya mwanadamu, hali ya wafu, na adhabu ya wakati ujao ili wayatafakari.
GSAM 125.3Mchungaji Stockman, wa Portland, Maine, alikuwa mtendakazi mwingine mwenye bidii katika mikutano ya uamsho ya William Miller katika mji huo. Alifariki majuma machache kabla ya mwisho wa mwaka wa Kiyahudi wa 1843, wakati Waadventista walipokuwa wakitumaini na kutarajia kwamba Bwana angekuja wakati huo.6
GSAM 125.4Kulikuwa na watu wengine maarufu ambao tutawataja tu kwa kukosa nafasi, kama vile N. N. Whiting, aliyefanya tafsiri ya Agano Jipya katika Kiingereza, inayojulikana kama Tafsiri ya Whiting; S. S. Snow, F. G. Brown, Apollos Hale, L. D. Mansfield, Geo. Needham, O. R. Fassett; George, Wesley, na Edwin Burnham (ndugu watatu), wote wakiwa watendakazi wenye uwezo katika ujumbe.
Maelezo ya chini ya ukurasa
- Habakuki 2:2, 3. ↩
- Ufunuo 14:6, 7. ↩
- Marko 1:14, 15, ↩
- Yoeli 2:30, 31. ↩
- Ufafanuzi wa Sura ya Ishirini na Nne ya Mathayo, kur. 49-60. S. Bliss, Boston, Mass., 1843. ↩
- Ni rahisi kuona, kama ilivyoelezwa katika Maandiko ya Awali, uk. 17, kwa nini Wachungaji Fitch na Stockman walikuwa na shauku ya kujua yaliyotokea tangu walipolala. ↩