Sura ya 11 — Ujumbe wa malaika wa pili
GSAM 171.1“Na malaika mwingine akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule mkuu, kwa sababu umewanywesha mataifa yote mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”1
GSAM 171.2“Ndipo mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika barabara na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na viwete, na vipofu.”2
GSAM 171.3Bwana, kupitia watumishi wake, alikuwa ameutikisa ulimwengu kwa ujumbe huu: “Saa ya hukumu yake imekuja,”—ujumbe ambao wote waliokiri kuwa watu wake wangeweza kuungana juu yake kama wangetaka. Huu ulikuwa mwito wa kwanza wa “karamu” ya arusi. Ulikuwa umetangazwa “kwa wale walioalikwa.”3 Kwa kuwa mwito huu ulikataliwa kwa visingizio mbalimbali, mwito wa pili ulitolewa, uliolingana na ujumbe wa malaika wa pili.4 Kwa mwito huu Bwana aliwatenga watu wa kusonga mbele hadi mwisho wa wakati, wakifuata nuru ya ukweli wake iliyozidi kuongezeka.
GSAM 171Mwito wa Pili wa Karamu ya Arusi
GSAM 171.4Ujumbe wa pili—ule unaofuata kilio cha saa ya hukumu—unasema, “Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule mkuu, kwa sababu umewanywesha mataifa yote mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.” Na mwito wa pili wa karamu unasema, “Tokeni upesi, mwende katika barabara na vichochoro vya mji, mkawalete hapa maskini, na vilema, na viwete, na vipofu.” Katika kila mojawapo ya maandiko haya, wale wanaokiri kuwa watu wa Bwana wanaitwa “mji.” Kwa sababu ya kanuni zao za imani zinazopingana na zenye machafuko, wanaitwa “Babeli.” Katika andiko lingine linalohusu nyakati za mwisho, tunaona kwamba muda mfupi kabla ya kuja kwa Bwana, watu wake wanaitwa watoke “Babeli:” “Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu, nao umekuwa makao ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na kizimba cha kila ndege mchafu na mwenye kuchukiza.... Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.”5
GSAM 172“Kumbuka Jinsi Ulivyosikia”
GSAM 172.1Katika ujumbe kwa kanisa la Sardi tunasoma, “Basi kumbuka jinsi ulivyopokea na kusikia, ukashike sana, ukatubu. Walakini usipokesha, nitakuja kwako kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako.”6 Kanisa la Sardi linaonekana kuwa lilitokana na Matengenezo ya Kanisa, baada ya kipindi cha giza cha kazi ya “Yezebeli”—kanisa lililoasi. Kanisa la Sardi liliambiwa kwamba hapo awali lilikuwa kanisa hai; lakini liliposikia na kukataa fundisho la kuja kwa Bwana, lilijiweka mahali ambapo tukio hilo lingeweza kulifikia ghafula kama “mwivi usiku.” Hivyo ndivyo mtume Paulo asemavyo katika 1 Wathesalonike 5:1-5, kwamba itakuwa hali ya wale wanaolia, “Amani na salama,” wakati kuja kwa Bwana kumekaribia. Wale wanaoifuata nuru ya ukweli wanaitwa “wana wa mchana,” na Bwana hatawajia kama mwivi.
GSAM 172.2Katika maelezo haya ya kinabii ya makanisa saba, tunaona kwamba kuanguka kwa kanisa la Sardi kunafuatwa mara moja na kanisa la Filadelfia, au (kama neno hilo linavyomaanisha) upendo wa kindugu. Hivyo ndivyo walivyokuwa wale waumini 50,000 ambao, kwa ujumbe wa malaika wa pili, walitolewa katika makanisa yote mbalimbali, wakaunganishwa katika kifungo kimoja cha upendo wa kindugu juu ya ukweli mkuu wa msingi wa ujio wa Kristo uliokuwa karibu sana.
GSAM 173Jinsi Ujumbe wa Pili Ulivyotangazwa
GSAM 173.1Gazeti la Kilio cha Usiku wa Manane la tarehe 12 Septemba 1844 lina maelezo yaliyotolewa na Mchungaji J. V. Himes kuhusu ujumbe wa malaika wa pili na hali zilizosababisha kutangazwa kwake. Barua yake imeandikwa McConnelsville, Ohio, tarehe 29 Agosti 1844, nayo inasema hivi:—
GSAM 173.2“Tulipoanza kazi pamoja na Ndugu Miller mwaka 1840, alikuwa ametoa mihadhara kwa miaka tisa. Katika muda huo alisimama karibu peke yake. Lakini kazi yake ilikuwa ya kudumu bila kukoma na yenye matokeo katika kuwaamsha wale waliokiri dini watambue tumaini la kweli la watu wa Mungu, na maandalizi yaliyohitajika kwa ajili ya ujio wa Bwana; na pia katika kuwaamsha watu wa tabaka zote ambao hawajaongoka watambue hali yao ya kupotea, na wajibu wa kutubu mara moja na kumgeukia Mungu, ili wajitayarishe kumlaki Bwana Arusi kwa amani atakapokuja. Hayo ndiyo yaliyokuwa makusudi makuu ya kazi yake. Hakujaribu kuwageuza watu wajiunge na dhehebu au kundi fulani la kidini.
GSAM 173.3“Tuliposadikishwa juu ya ukweli kwamba ujio ulikuwa karibu, na kulikubali fundisho hilo hadharani, tulikuwa na maoni hayohayo, nasi tukafuata njia hiyohiyo miongoni mwa madhehebu mbalimbali ambamo, kwa maongozi ya Mungu, tuliitwa kufanya kazi. Tuliwaambia wachungaji na makanisa kwamba haikuwa sehemu ya kazi yetu kuyavunja, au kuyagawa na kuleta machafuko ndani yake: Tulikuwa na kusudi moja lililo wazi, nalo lilikuwa kutoa ‘kilio,’ onyo la hukumu iliyokuwa ‘mlangoni,’ na kuwashawishi wanadamu wenzetu wajitayarishe kwa tukio hilo.... Wachungaji na washiriki waliofaidika na kazi yetu, lakini ambao hawakuwa wamelikubali fundisho hilo kwa moyo wa kweli, waliona kwamba iliwapasa ama kuambatana na fundisho hilo, kulihubiri na kulishikilia, au, katika saa ile ya kuamua iliyokuwa imewafikia, wangepata matatizo na waumini wenye msimamo thabiti na nia imara. Kwa hiyo waliamua kulipinga fundisho hilo, nao wakaazimia, wengine kwa njia moja na wengine kwa nyingine, kuzuia jambo hilo lisizungumzwe. Hilo liliwaweka ndugu na dada zetu waliokuwa miongoni mwao katika hali ya kujaribiwa sana. Wengi wao waliyapenda makanisa yao, wala hawakuweza kufikiria kuyaacha. Lakini walipodhihakiwa, kuonewa, na kwa njia mbalimbali kunyimwa haki na furaha walizokuwa nazo hapo awali, na walipozuiwa kupewa ‘chakula kwa wakati wake,’ na wimbo wa kuwalaghai wa ‘amani na salama’ ulipoimbwa masikioni mwao Sabato hadi Sabato, upesi waliacha upendeleo wao kwa makundi yao, wakainuka kwa nguvu zao kuu, wakaitupilia mbali nira, wakapaza kilio hiki: ‘Tokeni kwake, enyi watu wangu.’
GSAM 174Katika Hali ya Kujaribiwa
GSAM 174.1“Hali hii ilituweka katika majaribu, (1) Kwa sababu tulikuwa tumefikia mwisho kabisa wa wakati wetu wa kinabii, ambapo tulitarajia kwamba Bwana angewakusanya watu wake wote wawe kitu kimoja; na (2) sikuzote tulikuwa tumehubiri fundisho tofauti; na sasa kwa kuwa hali zilikuwa zimebadilika, tungalionekana kuwa watu wasio waaminifu ikiwa tungejiunga katika kilio cha kujitenga na kuvunjika kwa makanisa yaliyokuwa yametupokea sisi na ujumbe wetu. Kwa hiyo tulisita, na kuendelea kutenda kulingana na msimamo wetu wa kwanza, mpaka kanisa na wachungaji walipolifikisha jambo hilo mbali kiasi kwamba tukalazimika, kwa kumcha Mungu, kuchukua msimamo wa kuutetea ukweli na watoto wa Mungu waliokanyagwa.
GSAM 174Mfano wa Mitume kwa Njia Tuliyofuata
GSAM 174.2“‘Akaingia katika sinagogi, akanena kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana nao na kuwashawishi katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walipokuwa na mioyo migumu, wasiamini, wakiitukana Njia ile mbele ya makutano, akaondoka kwao, akawatenga wanafunzi, akihojiana kila siku katika shule ya mtu mmoja aitwaye Tirano.’7 Ilikuwa tu baada ya ‘wengine kuwa na mioyo migumu’ na ‘kuitukana Njia ile [kuja kwa Bwana] mbele ya makutano,’ ndipo ndugu zetu waliposukumwa kutoka na kujitenga na makanisa. Hawakuweza kuvumilia ‘matukano’ haya ya ‘watumwa waovu,’ na makanisa yaliyoweza kufuata njia ya uonevu na ‘matukano’ dhidi ya wale waliokuwa wakilitazamia ‘tumaini lenye baraka,’ kwao hayakuwa mengine bali binti za Babeli wa mafumbo. Waliyatangaza hivyo, nao wakaingia katika uhuru wa injili. Na ingawa huenda sisi sote tusikubaliane juu ya nini hasa kinachounda Babeli, tunakubaliana juu ya kujitenga mara moja na kabisa na wote wanaopinga fundisho la ujio na la ufalme wa Mungu uliokaribia. Tunaamini kwamba hili ni jambo la uzima na mauti. Ni mauti kuendelea kuungana na makundi hayo yanayodharau au kupinga kuja kwa Bwana. Ni uzima kutoka katika mapokeo yote ya wanadamu, na kusimama juu ya neno la Mungu, na kutazamia kila siku kuonekana kwa Bwana. Kwa hiyo sasa tunawaambia wote walionaswa kwa namna yoyote katika nira ya utumwa, ‘Tokeni kati yao, mkatengwe nao, asema Bwana, msiguse kitu kilicho najisi; nami nitawakaribisha, nami nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi.’”8
GSAM 175Upinzani Usioweza Kuelezeka
GSAM 175.1William Miller anasema hivi kuhusu mgongano uliokuwako wakati huo kati ya makanisa na Waadventista:—
GSAM 175.2“Ni kinyume kabisa na hali ya kawaida na ni jambo lisiloelezeka kwamba makanisa ya Kikristo yalikatae fundisho hili na kuwaondoa washiriki wao kwa sababu ya tumaini hili lenye baraka. Najua baadhi ya makanisa ya Wabaptisti yanasema kwamba hayawaondoi kwa sababu ya imani yao, bali kwa sababu ya kushiriki kwao Meza ya Bwana pamoja na waumini wa ujio. Basi ikiwa si kwa sababu ya imani yao katika Mwokozi ajaye, kwa nini mimi nimezuiwa kuhubiri katika mimbari zao, nami sijawahi kushiriki Meza ya Bwana isipokuwa katika kanisa la Wabaptisti? Hiki ni kisingizio cha uongo. Lakini hiki hakiwezi kuwa kisingizio cha Wamethodisti na Wapresbiteri; kwa maana wao wanaamini katika kushiriki Meza ya Bwana na watu wa madhehebu mbalimbali. Wanawaondoa kwa sababu gani? Nimesikia juu ya baadhi yao kuondolewa kwa sababu ya ‘kuimba’ nyimbo za ujio wa pili; wengine kwa sababu ya wazimu, ilhali wazimu wote uliothibitishwa dhidi yao ulikuwa kwamba walikuwa wakikesha wakimngojea Kristo. Ee Mungu, ‘uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.’”
GSAM 176Storrs Kuhusu Msimamo wa Makanisa
GSAM 176.1George Storrs alisema hivi kuhusu msimamo wa makanisa kwa Waadventista:—
GSAM 176.2“Ni lipi miongoni mwao, wakati huu, lisilosema, ‘Nimeketi kama malkia’? Na ni lipi miongoni mwao lisilojifurahisha kwa wazo kwamba siku moja litauteka ulimwengu, nao utatiishwa chini ya imani yake? Ni lipi miongoni mwao litakalomruhusu mtu abaki kwa amani ndani yake, ikiwa anakiri waziwazi na bila hofu imani yake kwamba ujio uko mlangoni? Je, masharti ya kubaki miongoni mwao bila kusumbuliwa si kwamba ‘uache kabisa’ kuikiri hadharani imani katika kuja kwa Bwana mwaka huu, bila kujali jinsi unavyosadiki jambo hilo, au jinsi unavyoona umuhimu wa kupaza kilio, ‘Mcheni Mungu, na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja’?”
GSAM 176Ushuhuda wa Mansfield
GSAM 176.3L. D. Mansfield, akiandika kutoka Oneida, N.Y., tarehe 21 Machi 1844, anashuhudia hivi:—
GSAM 176.4“Mungu anatenda katika mioyo ya watoto wake wapendwa wanaomngojea Bwana kutoka mbinguni, akiwaongoza wasimsikilize tu malaika ‘mwenye injili ya milele ya kuhubiri, akisema, Saa ya hukumu yake imekuja,’ bali pia waitii amri inayofuata, ‘Tokeni kwake, enyi watu wangu!’ Ninasadiki kwa ukamilifu zaidi kuliko hapo awali kwamba vyama vya kidini vya siku hizi vinaunda sehemu kubwa ya Babeli yule atakayeangushwa kwa nguvu, wala hataonekana tena kabisa.... Hata hivyo, inaonekana kwangu kwamba katika baadhi ya vyama hivyo kufanana kwake na pembe ndogo kunaonekana wazi sana. Mifano fulani itafafanua jambo hili.
GSAM 176Roho ya Umati Wenye Fujo Yadhihirika
GSAM 176.5“Ndugu mmoja aliyekuwa amefanya kazi kwa mafanikio makubwa katika eneo hili, akitangaza kuja kwa Bwana, alipanga kutoa mhadhara mahali fulani kwa wakati uliowekwa. Bwana alipanga mambo kiasi kwamba ndugu huyo alikuwa maili kumi na sita kutoka mahali pa mkutano huo, lakini mchungaji wa _____ alikuwapo, akiongoza umati wenye fujo, ukiwa na lami na manyoya, kwa kusudi la kumpaka lami na kumfunika manyoya yule mtumishi wa Mungu Aliye Juu Sana. Mchungaji huyohuyo alianza mikutano iliyoendelea kwa siku nyingi muda mfupi baadaye, lakini hali yote ilikuwa baridi na yenye kuganda kama mto wa barafu wa Kaskazini—hakuna mtu aliyeamshwa au kuongoka. Hatimaye mchungaji alisema kwamba aliamini ingembidi ‘kuketi kwenye kiti cha wanaotafuta wokovu.’
GSAM 177.1“Tangu tuanze kufanya mikutano hapa, kiongozi mmoja wa kikundi katika kijiji hiki aliwaambia wanakikundi wake kwamba ikiwa mtu yeyote angeingia nyumbani mwake na kusema anaamini Kristo atakuja mwaka huu, angemfukuza nje.”
GSAM 177Wajibu kwa Makanisa
GSAM 177.2Hapa tutatoa ushuhuda kutoka katika hotuba iliyotolewa kwa konferensi ya waumini wa ujio wa pili waliokusanyika Boston, Mass., yenye tarehe 31 Mei, 1844, na iliyotiwa sahihi na Wm. Miller, Elon Galusha, N. N. Whiting, Apollos Hale, na J. V. Himes. Wanasema:—
GSAM 177.3“Tunaweza pia kusema neno moja kuhusu wajibu wetu kwa makanisa. Hapa, kama ilivyo katika hali nyingine nyingi, tunaona kwamba hatari iko katika kupita kiasi upande wowote. Namna ya kwanza ya hatari hiyo ni kuruhusu mamlaka ya kanisa ambalo huenda sisi ni washiriki wake itunyamazishe katika jambo kama hili la wajibu. Hatuna shaka kwamba maelfu wamejiletea hukumu mbele za Mungu kwa kuyakubali madai yasiyopatana na Maandiko ya makanisa yao katika jambo hili. Kama wangekuwa thabiti na waaminifu, sasa wangekuwa katika hali salama zaidi na wenye manufaa zaidi, ingawa huenda pia wangeitwa kuteseka.
GSAM 177.4“Namna ya pili ya hatari ni kuikubali roho ya kulipiza kisasi dhidi ya makanisa kwa sababu ya udhalimu wao kwetu, na kupigana bila kubagua na mashirika yote ya namna hiyo. Kuhusu wajibu wa Waadventista kwa makanisa ambayo huenda wao ni washiriki wake, kama tungeombwa kutoa mwongozo, hatungeweza kutoa maagizo yoyote yanayoweza kutumika kwa wote. Lazima watende katika hofu ya Mungu, kulingana na hali ya kila jambo.
GSAM 178.1“Hata hivyo, tunapaswa kuwa thabiti katika kutimiza wajibu wetu, tukishuhudia ukweli katika kila nafasi inayofaa. Na ikiwa kwa kufuata njia hii tunayaudhi makanisa, nayo yanatutishia kutufukuza tusiponyamaza (ingawa, tukiona inafaa kuvunja uhusiano wetu na kanisa kwa amani, huenda hiyo ikawa njia bora zaidi), basi tutimize wajibu wetu, na tunapofukuzwa, tuvumilie udhalimu huo kwa subira, na tuwe tayari pamoja na Bwana wetu ‘kutoka nje ya lango, tukichukua shutuma zake.’”
GSAM 178.2Kutokana na nukuu hizi kuhusu matendo ya makanisa kwa wale waliokuwa wakitoa ujumbe wa malaika wa pili, ni rahisi kuona jinsi wale waliokusanywa katika zizi moja la kiroho, kama matokeo ya kwanza ya kutolewa kwa mwito huu wa pili wa “karamu ya jioni,” wanavyotajwa kuwa “vilema,” “viwete,” na “vipofu.” Maneno hayo yanaashiria kwa nguvu jinsi walivyotendewa vibaya kwa “kupigwa” na “watumishi wenzao,” ambao walikuwa wametengana nao.
GSAM 178Watu Waliojitenga Wachaguliwa Kupokea Kweli Mpya
GSAM 178.3Kusudi la Bwana linaweza kuonekana wazi katika kuitoa jamii ya watu walio tofauti na wengine kwa njia ya kutangazwa kwa ujumbe wa malaika wa pili—mwito wa pili wa “karamu ya jioni”—na “kilio cha usiku wa manane.” Kweli za thamani kwa siku za mwisho zilipaswa kuchunguzwa na kutangazwa. Kazi hiyo isingeweza kufanywa katika makanisa “yaliyofungwa na kanuni za imani,” kama vile kanisa la mitume lisingeweza kuhubiri injili kwa ulimwengu huku likidumisha uhusiano na madhehebu ya Kiyahudi. Mungu aliwaita watu wajitenge huko,9 Naye pia aliwaita waumini wa ujio wa pili wajitenge na wale ambao wangejaribu kuwazuia wasitoke nje ya mipaka ya kanuni zao za imani.
GSAM 179“Mahubiri Sita” ya Storrs
GSAM 179.1Muda mfupi baada ya kujitenga huku, tunaona kwamba nuru iliyafikia makundi ya waumini wa ujio wa pili kuhusu adhabu ya wakati ujao, kama ilivyoelezwa katika kijitabu cha George Storrs, “Mahubiri Sita.” Kilifundisha kwamba mwanadamu kwa asili ni wa kufa; kwamba wafu hawana fahamu kati ya kifo na ufufuo; kwamba adhabu ya mwisho ya wasiomcha Mungu itakuwa kuangamizwa kabisa; na kwamba kutokufa ni karama ya Mungu, inayopokewa kwa imani katika Bwana wetu Yesu Kristo pekee.
GSAM 179.2Maelfu ya Waadventista walikubali fundisho hili kuhusu asili ya mwanadamu, lakini si wote. Kulikataa hakukuleta machafuko kati yao, kwa kuwa lilionwa kuwa jambo la imani tu, wala si kipimo cha hali ya maadili ya mtu. Kwa hiyo jitihada zao za pamoja za kuuonya ulimwengu kuhusu kukaribia kwa Kristo hazikuvurugika. Hata hivyo, fundisho hilo liliamsha hasira ya makanisa dhidi yao.
GSAM 179Kushindwa Kuyakanusha “Mahubiri Sita”
GSAM 179.3Mchungaji wa Kimethodisti katika mji nilimoishi, ambaye hapo awali alikuwa amejiunga katika kuhubiri fundisho la ujio wa pili mwaka 1843, alipokea “Mahubiri Sita,” akayasoma, na kukiri kwa washiriki wa kanisa lake kwamba hakuweza kulikanusha fundisho hilo. Lakini alipoona kwamba wengi wa washiriki wa kanisa lake walikuwa wakilikubali, aliwashauri wengine wasikisome kitabu hicho, kwa kuwa “wangeliamini fundisho hilo kama wangekisoma.” Katika mwezi wa Septemba, 1844, baada ya mchungaji huyo kurudi kutoka kwenye konferensi ya kila mwaka, alisimama mimbarani mwake na kulikana hadharani fundisho la ujio wa pili, na kwa unyenyekevu akaliomba kanisa limsamehe kwa kuwahi kuwaalika wahadhiri kuzungumza katika nyumba hiyo ya ibada.
GSAM 179Kushtakiwa kwa Uzushi
GSAM 179.4Muda mfupi baada ya tendo hili la mchungaji, juhudi zilifanywa za kuwachukulia hatua waumini wa ujio wa pili kwa kosa la uzushi. Lakini kwa kuwa waliruhusiwa kutetea kesi zao kwa Biblia, kanisa halikupata ushindi. Watu kadhaa walifukuzwa katika kanisa hili kwa sababu mwenendo wao haukupatana na kanuni za kanisa, na wengine wengi walijiondoa kwa sababu ya kufukuzwa huku kwa washiriki ambao imani yao haikuweza kuonyeshwa kuwa kinyume na Maandiko. Hivyo fundisho la ujio wa pili likafungiwa nje milele katika kanisa ambalo mamia walikuwa wamempata Mwokozi na kufanywa wenye furaha katika Mungu.
GSAM 180.1Yale yaliyofanywa katika mji niliozaliwa yalifanywa pia katika mamia ya makanisa mengine kotekote nchini. Wale waliotendewa hivyo na ndugu zao wa zamani walipata faraja kubwa katika maneno ya nabii Isaya: “Lisikieni neno la Bwana, ninyi mlitetemekao kwa neno lake: Ndugu zenu waliowachukia, waliowatupa nje kwa ajili ya jina langu, walisema, Na atukuzwe Bwana; lakini yeye atatokea kwa furaha yenu, nao watatahayari.”10
GSAM 180Ghadhabu ya Waovu Yadhihirishwa
GSAM 180.2Kadiri siku ambayo Bwana alitarajiwa kuja ilivyokaribia, waumini walizidi kujitahidi katika kazi zao, na waovu walizidi kughadhabika na kudhihaki kwa ukali zaidi, kama itakavyoonekana katika taarifa ifuatayo iliyotolewa na mhariri wa gazeti la Kilio cha Usiku wa Manane (Midnight Cry) la tarehe 31 Oktoba, 1844:—
GSAM 180.3“Athari ambayo vuguvugu hili lilikuwa nayo kwa waovu pia ilisaidia sana kututhibitisha katika imani yetu kwamba Mungu alikuwa ndani yake. Watoto wa Mungu walipokusanyika kusujudu na kujinyenyekeza mbele zake, na kujiandaa kwa kuonekana kwake, kama ilivyowapasa kufanya watu wenye dhambi ambao wangeweza kuokolewa kwa neema tu, waovu walionyesha chuki kubwa kabisa. Tulipokuwa hatujatangaza mikutano yetu isipokuwa katika gazeti letu wenyewe, wala kuualika umma huko, wana wa Beliali walisongamana ndani yake na kusababisha fujo nyingi. Jioni ya Jumamosi, tarehe 12 ya mwezi huu [12 Oktoba, 1844], hatukufanya mkutano katika nyumba ya ibada, ili mtunzaji wa nyumba hiyo [msafishaji] apate nafasi ya kuisafisha kwa ajili ya Sabato [Jumapili]. Lakini kundi la wafanya fujo liliivamia nyumba hiyo, likamnyima hata nafasi hiyo. Hata hivyo, meya, bila kuombwa, aliingilia kati mara moja na kuwafukuza.
GSAM 181.1“Katika mikutano yetu siku ya Sabato iliyofuata, baada ya nyumba ya ibada kujaa, umati mkubwa ulijaa barabarani mbele ya jengo hilo, wengi wao wakiwa wamekasirika kwamba kuna watu walioamini katika ujio wa Bwana. Jioni, kwa sababu ya msisimko wa watu, hakukuwa na mkutano; hata hivyo barabara ilijaa kundi la wafanya fujo tangu mapema. Lakini meya na polisi wake wenye uwezo waliingilia kati upesi na kuwaondoa watu barabarani, baada ya kuwapeleka wachache katika kituo cha walinzi. Hatukuweza kuufananisha mwenendo wa kundi hilo na kitu kingine isipokuwa ule wa watu waliouzunguka mlango wa Lutu, jioni iliyotangulia kuangamizwa kwa Sodoma.... Kitendo hiki chao kilitokea kwa ghafula sana, kwa wakati mmoja na katika maeneo mengi sana, hata kujitokeza kwake siku ya kwanza ya mwezi wa saba wa Kiyahudi kulituthibitisha katika maoni yetu kwamba huu lazima ndio mwezi ule.”
GSAM 181Wenye Mzaha Wavaa Mavazi ya Kupaa Mbinguni
GSAM 181.2Tarehe 22 Oktoba, 1844, siku ambayo siku 2300 zilimalizika, huko Paris, Maine, waumini walipokuwa wamekusanyika katika nyumba ya ibada, wakimwomba Mungu kwa dhati kwa matarajio kwamba Bwana angekuja siku hiyo, wenye mzaha na dhihaka walikusanyika kuizunguka nyumba hiyo, wakiimba nyimbo za kukejeli. Wawili wa watu hao wenye fujo walivaa mavazi marefu meupe na kupanda juu ya paa la nyumba hiyo, wakaimba nyimbo na kuwadhihaki wale waliokuwa ndani, wakiomba na kungojea Bwana aje.
GSAM 181.3Yawezekana uongo ulioenezwa kuhusu Waadventista kuvaa mavazi ya kupaa mbinguni ulianzia katika tukio hili. Kwa maana ingawa magazeti ya ujio wa pili yametoa zawadi zinazofikia $500 kwa mfano mmoja uliothibitishwa wa Mwadventista aliyevaa vazi la kupaa mbinguni mwaka 1844, na hivyo akangojea Bwana aje, hakuna hata mfano mmoja uliowahi kutolewa.
GSAM 182Njozi ya Hazen Foss, 1844
GSAM 182.1Karibu na wakati huu, kijana aliyeitwa Hazen Foss aliishi Poland, Maine. Aliamini kwa uthabiti kwamba Bwana angekuja siku ya kumi ya mwezi wa saba. Alikuwa mtu mwenye sura nzuri, namna ya kusema iliyowavutia watu, na elimu nzuri kiasi. Majuma machache kabla ya “kilio cha usiku wa manane” kumalizika, Bwana alimkaribia na kumpa njozi, ambamo alionyeshwa safari ya watu wa ujio wa pili kwenda kwenye mji wa Mungu, pamoja na hatari zao. Alipewa jumbe fulani za maonyo ambazo alipaswa kuzitoa, na pia alionyeshwa majaribu na mateso ambayo yangefuata kama angekuwa mwaminifu katika kusimulia yale aliyoonyeshwa. Yeye, kama Bwana Foy, alionyeshwa hatua tatu ambazo kwazo watu wa Mungu wangefika kikamilifu kwenye njia ya kwenda kwenye mji mtakatifu. Kwa kuwa aliamini kwa uthabiti kwamba Bwana angekuja “baada ya siku chache zaidi” (kama walivyoimba wakati huo), hakuweza kuelewa sehemu ya njozi iliyohusu zile hatua tatu za kuingia kwenye njia. Na kwa kuwa kwa asili alikuwa na roho ya kiburi, aliukwepa msalaba, akakataa kuisimulia. Alipewa njozi ile mara ya pili, na zaidi ya hayo akaambiwa kwamba kama bado angekataa kusimulia aliyoonyeshwa, mzigo ungeondolewa kwake na kupewa mmoja wa watoto wa Bwana walio dhaifu zaidi, mtu ambaye angesimulia kwa uaminifu yale ambayo Mungu angemfunulia. Alikataa tena. Ndipo akapewa njozi ya tatu na kuambiwa kwamba ameondolewa jukumu hilo, na mzigo umewekwa juu ya mmoja wa walio dhaifu kuliko wote, ambaye angefanya aliyoagizwa na Bwana.
GSAM 182Foss Ashindwa Kuisimulia Njozi Yake
GSAM 182.2Jambo hili lilimshtua kijana huyo, naye akaamua kusimulia aliyoonyeshwa, kwa hiyo akatangaza wakati wa mkutano wake. Watu walikusanyika kwa wingi kuona na kusikia. Alisimulia kwa makini uzoefu wake, jinsi alivyokataa kusimulia yale ambayo Bwana alikuwa amemwonyesha, na yale ambayo yangetokana na kukataa kwake. “Sasa,” akasema, “nitaisimulia njozi.” Lakini ole wake! Alikuwa amechelewa mno: alisimama mbele ya watu akiwa bubu kama sanamu, na mwishowe akasema kwa uchungu mkubwa kabisa, “Siwezi kukumbuka hata neno moja la njozi ile.” Alikunjakunja mikono kwa uchungu, akisema, “Mungu ametimiza neno lake. Ameniondolea njozi,” na akiwa na fadhaa kubwa moyoni akasema, “Mimi ni mtu aliyepotea.” Tangu wakati huo alipoteza tumaini lake katika Kristo, akaingia katika hali ya kukata tamaa. Hakuhudhuria tena mkutano wa Waadventista, wala hakuwa na shauku binafsi katika mambo ya dini. Mwenendo wake katika mambo mengi, tukisema kwa upole, umekuwa ule wa mtu aliyenyimwa mvuto mpole wa Roho wa Bwana, wa mtu “aliyeachwa afuate njia zake mwenyewe, ashibishwe kwa matendo yake mwenyewe.” Alikufa mwaka 1893 akiwa katika hali hii ya moyo.
GSAM 183Njozi ya Foss Yasimuliwa na Mtu Mwingine
GSAM 183.1Karibu miezi mitatu tangu aliposhindwa kuikumbuka njozi yake, alisikia kutoka chumba cha jirani njozi ikisimuliwa na mtu mwingine. Mkutano huo ulifanyika katika nyumba ya kuishi ambayo yeye alikuwamo. Alihimizwa aingie katika mkutano, lakini akakataa kufanya hivyo. Alisema kwamba njozi hiyo ilifanana kwa karibu sana na ile aliyoonyeshwa, kama watu wawili wanavyoweza kusimulia jambo lilelile. Na hivyo yakajulikana yale aliyoyaona lakini akashindwa kuyakumbuka alipojaribu kuyasimulia. Baadaye alipomwona mtu huyo, alisema, “Huyo ndiye chombo ambacho Bwana ameweka mzigo juu yake.”
GSAM 183Kukatishwa Tamaa kwa Huzuni Kubwa
GSAM 183.2Hatimaye siku ya kumi ya mwezi wa saba kwa hesabu ya wakati ya Kiyahudi (22 Oktoba, 1844) ikafika. Iliwakuta maelfu kwa maelfu wakiutazamia wakati huo kwa ajili ya kutimizwa kwa matumaini yao. Hawakuwa wamefanya maandalizi yoyote ya mambo ya duniani kwa wakati wa baada ya tarehe hiyo. Hata hawakuwa wameliwazia wazo hili, “ikiwa hatakuja,” bali walikuwa wamepanga mambo yao ya duniani kama vile wangekuwa wakitarajia kwamba siku hiyo ingemaliza kipindi cha maisha yao ya kawaida. Walikuwa wamewaonya na kuwasihi waovu waikimbie ghadhabu inayokuja, na wengi wa hao waliogopa kwamba ujumbe huo ungeweza kuwa wa kweli. Walikuwa wamewashauri na kuomba pamoja na jamaa zao, na walikuwa wamewaaga wale miongoni mwao ambao hawakuwa wamempa Mungu mioyo yao. Kwa ufupi, walikuwa wameyaaga mambo yote ya duniani kwa uzito wote wa mtu anayejiona kuwa karibu kuonekana uso kwa uso mbele ya Hakimu wa dunia yote. Hivyo, wakiwa na wasiwasi uliokaribia kuwazuia kupumua, walikusanyika katika mahali pao pa ibada, wakitarajia kila dakika kusikia “sauti ya malaika mkuu na parapanda ya Mungu,” na kuziona mbingu zikiwaka kwa utukufu wa Mfalme wao anayekuja.
GSAM 184.1Saa zilipita polepole, na hatimaye jua lilipozama chini ya upeo wa magharibi, siku ya kumi ya mwezi wa saba wa Kiyahudi ilikuwa imekwisha. Vivuli vya usiku vilitanda tena juu ya ulimwengu kama sanda ya huzuni. Lakini pamoja na giza hilo, uchungu wa huzuni uliingia mioyoni mwa waumini wa ujio wa pili, huzuni ambayo kwa namna yake ingeweza kulinganishwa tu na huzuni ya wanafunzi wa Bwana wetu, waliposhika njia kurudi makwao kwa uzito moyoni katika usiku uliofuata kusulubiwa na kuzikwa kwa yule ambaye, muda mfupi tu uliotangulia, walikuwa wamemsindikiza kwa shangwe kuingia Yerusalemu kama Mfalme wao.