Sura ya 25 — Taasisi za elimu
GSAM 391.1“Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usisahau, wala usiyaache maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakuhifadhi; umpende, naye atakulinda. Hekima ndiyo jambo kuu; kwa hiyo jipatie hekima; na katika yote unayojipatia, jipatie ufahamu.”1
GSAM 391Shule ya Profesa G. H. Bell
GSAM 391.2Kazi ya elimu ya dhehebu imepanuka kwa kiasi kikubwa wakati huu. Kama matawi mengine ya kazi yaliyotajwa hapo awali, ilikuwa na mwanzo mdogo sana. Mwaka 1868 Profesa G. H. Bell alifungua shule katika jengo la zamani la ofisi, kwenye kona ya kaskazini-mashariki ya mitaa ya Kalamazoo na Washington, Battle Creek. Zaidi ya hayo, katika majira ya kuchipua ya mwaka 1871, baada ya kufungwa kwa Konferensi Kuu, yalifanywa mafunzo ya mihadhara kwa wachungaji kwa muda wa majuma manne, kwa kusudi la kuwasaidia wale waliohusika katika uchungaji na kazi ya kanisa.
GSAM 391Wito wa Kuwa na Shule ya Dhehebu
GSAM 391.3Katika Mapitio na Mbiu la Aprili 16, 1872, kulikuwa na makala yenye kichwa, “Je, Tuwe na Shule ya Dhehebu?” iliyofafanua wazi haja ya shule kama hiyo. Katika Mapitio na Mbiu la Julai 16 ilitangazwa kwamba shule ilifunguliwa ikiwa na wanafunzi kumi na wawili, ambao baada ya majuma mawili walikuwa wameongezeka hadi ishirini na watano, na darasa la jioni la sarufi lenye wanafunzi hamsini lilikuwa limeanzishwa. Muhula wa pili wa shule ulianza Septemba 16, 1872, ukiwa na wanafunzi arobaini. Kufikia Desemba 16 shule ilikuwa imekua sana hata ikahamishiwa katika jengo la ibada, ambamo madawati yanayokunjwa yaliunganishwa nyuma ya viti virefu vya kanisa. Sehemu ya elimu ya msingi yenye wanafunzi sitini na watatu pia iliendeshwa katika roshani ya kanisa.
GSAM 392Fedha Zachangwa kwa Ajili ya Chuo
GSAM 392.1Konferensi Kuu ya Machi, 1873, ilitumia muda mwingi kufikiria kama ilifaa kuchangisha fedha za kujenga majengo yanayofaa kwa kuendeshea shule ya dhehebu, ambamo watendakazi wangetayarishwa kuingia katika maeneo mbalimbali ya kazi. Jambo hilo lilipokubaliwa, kamati iliteuliwa kushughulikia ukusanyaji wa fedha zilizohitajika. Katika kipindi hicho, makala zenye hoja thabiti na za maana kuhusu jambo hili ziliandikwa na Wachungaji Butler, White, na wengine, na kuchapishwa mara kwa mara katika Mapitio na Mbiu. Kwa juhudi za Wachungaji Butler na Haskell katika mikutano mbalimbali ya makambi, fedha nyingi zilichangwa kwa ajili ya shule iliyopendekezwa.
GSAM 392.2Kikao kingine cha Konferensi kilifanyika Novemba 16, 1873, ambapo iliripotiwa kwamba ahadi za michango ya $52,000 zilikuwa tayari zimetolewa kwa mfuko wa elimu wa Waadventista wa Sabato, kwa ajili ya kupata ardhi na kujenga majengo yanayofaa katika msimu uliofuata. Katika kikao hicho hicho, kwa kura, kamati ya watu saba ilichaguliwa kuunda chama cha elimu na kupata mahali pa kujenga majengo hayo.
GSAM 392.3Katika konferensi iliyotajwa hapo juu, George I. Butler alichaguliwa kuwa Rais wa Konferensi Kuu, na Sidney Brownsberger kuwa Katibu. Wajumbe wa kamati iliyochaguliwa na Konferensi Kuu walikuwa George I. Butler, S. N. Haskell, na Harmon Lindsay. Majina ya James White, Ira Abbey, J. N. Andrews, na Uriah Smith yaliongezwa ili washirikiane na Kamati ya Konferensi Kuu kuwa Kamati ya Watu Saba, iliyosajiliwa kisheria kwa jina la “Chama cha Elimu cha Waadventista wa Sabato.” Tangu wakati huo Profesa Brownsberger alihusika na Chuo cha Battle Creek hadi alipoitwa kwenda kuongoza chuo kilichokuwa karibu kufunguliwa huko Healdsburg, California.
GSAM 393Ekari Kumi na Mbili Zanunuliwa kwa Ajili ya Chuo
GSAM 393.1Desemba 31, 1873, kamati hii ilinunua ekari kumi na mbili za ardhi katika sehemu ya magharibi ya Battle Creek, ambapo ekari saba kati yake zikawa eneo la Chuo cha Battle Creek.
GSAM 393.2Shule ya dhehebu ya Battle Creek ilianza muhula wake wa majira ya baridi katika vyumba vya jengo la tatu la ofisi Desemba 15, 1873, ikiwa na wanafunzi mia moja na kumi walioandikishwa.
GSAM 393Haja ya Shule za Dhehebu
GSAM 393.3Kuhusu haja yetu, kama dhehebu, ya kuwa na shule zinazotoa elimu inayofaa, Bibi White aliandika mwaka 1873 kama ifuatavyo:—
GSAM 393.4“Uwezo wote wa akili unapaswa kutumiwa na kukuzwa, ili wanaume na wanawake wawe na akili zilizositawi kwa uwiano. Ulimwengu umejaa wanaume na wanawake waliositawi upande mmoja tu, ambao wamekuwa hivyo kwa sababu baadhi ya vipawa vyao vilikuzwa huku vingine vikidumaa kwa kukosa kutumiwa. Elimu ya vijana wengi imeshindwa kutimiza kusudi lake. Wanasoma kupita kiasi huku wakipuuza mambo yanayohusu maisha ya utendaji na shughuli za kila siku....
GSAM 393Elimu Yenye Uwiano Yahitajika
GSAM 393.5“Kujishughulisha daima na masomo, kwa jinsi shule zinavyoendeshwa sasa, kunawafanya vijana wasifae kwa maisha ya utendaji. Akili ya mwanadamu lazima ifanye kazi. Isipotenda katika njia iliyo sawa, itatenda katika njia isiyo sawa. Ili kuhifadhi uwiano wa akili, kazi na masomo vinapaswa kuunganishwa shuleni.
GSAM 393.6“Katika vizazi vilivyopita, maandalizi yalipaswa kufanywa ili kutoa elimu kwa upana zaidi. Shule zilipaswa kuhusishwa na mashamba na sehemu za utengenezaji wa bidhaa. Walimu wa kazi za nyumbani walipaswa kuwapo, na sehemu ya muda wa kila siku ilipaswa kutengwa kwa kazi, ili nguvu za mwili na akili zitumike kwa usawa. Kama shule zingeanzishwa kwa mpango tulioutaja, sasa kusingekuwa na akili nyingi zisizo na uwiano.”2
GSAM 394Chuo cha Battle Creek
GSAM 394.1Katika majira ya kiangazi na ya vuli ya mwaka 1874, jengo la Chuo cha Battle Creek lilijengwa. Lilikuwa jengo la matofali lenye ghorofa tatu juu ya sehemu ya chini ya ardhi, lenye vipimo vya futi 75 x 75, katika umbo la msalaba wa Kigiriki. Lilikamilika na kuwekwa wakfu kwa shughuli zinazofaa Januari 4, 1875. Shule ilifunguliwa katika jengo hili ikiwa na wanafunzi zaidi ya mia moja na walimu saba wenye uwezo kwa idara mbalimbali. Chuo kilipofunguliwa katika mwaka wa masomo wa 1877, iliripotiwa kwamba wanafunzi mia mbili walikuwa wakihudhuria. Ripoti ya Chama cha Elimu iliyotolewa katika Konferensi Kuu ya Oktoba, 1880, ilionyesha kwamba wanafunzi 1400 walikuwa wameandikishwa katika Chuo cha Battle Creek tangu 1873 hadi Desemba, 1880.
GSAM 394Shule Nyingine Mbili Zafunguliwa
GSAM 394.2Katika Konferensi Kuu ya Desemba, 1882, iliripotiwa kwamba shule mbili za dhehebu zilikuwa zimefunguliwa chini ya usimamizi wa konferensi katika mwaka huo. Moja ilikuwa Chuo cha Healdsburg, huko Healdsburg, California, kilichofunguliwa Aprili 11; nyingine ilikuwa Akademia ya South Lancaster, huko South Lancaster, Massachusetts, iliyofunguliwa Aprili 19.
GSAM 394Chuo cha Healdsburg
GSAM 394.3Katika Mapitio na Mbiu la Januari 15, 1884, yalichapishwa maelezo yafuatayo yenye kuvutia kuhusu shule ya dhehebu ya Pwani ya Pasifiki:—
GSAM 394.4“Katika Septemba, 1881, Konferensi ya California iliamua kufungua shule ya dhehebu, na ikateua kamati kutekeleza jambo hilo. Kufikia Aprili, 1882, ardhi ya kutosha pamoja na jengo linalofaa lenye vyumba kumi vilikuwa vimenunuliwa, walimu wawili walikuwa wameajiriwa, na shule yenye wanafunzi thelathini na watatu ilikuwa imeanza. Katika mwaka wa masomo wa chuo (ulioanza Julai 29, 1882), shule ilisajiliwa rasmi kuwa chuo, kipande kingine cha ardhi cha ekari tano kikanunuliwa, jengo pana [kwa ajili ya makazi ya wanafunzi] likajengwa, walimu sita wakapatikana, na wanafunzi 152 wakaandikishwa. Tangu kufunguliwa kwake, ahadi za kutoa karibu $27,000 zilikuwa zimetolewa kwa ajili ya kazi hiyo, na sehemu kubwa ya fedha hizo imelipwa na watu wa California.”
GSAM 395Akademia ya South Lancaster
GSAM 395.1Watu wa New England walianzisha shule yao katika nyumba ya ibada huko South Lancaster, Massachusetts. Kwa juhudi zisizokoma za Mchungaji S. N. Haskell na kujitoa mhanga kwa watu wetu huko New England, majengo kadhaa ya shule yalikuwa tayari kuwekwa wakfu katika majira ya vuli ya mwaka 1884. Majengo yaliyokuwa mali ya Chama cha Akademia ya South Lancaster wakati huo yalikuwa matano, mawili yakiwa mapya kabisa. Jengo la akademia lilikuwa na vipimo vya futi 60 x 65, na jengo lingine jipya, la makazi ya wanafunzi, lilikuwa futi 36 x 88. Haya yaliwekwa wakfu Oktoba 19, 1884.
GSAM 395.2Taasisi hii, baada ya miaka ishirini na moja ya huduma yenye matokeo mazuri, ingali inafanikiwa, na imewatuma watendakazi wenye bidii katika kazi ya Bwana kwenda sehemu mbalimbali za ulimwengu. Mkuu wa akademia kwa sasa ni Frederick Griggs, ambaye pia ni katibu wa Idara ya Elimu ya Konferensi Kuu.
GSAM 395Shule ya Mafunzo ya London (Uingereza)
GSAM 395.3Kazi huko London, Uingereza, ilipoendelea kusonga mbele na kupata nguvu, ilionekana inafaa katika majira ya kiangazi ya mwaka 1887 kufungua shule ya mafunzo kwa watendakazi wa Biblia, ambayo ingeambatana na kazi halisi ya kufundisha Biblia. Kutoka katika shule hii watendakazi wametumwa kufanya kazi katika sehemu nyingine za Ufalme wa Muungano na katika Makoloni. Kwa sasa shule inayostawi inaendeshwa katika Ukumbi wa Duncombe, Kaskazini mwa London, chini ya uongozi wa Profesa H. R. Salisbury, aliyepata elimu yake ya awali katika chuo cha Battle Creek, Michigan.
GSAM 396Chuo cha Battle Creek Chapanuliwa
GSAM 396.1Haja ya nafasi zaidi katika Chuo cha Battle Creek ilikuwa kubwa sana hata ikawa lazima katika majira ya kiangazi ya mwaka 1886 kuongeza sehemu kubwa katika jengo la chuo, na mwaka uliofuata (1887), kujenga bweni (linalojulikana kama Bweni la Magharibi) kwa wanafunzi wa kike. Bweni la Magharibi lina vyumba vya wanafunzi 150, na watu 225 wanaweza kupata nafasi katika ukumbi wa kulia chakula; huku Bweni la Kusini, lililojengwa mwaka 1884 upande wa kusini wa eneo la chuo, likitumika kuwa bweni la wanafunzi wa kiume. Chuo kilipofunguliwa kwa muhula wa majira ya baridi wa 1886-87, wanafunzi 568 walikuwa wakihudhuria.
GSAM 396.2Mwaka 1885 Profesa W. W. Prescott aliwekwa kuwa mkuu wa Chuo cha Battle Creek, na muda mfupi baadaye akateuliwa kuwa Katibu wa Elimu wa dhehebu. Ilithibitika kwamba huo ulikuwa uamuzi wa busara. Chuo cha Battle Creek kilinufaika, na pia kwa juhudi za katibu huyo, pamoja na baraka za Mungu, umoja wa karibu zaidi na ufanisi mkubwa zaidi vilipatikana katika kazi ya shule zote za dhehebu letu.
GSAM 396Chuo cha Umishenari cha Emmanuel
GSAM 396.3Chuo cha Battle Creek kilitoa huduma yenye matokeo mazuri hadi mwaka 1901, ambapo ardhi na majengo yake viliuzwa kwa Chama cha Chuo cha Marekani cha Umishenari wa Kitabibu, na chama cha elimu kikavunjwa. Shirika jipya la chuo likaundwa mara moja, likaitwa Chuo cha Umishenari cha Emmanuel. Shamba lilipatikana karibu na Berrien Springs, kusini-magharibi mwa Michigan, ambako wanafunzi wamejenga majengo, na shule inayostawi inaendeshwa. Kusudi thabiti la shule hii ni kutoa “elimu ya pande zote,” kulingana na maelekezo yaliyonukuliwa katika sehemu ya mwanzo ya sura hii. Kuwafundisha watendakazi walio tayari kikamilifu kufanya kazi katika sehemu yoyote ya ulimwengu ambako wanaweza kuitwa kutumika kwa maongozi ya Mungu, ndiyo shauku na lengo kuu la walimu wa Chuo cha Umishenari cha Emmanuel.
GSAM 397Shule Kuu ya Biblia, Chicago, Illinois
GSAM 397.1Katika toleo la Mapitio na Mbiu la Machi, 1887, Mchungaji George I. Butler alipendekeza kwamba jengo la umishenari lijengwe huko Chicago, Illinois, ambalo lingetumika kuwa shule kuu ya Biblia kwa kuwafundisha watendakazi wa Biblia, na wakati huohuo lingeweza kutumika kuwa nyumba ya ibada na kituo cha umishenari kwa watu wetu katika mji huo. Katika majira ya vuli na ya baridi ya 1888-89 jengo hilo lilijengwa. Gharama, pamoja na viwanja, nyumba, samani, na kadhalika, ilikuwa karibu $28,000. Lilifunguliwa rasmi Aprili 4, 1889, kwa mafunzo maalumu ya wainjilisti wa vitabu. Wakati wa kuwekwa wakfu, ilielezwa kwamba watu wetu walijua watu wasiopungua elfu moja ambao tayari walikuwa wameukubali ukweli wa sasa katika sehemu mbalimbali za nchi kutokana na juhudi za watendakazi wa Biblia.
GSAM 397.2Shule hii iliendeshwa kwa ustadi na Mchungaji Geo. B. Starr hadi majira ya kuchipua ya mwaka 1891. Kisha, ikiwa na walimu walioteuliwa na Kamati ya Konferensi Kuu, iliendelea na kazi yake hadi mwaka 1893, ambapo iligundulika kwamba jengo halikutosha kutimiza mahitaji yaliyokuwa yakiongezeka ya mafundisho ya Biblia. Kwa kuwa mipango ilifanywa ya kuunganisha shule ya Biblia na Chuo cha Battle Creek, jengo la Chicago liliuzwa kwa Chama cha Umishenari wa Kitabibu na Hisani. Jengo hilo limepanuliwa na kuwekwa vifaa vya kituo kidogo cha tiba na afya, na sasa linaitwa Tawi la Chicago la Kituo cha Tiba na Afya cha Battle Creek.
GSAM 397Chuo cha Muungano, Nebraska
GSAM 397.3Konferensi Kuu ya 1889 ilifikiria pendekezo la kujenga chuo mahali ambapo pangefaa kwa konferensi za majimbo tisa yafuatayo: Iowa, Minnesota, Kansas, Missouri, Nebraska, Dakota, Texas, Colorado, na Arkansas. Kwa hiyo konferensi iliteua kamati iliyokuwa na wajibu wa kuchagua mahali panapofaa kwa shule hiyo. Wakazi wa maeneo kama Des Moines, Iowa, Fremont na Lincoln, Nebraska, na maeneo mengine walipopata habari za yale tuliyokuwa karibu kufanya, walishindana kutoa ahadi za michango kwa kazi hiyo, kwa kuwa watu wa kila mahali walitamani sana majengo hayo yawe katika mji wao. Kwa kuwa Lincoln, Nebraska, ilitoa ahadi za ukarimu zaidi, na pia ilionekana kuwa mahali panapofaa zaidi, shule iliwekwa huko.
GSAM 398.1Jengo kuu, yaani jengo la Chuo cha Muungano lenyewe, lina vipimo vya futi 141 x 84. Urefu kutoka ardhini hadi kilele cha kuba ni futi 100. Zaidi ya jengo hili kuna mabweni mawili, kila moja likiwa na vipimo vya futi 104 x 104 na ghorofa tatu. Ilitarajiwa kwamba mapato ya ardhi iliyotolewa kama zawadi yangelipa angalau nusu ya gharama ya kukiandaa chuo hiki kikuu cha dhehebu, ambamo watendakazi wangeelimishwa katika idara tofauti za Kiingereza, Kiskandinavia, na Kijerumani na walimu wakifundisha kwa lugha zao za asili.
GSAM 398.2Majengo yaliwekwa wakfu Septemba 24, 1891, na shule ikafunguliwa Septemba 30. Idadi ya walioandikishwa katika mwaka wa kwanza ilikuwa 301. Mwaka 1892 shule ilifunguliwa ikiwa na wanafunzi 222 waliohudhuria, na idadi ya walioandikishwa katika mwaka huo ilikuwa 553. Kati ya hawa, sabini na mmoja walikuwa katika idara ya Kijerumani, na themanini na watano katika idara ya Kiskandinavia.
GSAM 398.3Chuo kina shamba linalotoa kazi kwa wanafunzi wanaotaka kufanya kazi za kilimo. Chuo pia kina kiwanda cha kuoka mikate, ambamo vyakula vya afya hutengenezwa kwa kiasi fulani. Katika mwaka 1903 chama kiliundwa kwa kusudi la kuchapisha magazeti na vitabu katika lugha za Kijerumani, Kiswidi, na Kidenmaki-Kinorwe. Chama hiki kinamiliki nyumba yake ya uchapishaji na shughuli zote za uchapishaji za dhehebu katika Marekani kwa ajili ya watu wa mataifa hayo. Kazi inafanywa hasa na wanafunzi. Wanafundishwa kazi ya uchapishaji, na pia hapa hupata uzoefu kwa kufanya kazi ya umishenari wenyewe.
GSAM 398.4Kazi ya tiba pia ina nafasi katika chuo hiki. Kwa kutumia nafasi kwa uangalifu, iligundulika kwamba shule ingeweza kuendelea bila kutumia mojawapo ya mabweni yake makubwa, na hivyo, kwa gharama ndogo, kituo cha tiba na afya kikaanza kufanya kazi, nacho kinafanya kazi nzuri sana.
GSAM 399Chuo cha Walla Walla
GSAM 399.1Shule hii iko karibu na Walla Walla, katika Jimbo la Washington, na iliwekwa wakfu Desemba 8, 1892. Shule ilifunguliwa siku iliyotangulia ikiwa na wanafunzi 101 waliohudhuria. Idadi hii iliongezeka katika mwaka huo hadi 185. Shule hii ina shamba dogo na shughuli nyingine za uzalishaji. Inaendelea kustawi, na inafanya kazi nzuri. Profesa J. L. Kay sasa ndiye mkuu wa walimu.
GSAM 399Shule ya Australia
GSAM 399.2Agosti 24, 1892, shule ilifunguliwa huko Melbourne, Australia, katika jengo la kukodi, ikiwa na walimu watano. L. J. Rousseau, kutoka Chuo cha Battle Creek, Michigan, alikuwa mkuu wa kwanza wa shule hiyo. Katika mwaka 1894 shule hii ilikuwa na wanafunzi 89 walioandikishwa.
GSAM 399Kuhamia Avondale
GSAM 399.3Waanzilishi wa shule walipotamani kuunganisha kazi na masomo, ilionekana inafaa kubadili mahali pa shule; kwa hiyo ilihamishwa kutoka mji mkubwa wa Melbourne kwenda Avondale, Cooranbong, New South Wales, eneo la mashambani, ambako shamba lilipatikana na majengo yanayofaa yakajengwa. Kwa sasa shule inaendeshwa kwa mafanikio kwa mpango wa elimu inayoambatana na kazi za mikono.
GSAM 399Utabiri Kuhusu Avondale Watimizwa
GSAM 399.4Katika kuanzishwa na kuendeshwa kwake, lengo la kamati lilikuwa shule iendeshwe, kadiri iwezekanavyo, kwa kupatana na maelekezo yaliyotolewa kuhusu shule za elimu na kazi za mikono. Hii ilipaswa kuwa “shule ya mfano,” na uhakikisho ulitolewa tena na tena kwamba ikisimamiwa vizuri ingefanikiwa kama shule, na hata ardhi yenyewe, iliyokuwa imeonwa kuwa haina thamani, ingezaa mazao. Muda, pamoja na baraka za Bwana, umethibitisha ukweli wa utabiri huo. Licha ya ukame mkali wa miaka kadhaa mfululizo, ulioleta maafa katika shughuli za kilimo na kuharibu mavuno katika maeneo yote yaliyowazunguka, shamba la Avondale lilikuwa la kijani na lilizaa mazao. Hili lilikuwa jambo la ajabu sana, hata maofisa wa serikali wakaja kuuliza ni njia gani za kilimo zilizotumiwa kuleta mafanikio hayo ya kustaajabisha.
GSAM 400.1Ripoti ya shughuli za shule kwa mwaka 1903 inaonyesha ongezeko la asilimia hamsini katika mahudhurio. Hali ya fedha pia ilikuwa nzuri—gharama zote zilikuwa zimelipwa, na salio la $1,500 lilibaki katika hazina kwa matumizi ya shule. Profesa C. W. Irwin amekuwa msimamizi na mkuu wa shule kwa karibu miaka minne.
GSAM 400Akademia ya Mt. Vernon
GSAM 400.2Konferensi Kuu, mwaka 1893, ilipitisha azimio la kuunga mkono kufunguliwa kwa akademia huko Mt. Vernon, Ohio. Shule hii ina shughuli fulani za uzalishaji zinazoambatana nayo, na inaripotiwa kuwa inafanya kazi nzuri. Idadi ya walioandikishwa mwaka 1894 ilikuwa 140. Profesa J. W. Loughhead alikuwa ametumika kwa miaka kadhaa kuwa mkuu wa shule hii, hadi alipoitwa kwenda Washington, D.C. Anwani ya shule ni Academia, Ohio.
GSAM 400Shule ya Elimu na Kazi za Mikono ya Keene
GSAM 400.3Konferensi Kuu ya 1893 iliidhinisha kufunguliwa kwa shule ya elimu na kazi za mikono huko Keene, Texas. Shamba la zaidi ya ekari 130 lilipatikana, majengo yakajengwa, na shule ikafunguliwa chini ya Profesa C. B. Hughes na wasaidizi wake. Inaendeshwa kwa kupatana na mpango wa kuunganisha kazi na masomo. Idadi ya walioandikishwa mwaka 1894 ilikuwa wanafunzi 160. Shule hii pia imepata mafanikio dhahiri.
GSAM 400Chuo cha Muungano cha Claremont
GSAM 400.4Shule hii iko Kenilworth, karibu na Cape Town, Afrika Kusini. Walimu wake wengi walichaguliwa kutoka Chuo cha Battle Creek. Ilifunguliwa mwaka 1894, ikiwa na wanafunzi tisini walioandikishwa. Mwishoni mwa mwaka wa kwanza wa masomo, idadi ya wanafunzi ilikuwa imeongezeka kiasi kwamba ilibidi kupanua jengo la shule ili kupata nafasi zaidi. Kwa sasa chuo kiko chini ya usimamizi wa Profesa C. H. Hayton.
GSAM 401.1Waadventista wa Sabato pia waliendesha shule ya kijiji (ya msingi) huko Claremont yenye wanafunzi sabini, na shule ya kanisa huko Beaconsfield, iliyokuwa na wanafunzi thelathini walioandikishwa mwaka 1894.
GSAM 401Muhtasari wa Kazi ya Elimu, 1895
GSAM 401.2Ripoti ifuatayo ilitolewa na katibu wa elimu kwa Konferensi Kuu katika Februari, 1895:—
GSAM 401.3“Vituo vya elimu vya dhehebu vinaweza kuelezwa kwa muhtasari kama ifuatavyo: Kuna vyuo vitano vilivyo katika maeneo yafuatayo: Battle Creek, Michigan; College View, Nebraska; Healdsburg, California; College Place, Washington; na Kenilworth, Afrika Kusini. Kuna akademia nne, au shule zinazotoa masomo ya viwango vya akademia katika nchi hii, huko South Lancaster, Massachusetts; Mt. Vernon, Ohio; Keene, Texas; na Graysville, Tennessee.... Zaidi ya hizi kuna Shule ya Biblia ya Australia; shule huko Mexico inayohusishwa na kazi ya umishenari wa kitabibu; shule kwa watoto wenyeji katika Kisiwa cha Pitcairn; katika Raiatea, cha kundi la Visiwa vya Society, katika Bahari ya Pasifiki Kusini; katika Bonacca, cha Visiwa vya Bay katika Bahari ya Karibea; karibu shule kumi na tano za kanisa katika nchi hii na nchi za nje; shule mbili za Biblia za Konferensi Kuu; na shule nyingi kiasi za wainjilisti wa vitabu na za konferensi za maeneo ambazo hazijawekewa utaratibu rasmi.”
GSAM 401.4Akitoa muhtasari wa mahudhurio katika vyuo na shule za kawaida za dhehebu, katibu anasema: “Kwa makadirio ya tahadhari, kuna wanafunzi zaidi ya 3,000 wa umri mbalimbali walioandikishwa katika shule za Waadventista wa Sabato kwa sasa.”
GSAM 402Muhtasari wa Taasisi za Elimu, 1903
GSAM 402.1Kazi na taasisi za elimu miongoni mwa Waadventista wa Sabato zimekua kwa uwiano na matawi mengine ya ujumbe. Kama inavyoonyeshwa katika Kitabu cha Mwaka cha Konferensi Kuu cha 1904, kwa sasa kuna vyuo na akademia tisa katika Marekani, na tano katika nchi nyingine. Zile za nchi nyingine ziko katika maeneo yafuatayo: Avondale, New South Wales; Kenilworth, Claremont, karibu na Cape Town, Afrika Kusini; Holloway, London Kaskazini, Uingereza; Nyhyttan, Järnboås, Uswidi; Friedensau, karibu na Magdeburg, Ujerumani.
GSAM 402.2Kuna shule za kati kumi na nne katika Marekani, na tano katika nchi nyingine. Hizi za nchi nyingine ziko Copenhagen, Denmark; Honolulu, Eneo la Hawaii; Diamante, Entre Rios, Jamhuri ya Argentina, Amerika Kusini; Curityba, Brazili, Amerika Kusini; Brusque, Brazili, Amerika Kusini.
GSAM 402.3Zaidi ya taasisi za elimu zilizotajwa hapo juu, kuna shule 357 za makanisa mahalia zinazoendeshwa na dhehebu. Kati ya hizi, 317 ziko Marekani, na arobaini katika nchi nyingine. Kama tungekuwa na takwimu sahihi hadi sasa, hesabu hizi zingekuwa kubwa zaidi sana. Shule nyingi zimefunguliwa tangu mwisho wa mwaka 1902. Kwa mfano, Konferensi ya Nebraska iliripoti kuwa na shule kumi za kanisa. Februari 1, 1904, ripoti yao inaonyesha “shule ishirini na nne za kanisa,” ongezeko la kumi na nne katika konferensi moja.
GSAM 402.4Hakika mkono wa Bwana unaoongoza umeelekeza kwa namna ya ajabu na kufungua njia kwa kazi ya elimu miongoni mwa watu hawa. Na awape hekima wale walioitwa kusimamia tawi hili la kazi yake, ili shule mbalimbali ziendeshwe kwa kupatana na mpango alioueleza. Ndipo kutakapokuwa na makundi makubwa ya watendakazi wenye uwezo, waliokuzwa kikamilifu kwa ajili ya Bwana, wala si wanaume na wanawake “waliositawi upande mmoja tu” katika elimu na tabia. “Bwana alitoa neno,” asema mtunga zaburi, na “kundi [jeshi, pambizoni] la waliolitangaza lilikuwa kubwa.”