Sura ya 26 — Kazi yetu ya umishenari katika nchi za nje
GSAM 403.1“Imeandikwa, Wale ambao hawakuambiwa habari zake wataona; na wale ambao hawakusikia watafahamu.”1
GSAM 403.2Misheni yetu ya kwanza katika eneo lililo nje ya Marekani ilianzishwa mwaka 1874, wakati Mchungaji J. N. Andrews alipotumwa Uswisi na kuanza kazi huko.
GSAM 403ENEO LA KAZI LA ULAYA YA KATI
GSAM 403.3Wakati huo misheni hii ilijumuisha mataifa manane; yaani, Uswisi, Ufaransa, Italia, Uturuki, Ubelgiji, Hispania, Ureno na Ugiriki, eneo lenye watu 140,000,000.
GSAM 403.4Huenda ikapendeza kutaja hapa hali zilizowafanya watu wetu kuanza misheni katika eneo kubwa namna hii, wakati dhehebu lilikuwa bado na washiriki wachache.
GSAM 403Mchungaji Czechowski
GSAM 403.5Katika mwaka 1865, Mchungaji M. B. Czechowski, aliyekuwa kasisi Mkatoliki wa Kipolandi aliyeongoka na kuukubali ukweli wa sasa, alitamani watu wetu wamtume akiwa mmishenari katika Ulaya ya Kati. Kwa kuwa jambo hilo halikuwezekana wakati huo, aliwasilisha ombi lake kwa Waadventista wa siku ya kwanza ya juma huko Boston, Mass., ambao labda walimwona kuwa hana uhusiano wowote na watu wetu. Vyovyote ilivyokuwa, walipata fedha zilizohitajika, wakamtuma katika misheni aliyotamani.
GSAM 404Watunza Sabato nchini Uswisi
GSAM 404.1Mwaka 1866, alifundisha ukweli wa Sabato na ujumbe wa malaika wa tatu huko Tramelan, Uswisi, na jitihada hiyo ikatokeza kundi la watunza Sabato. Muda mfupi baadaye, aliwaacha ili aende kufundisha ujumbe huko Hungaria. Hakuliambia kundi la Tramelan chochote kuhusu kazi yetu huko Amerika, lakini Albert Vuilleumier, mmoja wao, aliweza kusoma Kiingereza. Kwa bahati, aliona nakala ya Mapitio ya Ujio wa Pili. Kwa njia hiyo mawasiliano kwa barua kati ya nchi hizo mbili yakaanza.
GSAM 404Mchungaji Erzenberger Atumwa Amerika
GSAM 404.2Mwaka 1869 James Erzenberger, wa Tramelan, alitumwa Amerika ili kujifunza lugha ya Kiingereza na kuyafahamu zaidi mafundisho na desturi za Waadventista wa Sabato. Alifika Battle Creek Juni 18, akakaa Amerika mwaka mmoja na nusu. Aliondoka New York katika safari yake ya kurudi Septemba 9, 1870. Mwezi Juni wa mwaka huohuo, Ademar Vuilleumier alitembelea nchi hii, ambamo alikaa miaka minne hivi. Aliporudi nyumbani kwao, alifuatana na Mchungaji Andrews. Walifika Neuchatel Oktoba 16, 1874.
GSAM 404.3Mwaka 1875, Mchungaji D. T. Bourdeau na familia yake waliondoka Amerika kwenda Ufaransa, ambako kamati ilikuwa imewateua kufanya kazi.
GSAM 404Gazeti la Kifaransa Laanzishwa
GSAM 404.4Mwaka uliofuata, mwezi Julai, 1876, huko Basel, Uswisi, uchapishaji wa gazeti la lugha ya Kifaransa ulianza, lenye jina Les Signes des Temps (Ishara za Nyakati). Mei 13, 1882, miaka sita baadaye, Mchungaji Haskell alisafiri kwa meli kutoka jiji la New York kwenda Ulaya. Katika safari hii ya umishenari, alikaa Uswisi kwa muda fulani.
GSAM 405Mchungaji Whitney Aenda Basel—Kifo cha Mchungaji Andrews
GSAM 405.1Julai 26, 1883, Mchungaji B. L. Whitney na familia yake walifika Basel, akiwa ameteuliwa na Kamati ya Konferensi Kuu kusimamia misheni hiyo, ili kumpunguzia mzigo Mchungaji Andrews, ambaye afya yake ilikuwa ikidhoofika haraka. Miezi michache baadaye, katika Oktoba ya mwaka huo, Mchungaji Andrews alifariki.
GSAM 405.2Katika ujana wake Mchungaji Andrews hakupata fursa za kusoma katika shule za juu na vyuo, lakini alikuwa na elimu nzuri, akiwa mtu ambaye ulimwengu humwita aliyejielimisha au kujijenga mwenyewe. Kwa kujituma katika masomo, alijua vizuri Kilatini, Kigiriki na Kiebrania, na katika miaka ya baadaye lugha ya Kifaransa. Alijifunza Kifaransa ili kimsaidie kuanzisha na kuendeleza kazi katika Misheni ya Ulaya ya Kati, ambako alifanya kazi katika miaka sita ya mwisho wa maisha yake, akiandikia na kuchapisha gazeti la Kifaransa la Ishara za Nyakati, na pia akihubiri katika lugha hiyo. Alikuwa akifanya kazi hiyo alipofikwa na mkono wa mauti.
GSAM 405Daktari Kellogg Barani Ulaya
GSAM 405.3Katika majira ya kuchipua ya mwaka 1883, Daktari J. H. Kellogg alitembelea Ulaya kwa ajili ya utafiti wa tiba. Alikaa siku chache katika kila moja ya misheni zetu, na ziara zake ziliwatia moyo sana watendakazi; hasa ushauri wake kuhusu kazi ya Basel ulithaminiwa sana na Mchungaji Andrews.
GSAM 405Mchungaji Butler Atembelea Ulaya
GSAM 405.4Katika Konferensi Kuu iliyofanyika Oktoba, 1883, ilipendekezwa kuanza uchapishaji wa gazeti nchini Uingereza haraka iwezekanavyo. Kutokana na uamuzi mwingine uliopitishwa katika mkutano huo, Wachungaji George I. Butler, M. C. Wilcox na A. C. Bourdeau walivuka bahari kwenda kusaidia kazi huko Ulaya na Uingereza. Mchungaji Butler alishuka Glasgow, Uskoti, Februari 27, 1884. Kusudi mojawapo la ziara ya Mchungaji Butler katika misheni za nchi za nje lilikuwa kujifunza, kwa kujionea mwenyewe, matatizo ya kuendeleza kazi katika nchi za nje na namna ya kuyashinda. Yeye pia alikaa kwa muda fulani Basel na katika eneo la Ulaya ya Kati. A. C. Bourdeau alifanya kazi miongoni mwa Wafaransa katika mabonde ya milima ya Alpi, miongoni mwa Wawaldo; naye M. C. Wilcox alijiunga na kazi ya uchapaji na uhariri nchini Uingereza, akakaa hadi mwisho wa mwaka 1886.
GSAM 406Nyumba ya Uchapishaji Yajengwa Basel
GSAM 406.1Mwaka 1884, nyumba ya uchapishaji, Imprimerie Polyglotte (jina lenye maana ya kuchapisha katika lugha nyingi), ilijengwa Basel. Mwezi Machi, 1885, H. W. Kellogg alipewa mamlaka na Kamati ya Konferensi Kuu kwenda Basel na kununua mashine zilizohitajika kwa kiwanda cha uchapaji. Alifanya hivyo, na kwa namna hiyo kiwanda cha uchapaji chenye vifaa vya kutosha, kilichomilikiwa na Waadventista wa Sabato, kikaanzishwa katika jiji la kale la Basel.
GSAM 406.2Wakati wa ziara ya Mchungaji Butler huko Ulaya, gazeti la Kijerumani lililoitwa Herold der Wahrheit (Mbiu ya Ukweli) lilichapishwa katika ofisi ya Basel. Mwaka huohuo jarida la Kiromania, Adevărulu Prezentu (Ukweli wa Sasa), pia lilichapishwa katika ofisi hiyo. Na bado jingine la Kiitaliano, lililoitwa L'Ultimo Messagio (Jumbe za Mwisho). Majarida hayo mawili yaliyotajwa mwisho yalikuwa ya kurasa kumi na sita na yalitolewa mara moja kila miezi mitatu. Katika Konferensi ya Uswisi, mwezi Oktoba, 1884, ilielezwa kwamba katika mwaka huo nakala 146,000 za majarida haya manne zilikuwa zimechapishwa na kusambazwa. Hadi mwaka 1895, wakati ofisi ya uchapaji (kwa sababu ya mateso huko Basel) ilipohamishwa kutoka jiji hilo kwenda Hamburg, Ujerumani, vitabu na vijitabu vilikuwa vimechapishwa katika lugha kumi na moja tofauti; yaani, Kifaransa, Kijerumani, Kiitaliano, Kiromania, Kihispania, Kibohemia, Kirusi, Kiholanzi, Kihungaria, Kiarmenia, Kituruki na Kituruki-Kigiriki. Kwa hiyo, kama jina lake lilivyoonyesha, ilikuwa taasisi ya “kuchapisha katika lugha nyingi.”
GSAM 407Bibi White Atembelea Ulaya
GSAM 407.1Septemba 3, 1885, Bibi White, mwanawe W. C. White na familia walifika Basel. Walikaa mwaka mmoja na nusu katika nchi za zamani, wakitembelea misheni zilizokuwa katika eneo la Ulaya ya Kati, ambako walitoa huduma yenye thamani isiyopimika kwa misheni mbalimbali.
GSAM 407Konferensi ya Uswisi Yaundwa
GSAM 407.2Septemba 10, 1885, Konferensi ya Uswisi iliundwa. Katika taarifa iliyotolewa wakati huo ilielezwa kwamba konferensi ilikuwa na mchungaji mmoja aliyewekewa mikono, wahubiri saba waliopewa kibali, makanisa kumi na washiriki 224. Hawa walilipa zaka ya $1,645.11 katika mwaka uliotangulia. Mbali na hiyo, michango ya $2,041.22 ilikuwa imetolewa kwa ajili ya kazi.
GSAM 407Mchungaji Waggoner Barani Ulaya
GSAM 407.3Bibi White, pamoja na W. C. White na familia, walirudi Amerika mwaka 1887. Mwaka huohuo Mchungaji J. H. Waggoner alialikwa kujiunga na Misheni ya Ulaya ya Kati. Alikaa zaidi ya miaka miwili katika eneo hili, akiishi Basel katika muda huo. Katika jiji hilo ndipo alipofariki, Aprili 20, 1889, kama ilivyoelezwa hapo awali.
GSAM 407.4Kudhoofika kwa afya ya Mchungaji Whitney, na kifo chake kilichofuata (Aprili 9, 1889), kulikuwa pigo jingine zito kwa misheni hii.
GSAM 407Mchungaji Robinson Barani Ulaya
GSAM 407.5Mchungaji D. A. Robinson, aliyekuwa akifanya kazi nchini Uingereza, alichaguliwa kuwa mrithi wa Mchungaji Whitney. Alifanya kazi kwa ufanisi katika eneo hili kwa miaka sita hivi, ndipo, kwa mwaliko wa Konferensi Kuu, alipoondoka kwenda India katika mwaka 1895. Kuondoka kwake kulifanya iwe lazima kuteua msimamizi mwingine.
GSAM 408Mchungaji Holser Msimamizi wa Eneo la Kazi
GSAM 408.1Mchungaji H. P. Holser ndiye aliyechaguliwa kwa nafasi hiyo, na pamoja na cheo hicho alichaguliwa kusimamia Misheni yote ya Ulaya ya Kati. Hapa alifanya kazi bila kuchoka na kwa ufanisi hadi mwaka 1901, wakati yeye pia aliposhindwa na madhara ya ugonjwa. Alifariki huko Canyon City, Colorado, Septemba 11, 1901.
GSAM 408.2Licha ya hali hizi ngumu, misheni ilikua na kazi ikasonga mbele, kama inavyoonyeshwa na taarifa iliyotolewa kwa Konferensi Kuu mwaka 1895, inayoeleza kwamba Konferensi ya Ulaya ya Kati ina makanisa kumi na tisa yenye washiriki 484, ambao walilipa zaka ya $4,378.18 katika mwaka uliotangulia. Wakati huo walikuwa na wachungaji wanne waliowekewa mikono na wahubiri watano waliopewa kibali.
GSAM 408MISHENI YA UJERUMANI NA URUSI
GSAM 408.3Mwaka 1870, J. H. Linderman, mchungaji wa kanisa lililo karibu na Elberfeld, Prusia, na washiriki arobaini wa kanisa hilo, walianza kuitunza Sabato ya siku ya saba kutokana na kujifunza Biblia, bila kujua kwamba kulikuwa na kundi jingine la Wakristo ulimwenguni waliokuwa wakiitunza siku hiyo kuwa Sabato. Habari za kundi hili ziliwafikia watu wetu kwa namna ya pekee. Mwombaji mmoja alifika katika nyumba ya misheni huko Basel siku ya Sabato. Familia ilikuwa ikijifunza somo la Shule ya Sabato, Biblia zikiwa zimefunguliwa mbele yao. Hali hiyo ilimvutia mtu huyo na kumfanya aulize maswali.
GSAM 408Kundi la Elberfeld
GSAM 408.4Alipojua kwamba hawakuwa Wayahudi, bali Wakristo waliokuwa wakiitunza Sabato ya siku ya saba, aliwaeleza habari za kundi hili la Elberfeld. Mchungaji Andrews aliona ni busara kuchunguza habari hiyo; kwa hiyo, akifuatana na Mchungaji Erzenberger, alikwenda Prusia mwanzoni mwa mwaka 1875, ambako walilikuta kundi kama walivyoelezwa. Mchungaji Erzenberger alibaki kwa muda akifanya kazi katika sehemu hiyo ya Ujerumani, na Januari 8, 1876, watu wanane walibatizwa huko Elberfeld, huo ukiwa ubatizo wa kwanza uliofanywa na Waadventista wa Sabato nchini Ujerumani.
GSAM 409.1Ukweli ulikuwa umepata nafasi nchini Urusi mapema tangu mwaka 1882, kupitia maandiko ya kusoma yaliyotumwa na ndugu Wajerumani huko Amerika kwa marafiki zao katika makoloni ya Wajerumani nchini Urusi.
GSAM 409Mchungaji Conradi Barani Ulaya
GSAM 409.2Mwaka 1885 Mchungaji L. R. Conradi aliondoka Amerika kwenda katika eneo la Ulaya ya Kati, kufanya kazi miongoni mwa Wajerumani. Juni 28, 1886, aliondoka Basel kwenda Krimea, Urusi. Huko, akifuatana na Mchungaji Perk, alisafiri kwenda Berdebulat, ambako dada wawili walibatizwa na kanisa lenye washiriki kumi na tisa likaundwa, hilo likiwa kanisa la kwanza la Waadventista wa Sabato nchini Urusi.
GSAM 409Wachungaji Conradi na Perk Wafungwa Gerezani
GSAM 409.3Mara tu baada ya hayo Wachungaji Conradi na Perk walikamatwa kwa kufundisha kinyume cha imani ya Kiorthodoksi, wakafungwa gerezani kwa majuma matano huko Perekop. Baada ya kuachiliwa kwake (kwa kuingilia kati kwa mwakilishi wa kidiplomasia wa Marekani), Mchungaji Conradi alitembelea Urusi ya Mashariki, kisha akarudi Uswisi.
GSAM 409Kazi Kwenye Volga, Urusi
GSAM 409.4Ilikuwa katika mwaka huohuo ambapo Mchungaji Laubhan alianza kufanya kazi nchini Urusi, karibu na nyumbani kwake, palipokuwa kwenye Mto Volga. Katika mwaka 1880, Mchungaji Klein, wa Kansas, alianza kazi katika sehemu za Wajerumani nchini Urusi, na kwa namna hiyo watendakazi wamepatikana kwa ajili ya eneo hili gumu lenye shida nyingi, na ingawa waumini wamepelekwa uhamishoni na kufungwa gerezani, Bwana ameibariki kazi kwa namna ya ajabu.
GSAM 409Mafanikio ya Wainjilisti wa Vitabu Nchini Ujerumani
GSAM 409.5Katika mwaka 1888, wainjilisti wa vitabu walianza kazi katika Prusia ya Rhine, Württemberg, Baden na Alsace. Watendakazi hao wanane au kumi wenye bidii na waaminifu walifanikiwa sana, hata katika mwaka mmoja idadi ifuatayo ya vitabu iliuzwa: Maisha ya Kristo, 3,000; Kutoka Edeni hadi Edeni, 2,000; na vijitabu 12,000. Kutokana na kazi hii, karibu kila mahali vitabu vilipouzwa na kusomwa, baadhi ya watu, mmoja au zaidi, waliukubali ukweli.
GSAM 410Misheni Yaanzishwa Hamburg
GSAM 410.1Mwezi Mei, 1889, kazi ya misheni ilianzishwa Hamburg, Ujerumani, na Mchungaji Conradi, na baada ya muda mfupi sana shule ya kuwafundisha watendakazi ilianzishwa. Oktoba iliyofuata Shule ya Sabato yenye washiriki ishirini na wanane iliundwa. Ilikuwa katika mwaka huu ambapo Mchungaji Haskell alitembelea misheni, kanisa lenye washiriki ishirini likaundwa, na ghala la vitabu likaanzishwa.
GSAM 410.2Wakati huo Mchungaji J. T. Boettcher alikuwa akishughulika na kazi miongoni mwa Wajerumani huko Barmen. Taarifa ilitolewa mwaka 1890 kwa Konferensi Kuu, ikieleza kwamba katika misheni ya Ujerumani na Urusi kulikuwa na makanisa tisa yaliyoundwa, yenye jumla ya washiriki 422, pamoja na watunza Sabato sabini na watano ambao bado hawakuwa wameundwa kuwa makanisa. Aprili 7 mwaka huohuo, wengine kumi na wawili walibatizwa na kujiunga na kanisa la Hamburg. Kufikia Desemba washiriki wa kanisa hili walikuwa wameongezeka hadi arobaini. Fedha zilizopatikana kwa mauzo ya vitabu kutoka ghalani, katika Hamburg, Uholanzi, Urusi na sehemu mbalimbali za Ujerumani, zilikuwa $5,000.
GSAM 410Mafanikio Barani Ulaya
GSAM 410.3Polepole lakini kwa hakika kazi ilisonga mbele katika Misheni ya Ulaya ya Kati, kama inavyoonyeshwa katika taarifa iliyotolewa kwenye Konferensi Kuu mwaka 1891. Wakati huo kulikuwa na makanisa matano nchini Ujerumani, yenye washiriki mia moja na arobaini, ambao sitini na wanne kati yao walikuwa washiriki wa kanisa la Hamburg. Zaka iliyolipwa ilikuwa $1,000. Vitabu vilivyouzwa melini na mmishenari wa meli huko Hamburg vilifikia thamani ya $500, nayo mauzo ya wainjilisti wa vitabu kwa mwaka huo katika eneo lote yalikuwa $6,000. Watu mia moja na hamsini walikuwa wameukubali ukweli nchini Austria, na nchini Urusi kulikuwa na makanisa kumi na matatu, yenye washiriki mia nne.
GSAM 411Watunza Sabato Watano wa Urusi Wapelekwa Uhamishoni
GSAM 411.1Karibu na wakati huo (1891), washiriki watano wa kanisa moja la Urusi, akiwemo kiongozi wao, walikuwa wamekamatwa kwa kufundisha mafundisho yaliyopingana na kanisa rasmi la nchi, na kuhukumiwa miaka mitano ya uhamisho huko ng'ambo ya Kaukazi. Walipaswa kufungwa pamoja kwa minyororo, na walitakiwa kutembea maili mia tano. Katika jaribu hili imani yao iliwategemeza, nao walikuwa na furaha katika Bwana. Katika mwaka huo kijitabu kilikuwa kimeandaliwa kwa namna ya masomo ya Biblia katika lugha ya Kirusi, kuhusu mateso ya Kristo, usingizi wa wafu, ni siku gani na kwa nini, na je, twaweza kujua?
GSAM 411.2Wakati wa Konferensi Kuu mwaka 1895, washiriki nchini Ujerumani walikuwa wameongezeka hadi 368, nayo zaka ya mwaka uliotangulia ilikuwa $2,327.43.
GSAM 411Watunza Sabato Zaidi Nchini Urusi
GSAM 411.3Nchini Urusi, ingawa wengi sana walikuwa wamehamia nchi nyingine, washiriki walikuwa wameongezeka hadi 467, ambao walilipa zaka ya $841.60.
GSAM 411.4Kutokana na maelezo yaliyotolewa na katibu wa misheni za nchi za nje katika somo la juma la maombi la mwaka 1896, tunajifunza kwamba
GSAM 411.4“katika eneo la Ujerumani na Urusi katika mwaka uliotangulia idadi yao ilikuwa imekaribia kuwa maradufu; idadi yao ikiwa imeongezeka kwa zaidi ya watu mia nne. Huko Berlin, Ujerumani, watu sitini walikuwa wakihudhuria ibada za kawaida za Sabato. Kujengwa kwa nyumba ya ibada ya misheni huko Hamburg kulikuwa kumeimarisha kazi huko. Huko Munich, Bavaria, watu kadhaa walikuwa wakisubiri ubatizo. Kulikuwa na waumini katika Leipsic, Königsberg, Magdeburg, Posen, Stuttgart na miji mingine mikubwa ya Ujerumani. Pia kulikuwa na kundi huko Rotterdam, Uholanzi.
GSAM 412.1“Nchini Urusi, wainjilisti wa vitabu walikuwa wamepata vibali kutoka serikalini. Machapisho yalikuwa yametafsiriwa katika lugha za Kilatvia na Kiestonia. Gazeti la Kijerumani lilikuwa limehamishwa kutoka Basel kwenda Hamburg, na katika ofisi hiyo walikuwa wakichapisha ukweli katika lugha kumi na nne.”
GSAM 412Ubatizo Nchini Hungaria
GSAM 412.2Katika mwaka huo ubatizo wa kwanza ulikuwa umefanyika nchini Hungaria, na mkutano wa kwanza wa maadhimisho ya maagizo ya Bwana huko Bohemia. Misheni ya meli ilikuwa imeanzishwa Galatz, nchini Romania, kwa ajili ya Danube na Bahari Nyeusi.
GSAM 412Uinjilisti wa Vitabu Nchini Ujerumani
GSAM 412.3Katika gazeti la Mmishenari wa Nyumbani la Desemba, 1895, Mchungaji Spies alisema kuhusu kazi ya uinjilisti wa vitabu katika eneo la Ujerumani,
GSAM 412.3“Wale waliokuwa wakisimamia kazi ya uinjilisti wa vitabu ilipoanzishwa katika eneo hili hawakuacha kuiendeleza, ingawa baadhi ya wachapishaji na wafanyabiashara wakuu wa vitabu huko Leipsic waliwaambia kwa uhakika kwamba ‘kuuza vitabu kwa kuandikisha wanunuzi kungeishia kushindwa.’
GSAM 412.4“Katika Agosti ya mwaka 1887 toleo la kwanza la Maisha ya Kristo lilitolewa katika lugha ya Kijerumani. Karibu na wakati kitabu hicho kilipokuwa tayari kusambazwa, mkutano wa mafunzo kwa wainjilisti wa vitabu ulifanyika Basel; huu ulikuwa mwanzo wa kazi ya uinjilisti wa vitabu nchini Ujerumani na pia katika Ulaya yote. Toleo la saba la kitabu hiki sasa limetoka katika mashine ya uchapaji katika lugha ya Kijerumani.
GSAM 412.5“Tangu Januari 1, 1895, wainjilisti wapya wa vitabu kumi na wawili wameingia katika eneo la kazi. Mwezi Juni, 1895, taarifa ilionyesha ongezeko la mauzo la asilimia hamsini. Kwa sasa jitihada ya pekee inafanywa kwa Herold der Wahrheit (Mbiu ya Ukweli), gazeti letu la Kijerumani. Baadhi ya makanisa yasiyo makubwa sana huchukua nakala hamsini hadi mia mbili, ambazo huziuza. Nao hupata mambo yenye kufurahisha sana katika kushughulika na wanunuzi. Katika Mapitio la Februari 18, 1896, Mchungaji Conradi alisema, ‘Tunaufunga mwaka 1895 tukiwa na watunza Sabato elfu moja na mia tano katika eneo la Ujerumani na Urusi.’”
GSAM 413MISHENI YA SKANDINAVIA
GSAM 413.1Kazi ya umishenari kwa watu wa Skandinavia ilianzishwa na Mchungaji John Matteson katika mwaka 1877. Tarehe 6 Juni alifika Vejle, katika Jyeland, Denmark. Alipokwenda katika nchi hiyo, kulikuwa na watu wachache waliokuwa wameanza kuitunza Sabato kwa kusoma magazeti na vijitabu walivyotumiwa na marafiki huko Amerika.
GSAM 413.2Tunapofuatilia mwanzo wa kazi hii, tunajifunza kwamba katika mwaka 1850, watu wanne waliokuwa wamehamia Amerika kutoka Norwei walianza kuitunza Sabato ya Bwana. Waliishi Oakland, Wisconsin. Wawili kati yao walikuwa baba na mama wa Mchungaji O. A. Olsen. Katika mwaka 1863 Mchungaji John Matteson alianza kuitunza Sabato ya siku ya saba. Aliishi Poysippi, Wisconsin. Katika miezi sita iliyofuata, kwa juhudi zake, watu wapatao arobaini wenye asili ya Denmark na Norwei walikubali mafundisho ya Waadventista wa Sabato. Mhubiri wa kwanza mwenye bidii aliyeungana naye katika huduma alikuwa Mchungaji J. F. Hanson wa Minnesota.
GSAM 413Kitabu cha Kwanza Kilichochapishwa kwa Kideni-Kinorwei
GSAM 413.3Katika mwaka 1866, Mchungaji John Matteson aliwaomba wasimamizi wa ofisi ya Mapitio na Mbiu ajue kama wangechapisha vitabu vidogo na vijitabu katika lugha ya Waskandinavia kwa ajili yao. Aliambiwa kwamba ukosefu wa fedha katika ofisi uliwazuia kufanya hivyo; lakini kulikuwa na watu wa taifa lake huko Wisconsin na Minnesota waliotamani sana ukweli uchapishwe katika lugha yao ya asili hivi kwamba, ingawa walikuwa na hali ya kawaida ya maisha na hawakufikia hamsini kwa idadi, walichanga fedha taslimu $1,000 na kumkabidhi kwa kusudi hilo. Akiwa na fedha hizo pamoja na maandishi mengi yaliyotayarishwa kwa uangalifu, Mchungaji Matteson alifika Battle Creek, akaomba tena vitabu vichapishwe. Kwa kuwa alikuwa tayari kuondoa vizuizi vilivyokuwa vimetajwa hapo awali, ombi lake lilikubaliwa, na tarehe 18 Machi 1867 akaanza kunisomea mimi na Mchungaji J. N. Andrews maandishi aliyokuwa ametayarisha kwa ajili ya kitabu chake, Liv og Død (Uzima na Mauti). Wakati huo tulikuwa wajumbe wa kamati ya uchapishaji. Yaani, alitueleza kwa Kiingereza yale ambayo maandishi yake yalisema kwa Kideni-Kinorwei.
GSAM 414Mchungaji Matteson Awa Mchapaji
GSAM 414.1Wakati huo hakukuwa na mchapaji ambaye angeweza kuacha kazi nyingine ili kumpangia herufi za uchapaji, kwa hiyo akaomba apewe nafasi ya kujifunza kuzipanga mwenyewe. Aliendelea na kazi hii mpaka alipokuwa amechapisha takriban kurasa elfu moja za vitabu vidogo na vijitabu katika lugha yake mwenyewe.
GSAM 414.2Akiwa na njia hii mpya ya kueneza ukweli miongoni mwa watu wake, alitoka kwa ujasiri mpya, akifanya mikutano katika majimbo mbalimbali. Tangu wakati huo kazi iliendelea kwa kasi kubwa miongoni mwa Waskandinavia.
GSAM 414Jarida la Kwanza Katika Lugha ya Kigeni
GSAM 414.3Kazi miongoni mwa watu wenye asili ya Denmark na Norwei ilikuwa imekua kiasi kwamba gazeti la kila mwezi lilihitajika, ambalo kupitia hilo watu wa asili hiyo wangepokea mafundisho na kutiwa moyo katika lugha yao wenyewe. Kwa hiyo, tarehe 1 Januari 1872, ofisi ya Mapitio na Mbiu ilitoa gazeti la kila mwezi kwa Kideni, lenye kurasa ishirini na nne katika umbo la jarida, lililoitwa Advent Tidende (Habari za Ujio). Mwaka uliofuata ukubwa wa jarida hili uliongezwa kufikia kurasa thelathini na mbili. Lilikuwa jarida la kwanza kutolewa na Waadventista wa Sabato katika lugha ya kigeni.
GSAM 414.4Katika mwaka 1874 waumini waliozungumza Kiswidi walikuwa na shauku kubwa hivi kwamba jarida la kila mwezi lenye kurasa kumi na sita lilianzishwa katika lugha hiyo, likiitwa Svensk Härold (Mbiu ya Kiswidi).
GSAM 414.5Wakati Mchungaji Matteson alipoanza kazi ya umishenari kwa watu wa Skandinavia katika nchi zao za asili (Juni 1877), nakala 266 za Tidende zilikuwa zikitumwa kutoka Amerika kwenda Denmark kila mwezi, na 60 kwenda Norwei. Kwa kusoma majarida hayo, watu kadhaa huko Skandinavia walikuwa tayari wanaitunza Sabato. Kutokana na kazi yake ya mwaka mmoja huko Denmark, makundi ya waumini yaliinuka katika sehemu kadhaa tofauti.
GSAM 415Ofisi ya Uchapishaji Huko Norwei
GSAM 415.1Baada ya hayo Mchungaji Matteson alikwenda Norwei, ambako tarehe 7 Juni 1879 alianzisha rasmi kanisa la washiriki thelathini na wanane, kutokana na kazi yake huko Christiana. Karibu na wakati huo Mchungaji J. P. Jasperson, kutoka Amerika, aliungana naye katika huduma. Katika mwaka huo pia chama cha uchapishaji kilianzishwa huko Norwei, na jengo likanunuliwa huko Christiana kwa gharama ya $14,580 kwa ajili ya ofisi ya uchapishaji, chumba cha mikutano kwa ibada za kanisa, na vyumba vya kuishi. Kwa muda fulani, gazeti la Tidernes Tegn (Ishara za Nyakati) lilitolewa kila juma kutoka ofisi ya Christiana kwa nakala chache.
GSAM 415.2Mwanzoni mwa majira ya kupukutika kwa majani ya mwaka 1880, Mchungaji Matteson alifika Amerika kutafuta msaada wa kupanua kazi ya Skandinavia. Alihudhuria Konferensi Kuu ya mwaka huo, akarudi Ulaya mwezi Aprili 1881, akiwa ametiwa moyo sana. Muda mfupi baada ya kurudi kwake, mashine ya uchapaji ya silinda ilinunuliwa na kuwekwa katika ofisi ya Christiana.
GSAM 415Majarida ya Afya kwa Kideni na Kiswidi
GSAM 415.3Mara moja walianza kuchapisha jarida la afya kwa Kideni, lililoitwa Sundheds Bladet. Katika mwaka 1883 alitoa jarida kama hilo kwa Kiswidi, pamoja na jarida la dini lililoitwa Sanningens Härold (Mbiu ya Ukweli). Katika mwaka 1884 walikuwa na vifaa vya ofisi vyenye thamani ya $2,563. Katika mwaka huo magazeti 115,000 yalikuwa yamechapishwa na kusambazwa kwa jumla, pamoja na maelfu mengi ya vijitabu na vitabu kadhaa.
GSAM 415Mchungaji Haskell Huko Skandinavia
GSAM 415.4Kazi katika nchi za Skandinavia ilipata msaada mkubwa kutokana na ziara ya Mchungaji Haskell katika mwaka 1882, na katika mwaka 1884 ilisaidiwa sana na kazi ya Wachungaji George I. Butler, B. L. Whitney, A. B. Oyen, na E. G. Olsen.
GSAM 416Bibi White Aisaidia Sana Skandinavia
GSAM 416.1Katika mwaka 1885, Bibi Ellen G. White na mwanawe, W. C. White, walifanya ziara huko Skandinavia, ambayo ilikuwa na thamani isiyopimika kwa kazi katika eneo hilo. Baadhi ya watu walikuwa wamepata wazo kwamba maskini katika nchi hiyo hawangeweza kutoa zaka, na kwamba haikuwa na faida kujaribu kutembelea watu ili kuuza vitabu. Ushuhuda uliotolewa na Bibi White ulikuja kwa wakati ufaao, nao ukapokelewa vizuri na watu, kama ilivyoonekana katika jibu lao kwa maneno haya: “Yote aliyoyasema Bwana tutayatenda, nasi tutatii.” Katika ziara hiyo, mabadiliko kamili yalitokea katika eneo la kazi la Skandinavia, hasa kutokana na juhudi zisizochoka za Bibi White.
GSAM 416Jengo Jipya la Ofisi Lajengwa Huko Norwei
GSAM 416.2Katika mwaka 1886 Wachungaji O. A. Olsen na N. Clausen walizitembelea nchi za Skandinavia, na huyu wa mwisho akakaa huko kwa muda mrefu. Katika mwaka 1885 jengo jipya la ofisi lilijengwa huko Christiana, na kwa mwaka ulioishia tarehe 1 Septemba 1886, ofisi ilipata kiasi cha $5,386.68 kutokana na mauzo ya vitabu na vijitabu pekee, huku kiasi kilichopokewa kwa malipo ya kuandikisha wapokeaji wa majarida kikiwa $3,146.03.
GSAM 416Makanisa Ishirini na Matano Huko Skandinavia
GSAM 416.3Taarifa iliyotolewa kwa Konferensi Kuu katika mwaka 1889 ilisema kwamba katika eneo la kazi la Skandinavia kulikuwa na makanisa ishirini na matano, yenye washiriki 926, ambao walitoa zaka ya $2,548.75; eneo hilo pia lilikuwa na wachungaji sita, wahubiri wanne wenye kibali, na wainjilisti wa vitabu hamsini na wawili. Mauzo ya vitabu kwa Norwei na Uswidi katika robo moja ya mwaka yalikuwa $2,161.26.
GSAM 416Shule Huko Christiana
GSAM 416.4Wakati huo shule ilikuwa ikiendelea huko Christiana, ikiwa na wanafunzi hamsini. Katika mwaka 1891, Wachungaji O. A. Olsen na E. J. Waggoner waliendesha mafunzo ya Biblia huko Christiana, yaliyohudhuriwa na wanafunzi mia moja. Katika mafunzo hayo, mafundisho ya kina kuhusu kazi ya uinjilisti wa vitabu yalitolewa.
GSAM 417Makanisa Arobaini Huko Skandinavia Katika Mwaka 1895
GSAM 417.1Miaka sita baadaye, katika mwaka 1895, tunaona taarifa iliyotolewa na Mchungaji D. A. Robinson, aliyekuwa wakati huo msimamizi wa wilaya ya kazi katika nchi za nje. Taarifa hiyo inaonyesha wazi sana ukuaji mkubwa wa kazi katika kipindi hicho, kwa hiyo tunainukuu kama ifuatavyo: “Skandinavia ina makanisa arobaini, na washiriki 1,458. Zaka ya mwaka ilikuwa $5,585.55. Kuna wachungaji kumi na watano waliowekewa mikono, wahubiri kumi na mmoja wenye kibali, na mauzo ya vitabu kwa mwaka yanafikia $40,000. Kiasi hiki kikubwa kimetokana hasa na juhudi za wainjilisti wa vitabu, tena katika nchi ambayo, katika mwaka 1885, wauzaji wa vitabu, na hata wachungaji wa imani yetu, walidai kwamba haingewezekana kuuza vitabu kwa kuwatembelea watu.
GSAM 417Konferensi Tatu za Skandinavia
GSAM 417.2Katika eneo la kazi la Skandinavia kwa sasa kuna konferensi tatu, ambazo tarehe za kuanzishwa kwake ni hizi: Denmark, 30 Mei 1880; Uswidi, 12 Machi 1882; Norwei, 10 Juni 1887. Mchungaji John Matteson, ambaye alikuwa wa kwanza kuanzisha Misheni ya Skandinavia na kuifanya kazi ya mwanzo kwa mafanikio makubwa, na ambaye alijitahidi sana na kujitoa mhanga kwa ajili ya ustawi wa watu hao, alipata ugonjwa ule wa kufisha, kifua kikuu, akafa huko El Monte, California, tarehe 30 Machi 1896, akiwa na umri wa miaka sitini na mmoja.
GSAM 417MISHENI YA UINGEREZA
GSAM 417.3William Ings, mzaliwa wa Hampshire, Uingereza, lakini Mmarekani kwa moyo na elimu, kwa kuwa alikuwa ameishi Marekani tangu utotoni, alifika Southampton kutoka Basel, Uswisi, tarehe 23 Mei 1878. Wakati huo alikaa kwa muda mfupi, majuma mawili tu, kisha akarudi kwa muda mfupi katika bara la Ulaya. Hata hivyo, muda mfupi baadaye alikwenda tena Southampton, ambako, baada ya miezi minne ya kazi ya nyumba kwa nyumba akigawa vijitabu na kufanya kazi yoyote ya umishenari iliyojitokeza, alitoa taarifa kwamba watu kumi walikuwa wanaitunza Sabato. Tarehe 30 Desemba ya mwaka huo, mimi na mke wangu tulifika Southampton, ambako tuliungana na Mchungaji Ings katika kazi ya kufanya mikutano wakati wa majira ya baridi katika Shirley Hall, na katika nyumba tuliyokuwa tumeikodi wenyewe. Katika majira ya kiangazi ya mwaka 1879, tulifanya mikutano ya hemani huko Southampton. Wakati huo na mahali hapo, Binti Maud Sisley (sasa Bibi Boyd) alijiunga na kazi, akifundisha Biblia na kufanya kazi ya nyumba kwa nyumba. Kutokana na juhudi hizi, watu kadhaa waliukubali ukweli. Katika majira ya baridi yaliyofuata tulifanya mikutano katika ukumbi uliokuwa Ravenswood Villa, jengo ambamo tuliishi na kuwa na ghala letu la vitabu.
GSAM 418Mkutano wa Hemani Huko Uingereza
GSAM 418.1Katika majira ya kiangazi ya mwaka 1880, Mchungaji Andrews, ingawa alikuwa dhaifu kiafya, alifika kutoka Uswisi kusaidia katika mkutano wa hemani huko Romsey, ambako watu wengine waliukubali ujumbe.
GSAM 418.2Tarehe 11 Januari 1880, chama cha vijitabu kilianzishwa. Washiriki waliipenda sana kazi hii, na machapisho mengi yaligawiwa.
GSAM 418.3Tarehe 8 Februari 1880, ubatizo wetu wa kwanza ulifanyika, nao watu sita waliokuwa wamejitayarisha walibatizwa. Kufikia tarehe 2 Julai 1881, watu ishirini na tisa waliokuwa wamejitayarisha walikuwa wamebatizwa kwa kuzamishwa majini huko Southampton.
GSAM 418Watendakazi Waongezeka Huko Uingereza
GSAM 418.4Kwa uamuzi wa kura wa Konferensi Kuu iliyofanyika katika majira ya kupukutika kwa majani ya mwaka 1881, Mchungaji A. A. John na mke wake, Geo. R. Drew, na Binti Jennie Thayer walikwenda Uingereza, wakajiunga na kazi katika eneo hilo la umishenari. Katika mwaka 1882, Mchungaji Haskell alitembelea eneo la kazi la Ulaya, akakaa siku kadhaa pamoja na watendakazi katika misheni ya Uingereza, akitoa msaada wa thamani kwa mawaidha na mashauri.
GSAM 418.5Mwezi Machi 1882, nyongeza ya Uingereza yenye kurasa mbili kwa ajili ya Ishara za Nyakati ilianza kuchapishwa, nayo ikaambatishwa katika nakala elfu moja za Ishara zilizotumwa kutoka Amerika. Hizi zilitumiwa katika kazi ya umishenari huko Britania Kuu. Taarifa ya kazi ya tarehe 1 Oktoba 1883 inaonyesha kwamba wakati huo kulikuwa na watunza Sabato mia moja. Zaka iliyotolewa tangu kuanzishwa kwa misheni ilikuwa $2,078.71.
GSAM 419Kazi ya Umishenari Melini
GSAM 419.1Kwa wema wa wasimamizi wa meli, Mchungaji Ings aliruhusiwa kutuma vifurushi vya vijitabu na magazeti bila malipo hadi bandari themanini kati ya bandari kuu za “Kampuni ya Meli za Mvuke ya Peninsular and Oriental,” huko Afrika Kusini, Hindia Mashariki na Hindia Magharibi, Amerika ya Kati, na Visiwa vya Bay. Ni kwa ushawishi wa machapisho yaliyotumwa kwa njia hiyo kwamba shauku iliamshwa kwa mara ya kwanza katika kisiwa cha Demarara. Tulipata habari hizi kupitia barua kutoka kisiwani humo.
GSAM 419“Historia ya Sabato” Yawekwa Katika Maktaba za Uingereza
GSAM 419.2Nakala ya Historia ya Sabato cha Mchungaji Andrews ilikuwa pia imewekwa katika kila moja ya maktaba za umma na vyumba vya kusomea bila malipo sitini kotekote Britania Kuu, na vitabu hivyo bado viko humo, vikisimulia historia hiyo kwa wale walio tayari kusoma.
GSAM 419.3Katika mwaka 1884 Mchungaji Butler alitembelea Uingereza, akiwa ameandamana na watendakazi wengine kwa ajili ya eneo hilo. Wachungaji S. H. Lane na Robert Andrews walisafiri kwa meli kutoka Boston kwenda kujiunga na misheni huko Britania Kuu tarehe 9 Mei 1885. Ziara ya Bibi White huko Uingereza ilikuwa chanzo cha nguvu na kutia moyo kwa watendakazi. Bibi White na mwanawe walikaa huko kwa majuma machache kabla ya kurudi Amerika kutoka eneo la kazi la Ulaya.
GSAM 419“Ukweli wa Leo” Laanzishwa
GSAM 419.4Mwanzoni mwa mwaka 1884, muda mfupi baada ya Mchungaji Butler kufika Uingereza, iliamuliwa kuanzisha huko Grimsby gazeti lenye kurasa nane lililotoka mara mbili kwa mwezi, lililoitwa Ukweli wa Leo, M. C. Wilcox akiwa mhariri. Gazeti hilo sasa linachapishwa London, Uingereza, likiwa la kila juma lenye kurasa kumi na sita, na kila juma hutolewa nakala zipatazo 18,000.
GSAM 420.1Katika mwaka 1889, Mchungaji Holser alitoa taarifa kwamba Misheni ya Uingereza ilikuwa na makanisa manane, yenye watunza Sabato mia mbili, ambao sitini na watano kati yao walikuwa London. Zaka ya mwaka uliotangulia ilikuwa $1,244.58. Kulikuwa na wachungaji wawili waliowekewa mikono, wahubiri wawili wenye kibali, wamishenari wawili wa melini, na watendakazi saba wa Biblia. Ilikuwa karibu na wakati huo kwamba Wachungaji Wm. Hutchinson na Francis Hope walijiunga na misheni ya Uingereza.
GSAM 420Pacific Press Huko London
GSAM 420.2Katika mwaka 1890 Kampuni ya Uchapishaji ya Pacific Press, ya Oakland, California, ilianzisha ofisi ya tawi katika 48 Paternoster Row, London, na ofisi ya uchapishaji katika 451 Holloway Road, London, N. Mauzo ya vitabu kutoka ofisi hiyo kwa mwaka wa kwanza, kwa bei za jumla, yalikuwa $9,556.89.
GSAM 420.3Mwezi Februari 1895, Mchungaji Robinson alitoa taarifa ifuatayo:
GSAM 420.3“Huko Britania Kuu kuna makanisa kumi na moja, washiriki 363, wachungaji watano, na mhubiri mmoja mwenye kibali. Zaka ya mwaka uliopita ilikuwa $5,077.20, au wastani wa $13.98 kwa kila mshiriki. Mali ya ofisi ya uchapishaji sasa inamilikiwa na kusimamiwa na Chama cha Kimataifa cha Vijitabu chenye Dhima ya Kikomo, kampuni ya Uingereza.”
GSAM 420.4Mwezi Desemba 1895, Katibu wa Umishenari Katika Nchi za Nje alitoa taarifa kwamba Britania Kuu ilikuwa na washiriki 560. Zaka ilikuwa imeongezeka kwa $1,000 katika mwaka huo. Wakati huo, makundi manane yalikuwa yakikusanyika siku ya Sabato katika sehemu mbalimbali za London.
GSAM 420.5Hivyo kazi katika eneo hilo la umishenari iliendelea, nyakati nyingine karibu bila maendeleo yake kuonekana. Mbegu hazichipuki haraka katika aina fulani za udongo kama zinavyochipuka katika nyingine. Kuota kwake huwa polepole zaidi, lakini ukuaji wake huwa thabiti na wenye nguvu zaidi. Ndivyo ilivyo kwa ukweli wa ujumbe wa tatu katika ufalme huu. Mbegu yake imepandwa, ikatia mizizi, na kukua polepole mpaka sasa imefikia ukubwa mkubwa kwa kulinganisha.
GSAM 421MISHENI YA AUSTRALASIA
GSAM 421.1Tarehe 10 Mei 1885, Wachungaji S. N. Haskell, J. O. Corliss na familia yake, M. C. Israel na familia yake, Wm. E. Arnold, na Henry Scott walisafiri kwa meli kutoka San Francisco kwenda kuanzisha misheni katika eneo la kazi la Australia. Miaka kumi na mmoja kabla ya wakati huo, katika mwaka 1874, katika mkutano uliofanyika Battle Creek, Bibi White alisema kwamba mataifa mengi bado yangeupokea ukweli, na kwamba alikuwa ameona mashine za uchapaji zikifanya kazi, na vitabu na magazeti vikichapishwa katika nchi mbalimbali. Alipoulizwa ataje nchi zilizokuwa zikimaanishwa, jibu lilikuwa kwamba Australia ndilo jina pekee aliloweza kukumbuka.
GSAM 421Mwangwi wa Biblia
GSAM 421.2Kutokana na kazi ya bidii na yenye mafanikio ya Mchungaji Haskell na wenzake, ujumbe ulienea kwa kasi sana hivi kwamba ilionekana lazima kuchapisha gazeti huko Australia. Kwa hiyo, mipango ya uchapishaji ilifanywa, na tarehe 1 Januari 1886 jarida la kila mwezi lenye kurasa kumi na sita lilitolewa Melbourne, likiitwa Mwangwi wa Biblia na Ishara za Nyakati. Toleo la kwanza lilichapishwa kwa nakala elfu sita, ilhali idadi ya kawaida ilikuwa elfu tatu tu.
GSAM 421Kanisa la Kwanza Laanzishwa Rasmi Huko Australia
GSAM 421.3Siku ya kwanza ya juma, tarehe 10 Aprili 1886, kanisa la kwanza la Waadventista wa Sabato huko Australia lilianzishwa rasmi. Walikuwapo watu kumi na wanane waliokuwa wametia sahihi agano, na wengine saba wakaomba kupokelewa kwa ubatizo. Hao walibatizwa Sabato iliyofuata, na kila Sabato kwa majuma kadhaa washiriki waliongezwa, mpaka kanisa likawa na watu hamsini na watano. Kufikia mwezi Mei 1886, jumla ya walioandikishwa ilikuwa tisini. Mbali na hao, kulikuwa na watu wapatao thelathini na watano katika sehemu nyingine waliokuwa wanaitunza Sabato.
GSAM 421.4Katika ofisi ya uchapishaji kulikuwa na mashine mbili nzuri za uchapaji na injini, vyote vikiwa vimelipiwa kikamilifu na kumilikiwa na Waadventista wa Sabato katika nchi hiyo ya mbali sana—yapata maili elfu saba kutoka ofisi yetu kubwa iliyoko Oakland, California.
GSAM 422.1Katika mwaka 1886 ujumbe ulienea hadi New Zealand. Taarifa kutoka eneo la kazi la Australia inasema kwamba kulikuwa na watunza Sabato hamsini huko New Zealand. Kiasi kilichopokewa kutokana na mauzo ya vitabu katika ofisi kilikuwa $700. Zaidi ya hayo, wainjilisti wa vitabu walikuwa wameuza nakala mia nne za Pambano Kuu huko New Zealand, na nakala elfu moja za Mawazo juu ya Danieli huko Australia.
GSAM 422Jengo la Ofisi nchini Australia
GSAM 422.2Katika taarifa iliyotolewa Julai 19, 1889, tunapata habari hizi: Jengo la ofisi ya uchapishaji huko Melbourne limekamilika, likiwa na chumba cha ibada kwa ajili ya mikutano ya kanisa.
GSAM 422Kazi Yaanza Tasmania
GSAM 422.3Konferensi imeundwa nchini Australia na nyingine nchini New Zealand, na Wachungaji Israel na Steed wameieneza kazi hadi Tasmania. Huko Tasmania, makanisa matatu tayari yameundwa, yenye jumla ya washiriki mia moja thelathini na sita. Mbali na hawa, kuna watunza Sabato wengine waliotawanyika ambao bado hawajaundwa kuwa makanisa.
GSAM 422.4Zaka ya mwaka katika eneo la kazi la Australia ilikuwa $9,371. Kulikuwa na wainjilisti wa vitabu kumi na watano katika eneo hilo, ambao mauzo yao ya vitabu yalifikia $19,500.
GSAM 422.5Katika safari yake ya pili ya kuzunguka ulimwengu, Mchungaji Haskell alitembelea Australia tena, akahudhuria mkutano wao wa konferensi uliofanyika Agosti, 1889, na kutoa msaada wenye manufaa kwa njia nyingi. Msaada huo ulithaminiwa sana na kundi hilo lililokuwa limeundwa karibuni. Watendakazi mbalimbali kutoka Amerika wameitembelea Australia mara kwa mara kwa ajili ya kusudi lile moja kuu—kuijenga na kuiimarisha kazi ya Mungu.
GSAM 422Bibi White nchini Australia
GSAM 422.6Katika majira ya kupukutika kwa majani ya mwaka 1891, Bibi E. G. White, mwanawe W. C. White, Mchungaji Geo. B. Starr, na wengine waliondoka California kwenda Australia, wakafika huko Desemba—katikati ya majira ya kiangazi katika bara hilo. Ushuhuda wa Bibi White, licha ya udhaifu wa mwili aliokuwa nao katika miaka tisa ya kukaa kwake katika nchi hiyo, ulisaidia sana kuifanya kazi ipatane ipasavyo na roho na mwelekeo wa ujumbe wa malaika wa tatu. Walipokuwa Australia, Mchungaji J. O. Corliss alijiunga tena na kazi huko, na W. A. Colcord na wengine wakaingia katika eneo hilo la kazi wakiwa wachungaji, walimu, na kadhalika.
GSAM 423Mchungaji Olsen nchini Australia
GSAM 423.1Katika kipindi cha uongozi wa Mchungaji O. A. Olsen akiwa mwenyekiti wa Konferensi Kuu, alitembelea taasisi zetu zote kuu katika sehemu zote za nchi. Hili lilihitaji kusafiri mbali sana—safari ya kuzunguka ulimwengu. Alifanya safari hiyo ili afahamu vizuri zaidi mahitaji yao na hali ya vituo mbalimbali vya umishenari, apate kuwa tayari kuvihudumia bila upendeleo. Katika safari hiyo, mwaka 1893, alikaa Australia kwa majuma kadhaa.
GSAM 423Konferensi ya Muungano ya Australasia
GSAM 423.2Katika wakati huo Konferensi ya Muungano ya Australasia iliundwa, ikijumuisha konferensi za Australia na New Zealand pamoja na maeneo ya umishenari ya Australia. Konferensi hii hukutana mara moja kila baada ya miaka miwili, na huendeshwa kwa utaratibu wa konferensi za miungano katika nchi nyingine. Katika mwaka 1893, wainjilisti wachache wa vitabu waliokuwa katika eneo hili waliuza toleo la nakala 5,000 za Hatua za Kumwendea Kristo, na toleo la pili lenye idadi ileile likachapishwa. Katika majira ya kiangazi ya 1894-95, walipokea maagizo 4,000 ya vitabu vilivyouzwa kwa kuagizwa mapema katika muda wa miezi minne.
GSAM 423Mchungaji Prescott nchini Australia
GSAM 423.3Mwaka 1895, Mchungaji W. W. Prescott, Katibu wa Elimu wa dhehebu, alikaa katika konferensi hii kwa miezi kadhaa, akitumia muda mwingi na kulitafakari sana tawi hili la kazi. Wakati huohuo aliendesha semina ya elimu iliyokuwa na manufaa makubwa kwao.
GSAM 424.1Taarifa ya kazi ya mwaka iliyowasilishwa kwa Konferensi Kuu ilitolewa na Mchungaji W. C. White, nayo ni kama ifuatavyo:
GSAM 424.1“Konferensi ya Muungano ya Australia inajumuisha makanisa kumi na saba yenye washiriki 1074, ambao walitoa zaka ya $9,810.10 katika mwaka uliotangulia. Konferensi hii ina wachungaji kumi na wawili waliowekewa mikono, wahubiri wawili wenye kibali cha kuhubiri, watendakazi watatu wa Biblia, na wainjilisti wa vitabu hamsini, ambao waliuza vitabu vyenye thamani ya $28,731.11 katika mwaka huo. Katika mwaka huo, koloni la New South Wales, lenye makanisa sita na washiriki 321, lilitenganishwa na Konferensi ya Australia, likapewa jina la Konferensi ya New South Wales.”
GSAM 424KAZI YA UMISHENARI AFRIKA KUSINI
GSAM 424.2Katika mkutano wa Konferensi Kuu uliofanyika Battle Creek mwaka 1886, suala la kuanzisha kazi ya umishenari Afrika Kusini lilizingatiwa. Kwa kuwa uamuzi ulifanywa wa kuunga mkono jambo hilo, mwanzoni mwa majira ya kiangazi ya 1887 jitihada ilifanywa kuanzisha kazi katika nchi hiyo ya mbali, ambako watu wachache waliokuwa tayari wameanza kuitunza Sabato walikuwa wakiomba watendakazi.
GSAM 424Wachungaji Boyd na Robinson Afrika Kusini
GSAM 424.3Kwa kusudi hilo, Mei 11, Mchungaji C. L. Boyd na familia yake, Mchungaji D. A. Robinson na mkewe, pamoja na watendakazi wengine, waliondoka kwa meli kutoka jiji la New York kuelekea Afrika, wakipitia Liverpool na London. Miaka mitatu baadaye, katika mkutano wa Konferensi Kuu, Bwana P. W. B. Wessels alisema kwamba watendakazi hao walipofika Afrika, kulikuwa na watu wapatao arobaini ambao tayari walikuwa wakiitunza Sabato ya amri ya nne kutokana na kusoma machapisho kuhusu jambo hilo na kujifunza Maandiko.
GSAM 424.4Wachungaji Robinson na Boyd walianza kazi ya umishenari huko Cape Town, na kutoka hapo ikaenea kuelekea kaskazini-mashariki karibu maili mia nane hadi Kimberley, katika maeneo ya migodi ya almasi.
GSAM 424.5Hadi mwaka 1889, kulikuwa na wachungaji wawili tu, mhubiri mmoja mwenye kibali cha kuhubiri, makanisa manne, na washiriki themanini; hawa walitoa zaka ya $2,798.36. Katika mwaka huo Mchungaji Ira J. Hankins, kutoka Amerika, alifanya kazi huko Cape Town kwa matokeo mazuri, na Bwana na Bibi Druillard walikuja kutoka Nebraska kujiunga na kazi mahali hapo, na kushiriki katika kazi ngumu na shida zinazowapata wale wanaoitwa kuwa waanzilishi wa kazi katika eneo jipya. Kazi ya Bibi Druillard ilikuwa hasa katika ghala la vitabu, ambako shughuli za idara hiyo ziliachwa chini ya usimamizi wake; naye Bwana Druillard alijishughulisha na kazi ya umishenari kwa jumla. Katika mwaka huo, aliuza vitabu vyenye thamani ya $750 katika meli zilizotia nanga bandarini hapo.
GSAM 425Mchungaji Haskell Barani Afrika
GSAM 425.1Ilikuwa Agosti ya mwaka huohuo ambapo Mchungaji Haskell alifika Cape Town. Miezi mitano ilitumika vizuri katika kuyatembelea na kufanya kazi pamoja na makundi mbalimbali huko Afrika Kusini. Kwa ziara hiyo kazi iliimarishwa na kujengwa, na moyo wake mwenyewe ukatiwa moyo kwa kuwa aliona matunda ya kazi yake. Shauku ya kazi ya elimu iliamshwa, hata wanafunzi kumi na wawili kutoka Afrika wakaja Amerika kusoma katika shule za dhehebu letu.
GSAM 425.2Wakati huohuo kazi ya uinjilisti wa vitabu ilipewa uangalifu unaostahili. Semina ya kuendeleza kazi hiyo ilifanyika Cape Town, ikiongozwa na Bwana E. M. Morrison, nayo ikalipa tawi hili muhimu la ujumbe uhai na nguvu mpya. Mara baada ya mafunzo yaliyotolewa katika semina hiyo, wainjilisti wa vitabu kumi na watatu, katika muda wa miezi sita, waliuza na kupeleka vitabu vyenye thamani ya $5,621.28 kwa wanunuzi. Kwa kweli, maagizo yalikuwa mengi sana hata “yakailemea” kabisa ofisi ya London, kwa kuwa vitabu havikuweza kutayarishwa kwa haraka ya kutosha kutosheleza mahitaji.
GSAM 425.3Mwaka 1892, Mchungaji A. T. Robinson alijiunga na kazi Afrika Kusini. Wakati huo kazi ilikuwa imekua kiasi cha kuhitaji ghala jipya la vitabu kuchukua nafasi ya lile la zamani. Kwa hiyo jengo jipya lilijengwa, kubwa vya kutosha kutoa nafasi kwa mikutano ya kanisa.
GSAM 426Jengo la Chuo Barani Afrika
GSAM 426.1Hivyo kazi imeendelea kusonga mbele hatua kwa hatua, hadi jengo la chuo likajengwa huko Claremont, kitongoji cha Cape Town, kwa gharama ya $35,000. Msaada pekee walioutaka kutoka kwa ndugu wa Amerika ulikuwa kutumiwa kundi la walimu wenye sifa za kufundisha masomo ya chuo, nao wenyewe wangegharimia kazi hiyo. Ombi hilo lilipotimizwa, shule ilifunguliwa Februari 1, 1893.
GSAM 426Konferensi ya Afrika Kusini
GSAM 426.2Konferensi ya Afrika Kusini iliundwa mwaka 1892. Katika mkutano wa Konferensi Kuu wa mwaka 1893, ilipigiwa kura na kupokelewa katika Konferensi Kuu. Wakati huo ilikuwa na makanisa matano, washiriki mia moja thelathini na wanane, ambao walitoa zaka ya $34,077.32 katika mwaka uliotangulia. Katika mkutano huo, Konferensi ya Afrika Kusini iliwakilishwa na Peter Wessels, ambaye kwa ukarimu alitoa $16,000 kwa Konferensi Kuu, kiasi kilichozidi kile ambacho Konferensi Kuu ilikuwa imetumia kuanzisha kazi Afrika Kusini. Mbali na zawadi hiyo, yeye na mmoja wa ndugu zake walitoa $40,000 kuanzisha kazi ya zahanati ya kutoa matibabu bila malipo katika jiji la Chicago.
GSAM 426.3Katika mkutano wa Konferensi Kuu wa mwaka 1895, Katibu wa Umishenari wa Nchi za Nje alisema hivi kuhusu eneo la kazi la Afrika:
GSAM 426.3“Konferensi ya Afrika Kusini imekuwapo kwa miaka miwili tu tangu kuundwa kwake, lakini katika muda huo Konferensi Kuu imetuma watendakazi kumi na wawili katika eneo hilo. Wawili kati yao wamekwenda katika sehemu za ndani za nchi wakiwa wamishenari wanaojitegemea kwa matumizi yao, na wengine wamejiunga na kazi katika idara mbalimbali. Konferensi hiyo ina shule inayositawi, makao ya yatima, na hospitali ya tiba na mapumziko inayojengwa. Takwimu zinaonyesha kuwa ina washiriki 184.”
GSAM 426Magazeti Yanayochapishwa Afrika Kusini
GSAM 426.4Suala la uhuru wa dini Afrika Kusini limewachochea watu wetu katika miezi michache iliyopita kuchapisha magazeti mawili, moja kwa Kiholanzi, linaloitwa De Wachter; jingine kwa Kiingereza, linaloitwa Mlinzi wa Afrika Kusini na Mwangwi wa Injili. Hili la pili husambaza nakala 4,000.
GSAM 427Konferensi ya Muungano ya Afrika Kusini
GSAM 427.1Mnamo Januari, 1903, Konferensi ya Muungano ya Afrika Kusini iliundwa, ikijumuisha konferensi za Koloni la Rasi na Natal-Transvaal, pamoja na maeneo ya umishenari ya Basutoland na Matabeleland chini ya usimamizi wa Konferensi ya Muungano. Katika konferensi hiyo kuna makanisa kumi na matano yaliyoundwa yenye washiriki 595, makundi tisa ambayo hayajaundwa kuwa makanisa yenye washiriki tisini, na watunza Sabato thelathini walio mbali na wenzao—jumla ya watu 715, ambao walitoa zaka ya $7,850. Kulikuwa na watendakazi thelathini na tisa, ambao kati yao ishirini na mmoja walilipwa mishahara na konferensi mbalimbali.
GSAM 427ENEO LA KAZI LA POLINESIA
GSAM 427.2Mwaka 1876, Mchungaji James White na mwandishi wa kitabu hiki tulituma juzuu moja ya Ishara za Nyakati na vijitabu kadhaa, pamoja na barua, kwenye Kisiwa cha Pitcairn. Machapisho hayo yaliwekwa katika meli iliyokuwa ikielekea New York kwa kuzunguka Rasi ya Horn. Tulihakikishiwa kwamba meli ingesimama Pitcairn, na kwamba kifurushi kingekabidhiwa huko. Hatukumjua mtu yeyote katika kisiwa hicho, wala hatukujua chochote kuhusu kisiwa chenyewe, isipokuwa sifa yake kwamba wakazi wake walikuwa watu waliojitoa kwa Mungu na kumcha. Magazeti hayo yalitumwa kwa kujaribu tu.
GSAM 427Ziara ya Pitcairn
GSAM 427.3Hatukusikia habari yoyote kutoka kwa watu hao wala kuhusu machapisho yetu mpaka Bwana John I. Tay alipokitembelea kisiwa hicho mwaka 1886, miaka kumi baadaye. Ndipo tulipojua kwamba kutokana na kusoma juzuu ya Ishara za Nyakati na vijitabu hivyo, wakati mmoja wakazi wote wa kisiwa hicho walikuwa karibu kuamua kubadili siku yao ya ibada kutoka siku ya kwanza ya juma hadi siku ya saba, na kuitunza Sabato ya Bwana. Hata hivyo, hawakufanya hivyo mpaka wakati wa ziara ya Bwana Tay. Kwa muda mrefu alikuwa amehisi moyoni msukumo mkubwa wa kukitembelea kisiwa hicho, lakini hakuwajua watu hao binafsi, wala hakujua shauku yao kwa ukweli iliyokuwa tayari imeamshwa.
GSAM 428.1Baada ya kurudi Amerika, aliomba kwa bidii sana meli ijengwe ili wamishenari waweze kusafirishwa kutoka kisiwa kimoja hadi kingine katika Bahari ya Pasifiki. Alihudhuria mkutano wa Konferensi Kuu uliofanyika mwaka 1889, akiwa na wazo hilo mbele ya mawazo yake yote, na huko akatetea kazi ya Visiwa vya Polinesia. Konferensi hiyo, ikiona manufaa ya mpango huo, ilipiga kura kukusanya kwa michango kiasi cha $12,000 cha kujenga au kununua meli kwa ajili ya kufanya kazi katika visiwa vya Bahari ya Pasifiki.
GSAM 428Kujengwa kwa Pitcairn
GSAM 428.2Kwa kupatana na uamuzi huo, meli ya Pitcairn ilijengwa katika majira ya kiangazi ya 1890, karibu na Benicia, yapata maili thelathini kutoka Oakland, California, kwa gharama ya $12,035.22. Katika robo tatu ya mwaka kiasi hicho cha fedha kilikusanywa na kutolewa na Shule za Sabato kwa ajili ya kusudi hilo pekee, wala hakukuwa kamwe na zawadi iliyotolewa kwa furaha na shauku kubwa zaidi. Meli hiyo iliwekwa wakfu huko Oakland, California, Septemba 25, 1890. Watu wapatao elfu moja na mia tano walikusanyika melini na gatini kushuhudia sherehe hiyo.
GSAM 428Safari ya Kwanza ya Pitcairn
GSAM 428.3Meli hiyo ilianza safari yake ya kwanza kutoka San Francisco kuelekea eneo lake la mbali la kazi, Oktoba 20. Waliokuwa melini wakiwa wamishenari ni Mchungaji E. H. Gates na mkewe, Mchungaji A. J. Read na mkewe, John I. Tay na mkewe, pamoja na mabaharia wamishenari chini ya Kapteni Marsh. Meli hiyo ilikwenda kwanza kwenye Kisiwa cha Pitcairn, maili elfu nne kusini mwa San Francisco, ikafika Novemba 25. Meli ilipoondoka kisiwani Desemba 17, watu wazima themanini na wawili walikuwa wamebatizwa na kuundwa kuwa kanisa la Waadventista wa Sabato. Kisha meli ilienda katika makundi ya visiwa vya Society, Hervey, Samoa, Urafiki, na Fiji, ikiwaachia watu wanaozungumza Kiingereza vitabu vya dini na vijitabu kuhusu afya na kiasi. Katika miezi minane, hadi Septemba, 1891, wamishenari waliuza vitabu vyenye thamani ya $1,900, pamoja na kugawa machapisho mengi bila malipo.
GSAM 429.1Wamishenari waliwekwa katika vituo kama ifuatavyo: Mchungaji Read huko Tahiti; Mchungaji Gates alibaki Pitcairn kumalizia kazi iliyokuwa tayari imeanza huko; naye Bwana Tay alichagua kufanya kazi katika kisiwa cha Fiji. Katika Mapitio na Mbiu la Aprili 14, 1904, Mchungaji Fulton anasema kuhusu kazi ya Fiji: “Sasa kuna watunza Sabato zaidi ya mia moja na hamsini katika eneo hili la umishenari.” Kutoka Fiji, meli ilisafiri kwenda Auckland, New Zealand, kwa ajili ya matengenezo na maboresho yaliyohitajika, na pia kupata akiba ya vitabu.
GSAM 429Vifo vya Wamishenari
GSAM 429.2Baada ya kutokuwapo kwa mwaka mmoja, miezi kumi na mmoja, na siku kumi na nane, Pitcairn ilirudi San Francisco, ikafika Oktoba 9, 1892. Katika muda huo Kapteni Marsh alikuwa amefariki na kuzikwa katika kisiwa cha New Zealand. Bwana Tay alipatwa na nimonia, ambayo hakupona. Yeye pia alifariki kwa amani, akazikwa katika nchi ya mbali ya Fiji; na hivyo maisha mawili yenye thamani yakatolewa mapema namna hiyo kwa ajili ya kazi ya umishenari ya Polinesia.
GSAM 429.3Wamishenari waliokuwa wameweka makao yao katika kisiwa cha Tahiti, huko Papeete, walipata furaha kwa kuona matunda ya kazi yao karibu mara moja. Kufikia wakati huo waliweza kutuma nyumbani taarifa ya kutia moyo kwamba watu arobaini walikuwa wameongoka na kuundwa kuwa kanisa la Waadventista wa Sabato.
GSAM 429Safari ya Pili ya Pitcairn
GSAM 429.4Meli iliondoka San Francisco katika safari yake ya pili, Januari 17, 1893, ikiwa na wamishenari hawa: B. J. Cady na mkewe, J. M. Cole na mkewe, E. C. Chapman na mkewe, na M. G. Kellogg, daktari wa tiba. Bibi Hattie Andre, kutoka Ohio, alifuatana nao akiwa mwalimu wa Kisiwa cha Pitcairn. Katika majira ya kupukutika kwa majani ya 1893, Bwana Cady alifungua shule huko Raiatea, katika kundi la visiwa vya Society, yenye wanafunzi sitini. Mwishoni mwa muhula wa kwanza idadi ilikuwa imeongezeka hadi mia moja na watano. Mwanzoni mwa muhula wa pili kulikuwa na wanafunzi mia moja na ishirini waliohudhuria.
GSAM 430Safari ya Tatu ya Pitcairn
GSAM 430.1Safari ya tatu ya meli ilifanyika mwaka 1893-94. Wamishenari wa safari hii walikuwa G. O. Wellman na mkewe pamoja na Lillian White, wote kutoka Michigan, waliokuwa wamepangiwa kwenda Raiatea kumsaidia Mchungaji Cady katika kazi yake. Bwana Stringer na mkewe walikwenda wakiwa wamishenari wanaojitegemea kwa matumizi yao. Walibaki Rurutu. Huko Raratonga, ambako watu waliitunza Jumamosi wakiichukulia kuwa Jumapili, Daktari Caldwell na mkewe waliwekwa kuwa watendakazi; nao Mchungaji Buckner na mkewe, kutoka California, wakaachwa Pitcairn. Wakati wa kukaa kwake na watu hao, shughuli nyingi mpya za uzalishaji zilianzishwa, ambazo kwa njia nyingi zimekuwa na manufaa kwa wakazi. Kwanza kabisa, kinu cha upepo cha kusaga mahindi ambayo sasa hulimwa kisiwani kilijengwa, na kwa nguvu hiyohiyo ya upepo mitambo midogo huendeshwa, jambo ambalo limeleta shughuli nyingine za uzalishaji ambazo wakazi wa kisiwa hicho hawakuzijua hapo awali.
GSAM 430Safari ya Nne ya Pitcairn
GSAM 430.2Desemba 15, 1895, Katibu wa Umishenari wa Nchi za Nje alisema:—
GSAM 430.3“Pitcairn sasa iko bandarini baada ya kurudi kutoka safari yake ya nne.... Kazi imeanzishwa katika makundi tisa tofauti ya visiwa, na watendakazi wafuatao wanafanya kazi humo:—
GSAM 430.4“Katika Kisiwa cha Pitcairn, walimu, E. S. Butz na mkewe, na Hattie Andre. Kisiwa cha Norfolk, baadhi ya wamishenari wanaojitegemea kwa matumizi yao wanafanya kazi hapa, nao walikuja kutoka Australia. Visiwa vya Society, mchungaji, B. J. Cady; wamishenari wa tiba, Bwana na Bibi R. A. Prickett. Raratonga, wamishenari wa tiba, Daktari J. E. Caldwell na mkewe, Bibi Lillian White na Bibi Maude Young; walimu, G. O. Wellman na mkewe, Mchungaji J. D. Rice na mkewe. Fiji, Mchungaji J. M. Cole na mkewe. Visiwa vya Urafiki, Mchungaji E. Hilliard na mkewe. Rurutu, Bwana na Bibi Stringer, wamishenari wanaojitegemea kwa matumizi yao. Hawaii, Mchungaji E. H. Gates na mkewe; walimu, H. H. Brand na mkewe. Samoa, Daktari F. E. Braucht na mkewe. Mchungaji D. A. Owen pamoja na mwanawe wa kiume na wa kike, wamishenari wanaojitegemea kwa matumizi yao.
GSAM 431.1“Katika safari zake nne, Pitcairn imeuza na kugawa machapisho mengi. Kwa sababu hiyo, watunza Sabato wamepatikana katika sehemu nyingi. Makanisa yameundwa katika Kisiwa cha Pitcairn, Norfolk, na Tahiti.”
GSAM 431Meli Pitcairn yauzwa
GSAM 431.2Kwa kuwa sasa kuna njia za kufika katika eneo la kazi la Polinesia ambazo hazikuwapo meli ilipojengwa, meli hiyo imeuzwa, na njia nyingine zinatumiwa kuendeleza kazi. Mchungaji E. H. Gates sasa ndiye msimamizi wa eneo la kazi la Polinesia, naye anaripoti maendeleo katika makundi mbalimbali ya visiwa.
GSAM 431VISIWA VYA INDIA MAGHARIBI
GSAM 431.3Katika majira ya baridi ya 1889, Bwana Wm. Arnold, kutoka Amerika, alianza kazi ya uinjilisti wa vitabu katika Visiwa vya India Magharibi. Alipokuwa akifanya kazi hiyo, alifanikiwa kupata majina na anwani za watu elfu moja na mia mbili, ambazo zilitumwa kwa Chama cha Kimataifa cha Vijitabu ili kitumie katika kazi ya umishenari. Kwa kuandikiana barua na kutuma machapisho kwenye anwani hizo, shauku ya kuujua ukweli iliamshwa, na hivyo njia ikafunguliwa ya kueneza injili kwa kuhubiri Neno.
GSAM 431.4Kwa kuitikia wito wa kazi ya kichungaji, Mchungaji D. A. Ball alienda Barbados na sehemu nyingine kufanya kazi, mnamo Novemba, 1890. Watu kadhaa waliupokea ukweli kutokana na juhudi zake. Katika mwaka 1892, Bwana Patterson, kutoka California, alitembelea visiwa akiuza kitabu cha Masomo ya Biblia, naye alifanikiwa vizuri. Katika mwaka 1893, B. B. Newman aliondoka Florida kwenda Jamaika ili asimamie kazi ya uinjilisti wa vitabu wakati Bwana Arnold hayupo. Bwana Evans na Bwana Hackett pia walienda katika Visiwa vya India Magharibi mwaka huohuo, ili washiriki katika tawi hili la kazi. Katika mwezi wa Mei, Mchungaji Haysmer na mkewe waliingia katika eneo hili kufanya kazi kadiri njia ingefunguka. Muda mfupi baada ya hapo Bwana Arnold alirudi, safari hii akiuza vitabu vinavyohusu afya. Hadi Julai, 1895, vitabu vya aina hii vyenye thamani ya $8,200 vilikuwa vimeuzwa katika Jamaika peke yake, huku mauzo ya vitabu vya dini yakifikia $7,654, au jumla ya $15,854. Kusambazwa kwa machapisho mengi namna hiyo kulisaidia sana kuanzishwa kwa kanisa lenye utaratibu mzuri huko Kingston, lenye washiriki sabini na watano, na kufungua njia za kazi ya kichungaji katika sehemu nyingine za kisiwa hicho.
GSAM 432Trinidad
GSAM 432.1Kazi hapa ilianzishwa kwa namna inayofanana na ile ya Jamaika. Katika mwaka 1889, Bwana F. B. Grant na mkewe walialikwa kutembelea kisiwa hicho kwa kusudi la kuanzisha usambazaji wa machapisho ya dhehebu letu; na kwa mwaliko, Mchungaji Flowers na mkewe waliwafuata muda mfupi baadaye kufanya kazi kadiri njia ilivyofunguka. Walifanikiwa vizuri hadi Mchungaji Flowers alipopatwa na homa, iliyosababisha kifo chake tarehe 29 Juni, 1894. Mchungaji E. W. Webster alichaguliwa kuchukua mahali pake, naye alisafiri kwa meli kutoka New York mnamo Agosti, 1895.
GSAM 432.2Katika mwaka 1896 watendakazi katika Visiwa vya India Magharibi walikuwa kama ifuatavyo: Huko Jamaika, Mchungaji A. J. Haysmer na W. W. Eastman; na wainjilisti kadhaa wa vitabu walikuwa katika Visiwa vya Bahama. Katika Antili Ndogo walikuwapo Mchungaji E. Van Deusen na mkewe, pamoja na C. F. Parmlee na mkewe wakiwa watendakazi wa Biblia, na Bwana Bean na Bwana Hackett wakiwa wainjilisti wa vitabu. Huko Trinidad, Mchungaji E. W. Webster na mkewe, pamoja na Binti Stella Colvin akiwa mmishenari wa tiba. Matokeo yalikuwa watunza Sabato mia moja na kumi katika Jamaika, na watunza Sabato hamsini katika Trinidad, waliokuwa wamekusanyika katika eneo la Couva; kanisa moja katika Barbados, na kundi moja katika Antigua, Antili Ndogo.
GSAM 432AMERIKA YA KATI
GSAM 432.3Mchungaji F. J. Hutchins na mkewe waliondoka Marekani kwenda Visiwa vya Ghuba, tarehe 16 Novemba, 1891. Wakati huo kulikuwapo watu wapatao ishirini, hasa katika Ruatan, waliokuwa wakiitunza Sabato ya amri ya nne kulingana na Amri Kumi; walikuwa wamevutwa kwanza kuuangalia ukweli huu kwa machapisho waliyotumiwa kwa posta. Miaka mitatu baadaye, katika mwaka 1894, W. A. Miller na mkewe waliondoka California kwenda Bonacca, ambako walijiunga na kazi ya elimu wakiwa walimu katika shule iliyofunguliwa tarehe 4 Julai, 1894, katika jengo la shule lililojengwa na Waadventista wa Sabato. Wastani wa mahudhurio katika muhula wa kwanza ulikuwa wanafunzi thelathini na wanne. Katika mwaka 1895 ilielezwa kwamba shule hiyo ilikuwa ikijitegemea, kwa kuwa idadi ya wanafunzi ilikuwa imeongezeka hadi arobaini na watano.
GSAM 433.1Katika mkutano wa Konferensi Kuu uliofanyika mwaka 1895, Mchungaji Hutchins aliripoti kuwapo kwa watu mia moja katika visiwa hivyo waliokuwa wakiutii ujumbe, naye pia alisema kwamba nyumba mbili za mikutano zilikuwa zimejengwa na zilimilikiwa na Waadventista wa Sabato. Kwa sababu ardhi ilikuwa haba, na kwa hiyo yenye thamani kubwa kwa kilimo, moja ya nyumba hizo za ibada ilijengwa juu ya maji. Hati za umiliki wa majengo haya mawili na jengo la shule zilikabidhiwa kwa Chama cha Konferensi Kuu. Thamani ya mali ya Konferensi katika kisiwa hicho ilikadiriwa kuwa $1,789.60. Thamani ya vitabu vilivyouzwa hadi mwaka 1895 ilikuwa $2,243.
GSAM 433Meli ndogo kwa ajili ya Amerika ya Kati
GSAM 433.2Baada ya Konferensi kuonyeshwa urahisi na faida za kuwa na meli ndogo ambayo ingetumiwa kuwasafirisha wamishenari kutoka kisiwa kimoja kwenda kingine, ilipigiwa kura kwamba chombo kama hicho kijengwe kwa ajili ya kazi katika Visiwa vya Ghuba, kwa gharama isiyozidi $3,000.
GSAM 433.3Katika mwaka 1896 kulikuwa na watendakazi wanne tu katika Amerika ya Kati: Mchungaji F. J. Hutchins na mkewe, na Mchungaji J. A. Morrow na mkewe katika Honduras ya Kihispania. Huko Belize, mji mkuu wa Honduras ya Kiingereza, kulikuwa na kundi la waumini waliokuwa wakiitunza siku ya saba kulingana na amri ya nne. Sehemu kubwa ya kazi katika eneo hili imefanywa katika visiwa vya Bahari ya Karibea. Hapa vitabu vya thamani ya dola elfu kadhaa vilikuwa vimeuzwa, na watu sitini walikuwa wakifurahia ukweli wa ujumbe wa malaika wa tatu.
GSAM 434Kifo cha Mchungaji Hutchins
GSAM 434.1Kwa miaka ipatayo kumi na miwili Mchungaji F. J. Hutchins alifanya kazi kwa uaminifu mkubwa na bidii katika eneo la Amerika ya Kati. Hatimaye nguvu zake zilishindwa, naye akafa kwa ugonjwa. Sasa amepumzika katika usingizi, akingojea mwito wa Bwana—mwito utakaowaamsha waaminifu.
GSAM 434AMERIKA YA KUSINI
GSAM 434.2Ilikuwa kwa njia ya machapisho kwamba mafundisho ya Waadventista wa Sabato yaliingizwa kwanza katika Amerika ya Kusini. Mnamo Oktoba, 1891, Mabwana Snyder, Stauffer, na Nowlin walianza kazi yao wakiwa wainjilisti wa vitabu katika Ajentina. Katika mwaka 1893, kwa uamuzi wa kura wa Konferensi Kuu, Mchungaji F. H. Westphal, kutoka Illinois, mchungaji Mjerumani, alijiunga na kazi katika eneo hili la umishenari; na katika mwaka 1894, Frank Kelley, kutoka California, alienda katika Muungano wa Majimbo ya Kolombia akiwa mmishenari anayejitegemea. Miezi michache baadaye, watendakazi wengine waliwafuata hawa, na hivyo kazi ikaanza katika misheni hii mpya. Katika mwaka 1896 taarifa ifuatayo ilitolewa kuhusu kazi katika eneo hili: Chile ina mchungaji mmoja, Mchungaji G. H. Baber, aliyefika tarehe 19 Oktoba, 1895; na wainjilisti wawili wa vitabu, F. W. Richards na F. H. Davis. Ajentina pia ina wachungaji wawili, F. H. Westphal na Jean Vuilleumier; na wainjilisti wawili wa vitabu, O. Oppegard na C. A. Nowlin. Zaidi ya hawa kuna watendakazi wanne wa Biblia, Lucy Post, Bwana na Bibi Snyder, na John McCarthy. Brazili ina wachungaji wawili, Mchungaji W. H. Thurston na H. F. Graf; na wainjilisti watatu wa vitabu, A. B. Stauffer, J. F. Berger na J. A. Berger. Guiana ya Kiingereza ina wachungaji wawili, Mchungaji W. G. Kneeland na Mchungaji P. Giddings; na wamishenari wawili wa tiba, Daktari B. J. Fercoit na mkewe.
GSAM 435.1Kufikia mwaka 1896, vitabu vya thamani ya dola elfu moja vilikuwa vimeuzwa katika Chile, na watunza Sabato thelathini walikuwa wameipokea Sabato na kweli zinazohusiana nayo kwa kusoma machapisho waliyonunua kwa wainjilisti wa vitabu. Katika Brazili na Ajentina vitabu vya thamani ya dola elfu kumi vilikuwa vimeuzwa; na lililokuwa bora zaidi, kulikuwa na watu mia moja waliokuwa wakiitunza Sabato. Kanisa moja na Shule tano za Sabato zilikuwa zimeanzishwa. Katika Ajentina kulikuwa na makanisa matatu yaliyoanzishwa rasmi, katika Buenos Aires, Crespo, na San Cristobal, kila mahali likiwapo moja. Pia kulikuwa na kanisa moja lililoanzishwa rasmi katika Guiana ya Kiingereza, na watunza Sabato hamsini, na kufanya jumla ya Waadventista wa Sabato mia moja na hamsini katika Amerika ya Kusini.
GSAM 435CHAMA CHA UMISHENARI CHA KUSINI
GSAM 435.2Kwa kusema kwa usahihi kabisa, chama hiki hakiwezi kuitwa cha nchi za nje, ingawa kinafanya kazi ya kuwahubiria injili watu wa kutoka nje (Waafrika) katika nchi yetu wenyewe. Sifa nyingi zinastahili kutolewa kwa juhudi za kudumu za Mchungaji J. E. White, chini ya baraka ya Mungu, kwa matokeo ambayo tayari yamepatikana.
GSAM 435.3Katika majira ya baridi ya 1893, nilipokuwa nikitumikia kama mwenyekiti wa Konferensi ya Illinois, Mchungaji White alikuja kwangu akiwa amelemewa sana na mzigo wa kuwasaidia watu weusi katika Majimbo ya Kusini. Kwa kuwa alikuwa anakaa Chicago kwa majuma machache, aliomba apewe nafasi ya kufanya kazi kwa ajili ya watu weusi waliokuwa wakiishi mjini humo. Ombi hilo lilikubaliwa kwa furaha kubwa, na hapo ndipo kwa kweli kazi yake kwa ajili ya watu hawa wenye taabu ilipoanzia.
GSAM 435Meli ya mvuke ya umishenari ya Mchungaji White
GSAM 435.4Tangu wakati huo alikuwa akiomba na kupanga kwa ajili ya eneo la kazi la Kusini. Alipokuwa akitafakari, mipango yake ilikomaa, na hatimaye ikazaa ujenzi wa meli ya mvuke karibu na Ziwa Michigan, iliyoitwa Nyota ya Asubuhi. Akiwa na “Betheli” hii inayoelea, alienda Chicago, na kutoka huko akateremka Mito ya Illinois na Mississippi, akafika Vicksburg, Mississippi, tarehe 10 Januari, 1895. Hapa, akiwa na washirika wachache, alianza kazi yake katika eneo ambalo halikuwa limewahi kufanyiwa kazi.
GSAM 436Kazi ya Chama cha Umishenari cha Kusini
GSAM 436.1Tunanukuu taarifa iliyotolewa na Mchungaji White katika mkutano wa Konferensi Kuu, tarehe 9 Aprili, 1903, inayoeleza matokeo ya kazi na kuonyesha hali ya kazi ya umishenari ya Kusini wakati huo:—
GSAM 436.2“Chama chetu kimejenga shule tano katika Mississippi na sasa kinaziendesha.... Shule hizi ziko Vicksburg, Yazoo City, Columbus, na Jackson.... Watendakazi wetu pia wameendeleza juhudi katika Nashville, Memphis, na Edgefield Junction, huko Tennessee, na katika Louisville na Bowling Green, huko Kentucky.
GSAM 436Watendakazi katika Kusini
GSAM 436.3“Kwa sasa kuna watendakazi ishirini na saba katika idara mbalimbali za Chama. Wachungaji watano waliowekewa mikono wameandaliwa katika kazi ya Chama cha Umishenari cha Kusini.... Walimu kumi na watatu wa shule wameandaliwa kwa njia mbalimbali kwa ajili ya kazi yao.... Kijana mmoja anasomeshwa na Chama ili awe daktari, katika Chuo cha Tiba cha Meharry, huko Nashville, na mwingine anasaidiwa katika masomo yake katika chuo hichohicho.... Watendakazi fulani wazuri wa Biblia wameandaliwa. Baadhi ya walimu pia wanakuwa watendakazi hodari katika idara hii.
GSAM 436Meli ya mvuke “Nyota ya Asubuhi”
GSAM 436.4“Nyota ya Asubuhi ni mali yangu binafsi, iliyojengwa kwa fedha zangu mwenyewe. Zaidi ya hayo, gharama zote za uendeshaji wa meli hii zimelipwa kutokana na mapato yangu mwenyewe. Nitasema pia kwamba gharama za maisha ndani ya meli zililipwa nami mwenyewe sikuzote. Mara nyingi kundi lilikuwa na watu kumi hadi kumi na wanane.... Hata mishahara ya watendakazi wote walioajiriwa na Chama kwa miaka mingi haikutolewa katika michango, bali katika mapato yangu binafsi.
GSAM 437Jinsi fedha zilivyopatikana kwa ajili ya misheni ya Kusini
GSAM 437.1“Huenda swali likaulizwa, ‘Fedha hizi mlizipata wapi?’ Bwana alitupatia. Vijitabu fulani vilichapishwa. Kwanza, Kitabu cha Mwanzo cha Injili, ambacho hapo awali kilikusudiwa kutumiwa katika kuwafundisha watu weusi. Mauzo ya nakala elfu chache yalitarajiwa, lakini kwa mshangao wetu yamefikia karibu nakala milioni moja.
GSAM 437.2“Mama [Bibi E. G. White] alitusaidia kwa kitabu Kristo Mwokozi Wetu, ambacho kiliuzwa nakala laki tatu au nne. Nakala laki mbili au tatu za Hadithi Bora Zaidi zimeuzwa. Inakadiriwa kwamba nakala za Mfalme Ajaye zilizosambazwa zinatosha kufanya nguzo yenye kimo cha maili nne. Kwa mapato ya haki za uandishi ya vitabu hivi, mbali na kugharimia shughuli nyingine nyingi na matawi ya kazi, tulijenga Nyota ya Asubuhi.”
GSAM 437KATIKA NCHI NYINGI
GSAM 437Meksiko
GSAM 437.3Kazi yetu katika nchi hii ilianza mwaka 1894, kwa kuanzishwa kwa misheni ya tiba katika Guadalajara. Katika mwaka 1896 kundi la watendakazi liliripotiwa kama ifuatavyo: Mchungaji D. T. Jones na mkewe, waliokuwa wakisimamia misheni hiyo. Walimu walikuwa Ora A. Osborne, Bibi A. Cooper, Kate Ross, na msaidizi mmoja mwenyeji. Wamishenari wa tiba walikuwa Daktari J. A. Neal, A. Cooper, Bibi A. J. Rice, Bibi Bartlett, na Bibi Rachel Flowers. Wagonjwa arobaini kwa siku walikuwa wakipata huduma katika misheni, na wanafunzi arobaini walihudhuria shule ya misheni. Wakati huo taasisi mpya ya tiba na mapumziko ilikuwa ikijengwa, kwa gharama ya $12,000.
GSAM 437Afrika ya Kati
GSAM 437.4Katika mwaka 1893 kazi ya ujumbe wa malaika wa tatu ilikuwa imeendelea sana kiasi kwamba Kamati ya Konferensi Kuu iliona kuwa kuna sababu za kupendekeza kuanzishwa kwa misheni katika Afrika ya Kati. Kwa hiyo ilipigiwa kura, “Kwamba mara tu itakapowezekana misheni ifunguliwe katika Matabeleland.” Kwa kupatana na uamuzi huu, kundi la Waadventista wa Sabato liliingia katika nchi hiyo mwaka 1894 na kuchagua shamba la ekari 12,000. Katika mkutano wa konferensi wa mwaka 1895, Mchungaji C. B. Tripp na mkewe, W. H. Anderson na mkewe, na Daktari A. S. Carmichael walichaguliwa kuwa wamishenari katika eneo hili la mbali. Mara moja walianza matayarisho ya safari ndefu, na baada ya safari njema ya baharini walifika walikokwenda tarehe 26 Julai, 1895.
GSAM 438Pwani ya Dhahabu
GSAM 438.1Kwa miaka kadhaa kilio cha Kimakedonia cha kuomba msaada kilikuwa kimewafikia Waadventista wa Sabato kutoka Pwani ya Magharibi ya Afrika. Shauku ya kuujua ukweli ilikuwa imeamshwa kwa kusoma machapisho ya Waadventista, lakini msaada haukutumwa hadi mwaka 1894 au karibu na wakati huo. Ndipo Mchungaji Sanford na Bwana Rudolph walipoalikwa na Kamati ya Konferensi Kuu kuanza kazi ambayo ilikuwa imengoja kwa muda mrefu sana. Waliingia katika eneo hilo kwa bidii na ujasiri. Hata hivyo, muda si mrefu baada ya hapo Mchungaji Sanford alipatwa na homa, ambayo imeenea huko sana hata nchi hiyo huitwa “kaburi la mzungu.” Alishikwa nayo mara tatu, kisha, ili aendelee kuishi, akalazimika kurudi Amerika. Wengine walitumwa katika Pwani ya Magharibi, miongoni mwao Mchungaji D. U. Hale, Geo. F. Kerr na mkewe, na G. P. Riggs. Hata hivyo, huyu wa mwisho alidhoofishwa sana na ugonjwa kiasi kwamba matumaini ya kuokoa maisha yake yalipotea, naye akakimbilia Uingereza kwa tumaini la kunufaika na mabadiliko ya hali ya hewa; katika hili yeye na rafiki zake walikatishwa tamaa, kwa kuwa alizidi kudhoofika polepole, na hatimaye akafa, na huko akazikwa. Yeye pia anangojea kuja kwa Mpaji wa Uzima.
GSAM 438India
GSAM 438.2Tarehe 12 Januari, 1890, Mchungaji Haskell alisafiri kwa meli kutoka bandari ya Durban, kwenye pwani ya kusini-mashariki ya Afrika, kwenda Calcutta, India, China, na Japani. Kabla ya tarehe hiyo, Percy T. Magan, katibu wake, alikuwa amejiunga naye. Kusudi la safari hii ya kwenda India lilikuwa kufanya uchunguzi wa awali ili kupata habari ambazo zingewawezesha kutoa mashauri na ushauri wakati Waadventista wa Sabato watakapoanza shughuli za umishenari kwa vitendo katika eneo hilo. Ikiwa na wazo la kuanzisha misheni katika India, Konferensi Kuu, katika mwaka 1893, ilipendekeza kwamba Wm. Lenker aende katika nchi hiyo akiwa mwinjilisti wa vitabu. Kwa kutekeleza pendekezo hili, alienda India na kuanzisha usambazaji wa machapisho ya Waadventista wa Sabato. Baadaye Bwana Lenker aliripoti kwamba yeye na watu wengine wanne walikuwa, hadi mwaka 1896, wametembelea sehemu mbalimbali za India wakifanya uinjilisti wa vitabu, na walikuwa wameuza machapisho yenye thamani ya $10,000. Ili kuonyesha shauku iliyoamshwa na vitabu vilivyouzwa, alisema zaidi kwamba alipokuwa akiuza vitabu karibu na Madras, kwenye pwani ya magharibi ya India, “mhubiri mmoja mwenyeji alitembea maili sitini ili kununua nakala ya Mawazo juu ya Danieli na Ufunuo.”
GSAM 439Georgia Burrus katika India
GSAM 439.1Katika mwaka 1895 Binti Georgia Burrus aliondoka California kwenda India. Alipofika huko alianza mara moja kujifunza lugha ya Kibengali, na muda mfupi baadaye akaanza kazi ya umishenari. Kufikia mwaka 1896 watu kadhaa walikuwa wameanza kuitunza Sabato ya Bwana kwa kushirikiana na watendakazi wetu.
GSAM 439.2Watendakazi katika eneo hilo mwaka 1896 walikuwa Mchungaji D. A. Robinson na mkewe. Binti May Taylor na Binti Georgia Burrus walikuwa watendakazi wa Biblia. Bwana Lenker na Bwana Masters walikuwa wainjilisti wa vitabu. Jengo linalofaa lilikuwa limepatikana kwa ajili ya makao ya misheni, na miito ya kutaka madaktari, wauguzi, na msaada zaidi ili kukidhi mahitaji yaliyokuwa yakiwabana ilikuwa imetumwa nchini kwetu. Mchungaji Brown, pamoja na wengine, aliitikia wito huu. Yeye na Mchungaji D. A. Robinson wote wawili walikufa huko Karmatar, Bengal, India, mwishoni mwa Desemba, 1899.
GSAM 439Hawaii, Visiwa vya Sandwich
GSAM 439.3Katika mwaka 1884, Bwana La Rue na Henry Scott walienda Hawaii wakiwa wamishenari, kwa gharama zao wenyewe. Walianza kazi yao kwa kuwafikia watu mmoja mmoja katika umishenari na kuuza vitabu. Hii iliamsha shauku kubwa sana katika kisiwa hicho hata Konferensi Kuu, mnamo Novemba, 1885, ilipiga kura kwamba Mchungaji Wm. Healy aende Hawaii kufanya kazi katika msimu uliofuata, na kwamba Konferensi ya California iombwe kuazimisha hema kwa kusudi hilo. Akiwa amepatiwa vifaa hivi, Mchungaji Healy na wale waliokuwa tayari katika kisiwa hicho waliendesha mkutano wa hemani katika majira ya joto ya 1886. Kutokana na juhudi hii watu kadhaa waliupokea ujumbe. Bwana La Rue alibaki Honolulu hadi mwaka 1889, aliposafiri kwa meli kwenda Hong Kong, China.
GSAM 440Kazi miongoni mwa Wachina katika Hawaii
GSAM 440.1Kazi kidogo tu ya kichungaji ilitolewa kwa kisiwa hicho hadi Konferensi Kuu ilipokutana katika mwezi wa Machi, 1895; wakati huo ilipigiwa kura kwamba “Mchungaji Gates na mkewe, pamoja na Bwana na Bibi Brand wakiwa walimu wa Wachina, waende Honolulu kushiriki katika kazi ya umishenari.” Kazi ya kufundisha ilianza mara moja, na Mchungaji Gates, ingawa afya yake ilikuwa dhaifu, alifanya aliloweza kuisukuma kazi mbele. Daktari na wauguzi waliwafuata wamishenari muda mfupi baadaye, na kazi katika tawi hilo la ujumbe ikaanza vizuri.
GSAM 440Muhtasari wa misheni, tarehe 1 Januari, 1903
GSAM 440.2Taarifa ya Katibu wa Umishenari wa Nchi za Nje, iliyotolewa tarehe 31 Desemba, 1902, inaeleza kazi ya ujumbe inavyoendeshwa nje ya Marekani kama ifuatavyo:—
GSAM 440.3Konferensi ya Muungano ya Australia, inayoundwa na konferensi za Victoria, New South Wales, Nyuzilandi, Queensland, Australia Kusini, Tasmania, na Australia Magharibi.
GSAM 440.4Konferensi Kuu ya Ulaya, inayoundwa na Konferensi ya Muungano ya Ujerumani, Ujerumani Magharibi, Ujerumani Mashariki, Ujerumani Kusini, Uholanzi na Ubelgiji ya Kiflamandi, Austria-Hungaria, na Nchi za Balkan, Uswisi ya Kijerumani, Urusi Kusini, Urusi Kaskazini, na Urusi ya Kati.
GSAM 440.5Konferensi ya Muungano ya Skandinavia, inayojumuisha Denmark, Norwe, Uswidi, Ufini, na Aisilandi.
GSAM 441.1Konferensi ya Muungano ya Uingereza, inayojumuisha Uingereza Kaskazini, Uingereza Kusini, Ayalandi, Uskoti, na Wales.
GSAM 441.2Konferensi ya Muungano ya Kifaransa na Kilatini, inayojumuisha Uswisi ya Kifaransa, Ufaransa, na Italia.
GSAM 441.3Misheni ya Mashariki, inayojumuisha Misri, Siria, na Uturuki.
GSAM 441.4Konferensi ya Muungano ya Afrika Kusini, inayojumuisha Koloni la Rasi, Natal-Transvaal, Basutoland, na Matabeleland.
GSAM 441.5Maeneo mengine mbalimbali: Bermuda, Brazili, Guiana ya Kiingereza na ya Kiholanzi, Amerika ya Kati (Kusini), China, Fiji, India, Jamaika, Japani, Antili Ndogo, Meksiko, Nyasaland, Pitcairn, Puerto Rico, Mto Plate, Raratonga, Samoa, Visiwa vya Society, Sumatra, Tonga, Trinidad, Pwani ya Magharibi (Amerika ya Kusini), na Pwani ya Magharibi (Afrika).
GSAM 441.6Idadi ya watendakazi wanaofanya kazi katika maeneo haya mbalimbali, wakiwamo wachungaji, wahubiri wenye leseni, watendakazi wa Biblia, wasambazaji wa vitabu, na wainjilisti wa vitabu, ni 754.
GSAM 441Vituo muhimu vya kazi vimeanzishwa
GSAM 441.7Kutokana na maelezo haya mafupi kuhusu misheni zetu tunaweza kusema, kama alivyosema Katibu wa Umishenari wa Nchi za Nje katika mwaka 1896:
GSAM 441.7“Kwa kuwa sasa ujumbe umejikita katika vituo hivi muhimu karibu kila sehemu ya ulimwengu, Mungu, kwa uwezo wake usio na kikomo, anaweza kutimiza kazi kubwa na yenye nguvu katika muda mfupi sana. Ataifupisha kazi yake katika haki.”
Maelezo ya chini ya ukurasa
- Warumi 15:21. ↩