Sura ya 22 — Muundo wa kanisa
GSAM 343.1“Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopungua, na kuweka wazee katika kila mji, kama nilivyokuamuru.”1
GSAM 343.2Katika kuendelezwa kwa ujumbe wa malaika wa tatu, miaka kumi na miwili ilikuwa imepita (tangu 1846 hadi 1858) kabla ya watu wetu kuonekana kutambua haja ya kuwa na ushirika wenye muundo rasmi zaidi ya kuamini tu ukweli na kuwa na upendo wa Kikristo. Ingawa Bwana alikuwa amesema na watu wake kuhusu jambo hili kupitia karama ya unabii, ilionekana kwamba walihitaji kupitia matatizo fulani ili waamke kabisa na kutambua haja ya kuunda konferensi, makanisa na vyama vya kusimamia mali na mambo ya fedha ya kazi ya Mungu.
GSAM 343Upinzani kwa Muundo wa Kanisa
GSAM 343.3Katika tanbihi iliyo kwenye ukurasa wa 12 wa Nyongeza ya Uzoefu na Njozi, iliyochapishwa mwaka 1854, Mchungaji James White anasema:—
GSAM 343.4“Baada ya wakati uliotazamiwa kupita mwaka 1844 kulikuwa na machafuko makubwa, na wengi walipinga muundo wowote wa kanisa, wakidai kwamba haukupatana na uhuru mkamilifu wa injili! Bibi White daima alipinga kila aina ya ushupavu wa kidini usio na kiasi, na tangu mapema alitangaza kwamba muundo fulani ulihitajika ili kuzuia na kurekebisha machafuko. Ni wachache wakati huu wanaoweza kuelewa uthabiti uliohitajika wakati huo ili ashikilie msimamo wake dhidi ya hali iliyoenea ya kukataa utaratibu na mamlaka.”
GSAM 344.1Umoja ambao umekuwapo miongoni mwa Waadventista Wasabato umeimarishwa na kudumishwa sana na maonyo na maagizo yake yaliyotolewa kwa wakati unaofaa.
GSAM 344George Storrs Kuhusu Muundo wa Kanisa
GSAM 344.2Maneno yafuatayo ya George Storrs, yaliyoandikwa mwaka 1844, yataonyesha yale waliyofundishwa kuhusu muundo wa kanisa wale waliokuwa wamejitenga na makanisa chini ya tangazo la ujio wa pili:—
GSAM 344.3“Jihadharini msitafute kuunda kanisa jingine. Hakuna kanisa linaloweza kuundwa kwa ubuni wa mwanadamu bila kuwa Babeli mara tu linapoundwa. Bwana aliliunda kanisa lake mwenyewe kwa vifungo imara vya upendo. Haviwezi kufanywa vifungo vilivyo imara kuliko hivyo; na vifungo hivyo visipoweza kuwaunganisha wale wanaojidai kuwa wafuasi wa Kristo, wanakoma kuwa wafuasi wake, na kwa kawaida hujitenga na mwili.”2
GSAM 344Utaratibu Katika Nyakati za Mitume
GSAM 344.4Waadventista Wasabato, kama ilivyoelezwa hapo awali, walikuwa bila muundo wowote rasmi kwa miaka mingi, hata hawakuwa na muundo wa kanisa. Mtu yeyote aliyekuwa na ujasiri wa kukubali ukweli na kuutii licha ya shinikizo la upinzani kutoka nje lililokuwapo wakati huo, alihesabiwa kuwa mwaminifu na anayestahili upendo na ushirika wa Kikristo. Katika siku za mitume ulifika wakati ambapo ilikuwa lazima “kuyatengeneza yaliyopungua.”3 Karibu mwaka 65 B.K. Tito alipewa mamlaka ya “kuweka wazee katika kila mji” ambako kulikuwa na waumini, na Timotheo alipokea maagizo ya kina kuhusu jambo hilo.4
GSAM 344Mchungaji White Kuhusu Muundo wa Kanisa
GSAM 344.5Maneno yafuatayo ya Mchungaji James White kuhusu muundo wa kanisa na nidhamu yalichapishwa katika Mapitio na Mbiu la Januari 4, 1881:—
GSAM 345.1“Muundo wa kanisa ulikusudiwa kuhakikisha umoja katika utendaji, na kuwa kinga dhidi ya udanganyifu. Haukukusudiwa kamwe kuwa mjeledi wa kulazimisha utii, bali kuwalinda watu wa Mungu. Kristo hawasukumi watu wake kwa nguvu; anawaita. ‘Kondoo wangu huisikia sauti yangu, nami nawajua, nao hunifuata.’ Kichwa chetu kilicho hai hutangulia njiani, na kuwaita watu wake wamfuate.
GSAM 345.2“Kanuni za imani zilizotungwa na wanadamu haziwezi kuleta umoja. Nguvu ya kulazimisha ya kanisa haiwezi kulisukuma kanisa liwe mwili mmoja. Kristo hakukusudia kamwe kwamba akili za wanadamu zifinyangwe kwa ajili ya mbingu kwa ushawishi wa akili za wanadamu wengine. ‘Kichwa cha kila mwanamume ni Kristo.’ Sehemu yake ni kuongoza, na kufinyanga, na kutia chapa ya sura yake mwenyewe kwa warithi wa utukufu wa milele. Hata muundo wa kanisa ukiwa wa maana kiasi gani katika kulilinda kanisa na kuhakikisha upatano katika utendaji, haupaswi kuingilia na kuondoa nidhamu mikononi mwa Bwana.
GSAM 345Umoja Kati ya Misimamo Miwili Iliyopita Kiasi
GSAM 345.3“Kati ya misimamo miwili iliyopita kiasi, yaani nguvu ya kulazimisha ya kanisa na kujitegemea kusikotakaswa, tunaipata siri kuu ya umoja na ufanisi katika huduma na katika kanisa la Mungu. Tunaelekezwa kulitazama jambo hili katika nasaha nzito sana za mtume Petro mwenye kustahiwa kwa wazee wa wakati wake: ‘Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee mwenzenu, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki pia wa utukufu utakaofunuliwa: lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, mkilisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari; si kwa kutaka faida ya aibu, bali kwa moyo wa utayari; wala si kama mabwana juu ya urithi wa Mungu, bali mkiwa vielelezo kwa kundi. Na Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji ya utukufu isiyonyauka. Vivyo hivyo, ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote nyenyekeaneni, na kujivika unyenyekevu; kwa maana Mungu huwapinga wenye kiburi, na kuwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.’5
GSAM 346Urahisi na Muundo wa Utaratibu wa Agano Jipya
GSAM 346.1“Wale waliotayarisha muundo uliokubaliwa na Waadventista Wasabato walijitahidi kuingiza ndani yake, kadiri ilivyowezekana, urahisi wa maneno na wa muundo unaopatikana katika Agano Jipya. Kadiri roho ya injili inavyodhihirishwa zaidi, na kadiri mfumo unavyokuwa rahisi zaidi, ndivyo unavyokuwa na ufanisi zaidi.
GSAM 346.2“Konferensi Kuu husimamia kazi kwa ujumla katika matawi yake yote, kutia ndani konferensi za majimbo. Konferensi ya jimbo husimamia matawi yote ya kazi katika jimbo, kutia ndani makanisa yaliyomo katika jimbo hilo. Nalo kanisa ni kundi la Wakristo walioungana kwa agano rahisi la kushika amri za Mungu na imani ya Yesu.
GSAM 346Viongozi wa Kanisa ni Watumishi
GSAM 346.3“Viongozi wa kanisa mahalia ni watumishi wa kanisa hilo, wala si mabwana wa kulitawala kwa nguvu. ‘Aliye mkubwa miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu.’6 Viongozi hao wanapaswa kuwa vielelezo kwa washiriki wa kanisa katika uvumilivu, kukesha, sala, wema na ukarimu, na wanapaswa kuwaonyesha kwa kiasi kikubwa wale wanaowatumikia upendo ule unaodhihirishwa katika maisha na mafundisho ya Bwana wetu.”
GSAM 346Ushuhuda wa Kwanza Kuhusu Utaratibu
GSAM 346.4Katika Nyongeza ya Uzoefu na Njozi, iliyochapishwa mwaka 1854, yametolewa maagizo fulani ya pekee kuhusu utaratibu wa injili. Kwenye ukurasa wa kumi na tano tunasoma yafuatayo:—
GSAM 346.5“Kanisa lazima likimbilie neno la Mungu, na kujengwa juu ya utaratibu wa injili, ambao umepuuzwa na kuachwa. Jambo hili ni la lazima kabisa ili kulileta kanisa katika umoja wa imani.”
GSAM 347Utaratibu Unahitajika Karibu na Mwisho
GSAM 347.1Katika ushuhuda uliotolewa Desemba 23, 1860, tunasoma:
GSAM 347.1“Tunapokaribia mwisho wa wakati, Shetani anashuka akiwa na nguvu nyingi, akijua kwamba wakati wake ni mfupi. Nguvu zake zitatumiwa hasa dhidi ya masalio. Atapigana nao, na kutafuta kuwagawanya na kuwatawanya, ili wadhoofike na kuangushwa. Watu wa Mungu wanapaswa kutenda kwa ufahamu, na wanapaswa kuungana katika juhudi zao. Wanapaswa kuwa na nia moja na uamuzi mmoja; hapo juhudi zao hazitatawanyika, bali zitakuwa na matokeo yenye nguvu katika kuijenga kazi ya ukweli wa sasa. Utaratibu lazima uzingatiwe, na lazima pawe na umoja katika kudumisha utaratibu, la sivyo Shetani atapata nafasi ya kuwashinda.”7
GSAM 347Utaratibu wa Malaika Unapaswa Kuigwa
GSAM 347.2Katika Ushuhuda Na. 14, uliochapishwa mwaka 1868, tunasoma: “Kadiri tunavyoiga kwa ukaribu zaidi upatano na utaratibu wa jeshi la malaika, ndivyo juhudi za wajumbe hao wa mbinguni kwa ajili yetu zitakavyofanikiwa zaidi. Tusipoona haja ya kutenda kwa upatano, na tukiwa bila utaratibu, bila nidhamu, na bila muundo katika mwenendo wetu wa kazi, malaika, ambao wamepangwa kikamilifu na hutenda kwa utaratibu mkamilifu, hawawezi kutufanyia kazi kwa mafanikio. Wanaondoka kwa huzuni, kwa maana hawajapewa mamlaka ya kubariki machafuko, vurugu na ukosefu wa muundo.
GSAM 347Mungu Bado ni Mungu wa Utaratibu
GSAM 347.3“Je, Mungu amebadilika, asiwe tena Mungu wa utaratibu? La; yeye ni yuleyule katika kipindi cha sasa kama alivyokuwa katika kipindi kilichotangulia. Paulo anasema, ‘Mungu si chanzo cha machafuko, bali cha amani.’ Anataka mambo yafanywe kwa uangalifu uleule sasa kama alivyotaka wakati huo. Naye anakusudia tujifunze masomo ya utaratibu na muundo kutokana na utaratibu mkamilifu aliouweka siku za Musa kwa manufaa ya wana wa Israeli.”8
GSAM 348Sala ya Kristo kwa Ajili ya Utaratibu
GSAM 348.1Katika ushuhuda ulioandikwa mwaka 1882 tunaona wazo hilohilo likielezwa kwa maneno haya,
GSAM 348.1“Kwamba umoja na upendo viwepo miongoni mwa wanafunzi wake ndilo lililokuwa ombi kuu la sala ya mwisho ya Mwokozi wetu kwa ajili yao kabla ya kusulubiwa kwake.... ‘Wala si hao tu ninaowaombea; bali na wale watakaoniamini kwa neno lao; ili wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe na umoja ndani yetu; ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma.’”9
GSAM 348Hatari ya Kujitegemea kwa Mtu Binafsi
GSAM 348.2Mwaka 1885 ushuhuda huu ulitolewa:
GSAM 348.2“Jambo moja litahitaji kuangaliwa kwa makini, nalo ni kujitegemea kwa mtu binafsi. Tukiwa askari katika jeshi la Kristo, tunapaswa kutenda kwa pamoja katika idara mbalimbali za kazi.”10
GSAM 348Shetani Hufurahia Kuvunja Utaratibu
GSAM 348.3Katika ushuhuda maalumu uliochapishwa mwaka 1895 tunasoma,
GSAM 348.3“Lo, jinsi Shetani angefurahi kuingia miongoni mwa watu hawa na kuvuruga muundo wa kazi wakati ambapo muundo imara unahitajika kabisa, nao utakuwa nguvu kubwa zaidi ya kuzuia maasi ya udanganyifu na kukanusha madai yasiyothibitishwa na neno la Mungu. Tunataka kushikilia hatamu kwa usawa, ili mfumo wa kanuni na utaratibu usivunjike.”
GSAM 348Kuwatambulisha Wachungaji kwa Mapendekezo
GSAM 348.4Mojawapo ya mambo ya kwanza yaliyopaswa kufikiriwa katika kuweka utaratibu miongoni mwa watu wetu, kupatana na shuhuda zilizonukuliwa sasa hivi, lilikuwa namna fulani ya kuwatambua wale waliohubiri ujumbe. Tangu mwaka 1850 hadi 1861, mpango uliotumiwa ulikuwa wa kuwapa wachungaji waliokuwa wamethibitisha karama yao, ambao ilionekana wazi kwamba walikubaliwa na Bwana na walipatana na kazi yote, kadi ya kuwapendekeza wapokelewe katika ushirika wa watu wa Bwana kila mahali, ikisema tu kwamba walikubaliwa katika kazi ya huduma ya injili. Kadi hizo ziliwekewa tarehe na kutiwa saini na wachungaji wawili waliokuwa miongoni mwa viongozi wakuu, ambao watu wetu waliwajua kuwa viongozi katika kazi.
GSAM 349Matunzo ya Wachungaji
GSAM 349.1Katika majira ya baridi ya mwaka 1858-59 yalitolewa maagizo kwamba Biblia ilikuwa na mfumo kamili wa kugharimia huduma ya wachungaji, na kwamba kama watu wetu wangelichunguza jambo hilo kwa msingi wa Maandiko wangeupata mfumo huo. Kwa hiyo darasa la Biblia lilifanyika Battle Creek, likiongozwa na Mchungaji J. N. Andrews. Baada ya kujifunza Maandiko kwa uangalifu na kwa sala, makala ilitayarishwa na kuchapishwa katika Mapitio na Mbiu la Februari 3, 1859, ikieleza mpango uliokuwa na kanuni ya kutoa zaka. Hotuba kuhusu jambo hilo iliwasilishwa mbele ya kusanyiko kubwa la watu wetu, waliokusanyika katika mkutano mkuu huko Battle Creek, Michigan, Juni 6, 1859, na kupitishwa kwa kauli moja kwa kura ya kusanyiko lote.
GSAM 349Kusifiwa kwa Utaratibu Uliowekwa
GSAM 349.2Katika Ushuhuda Na. 6, wa mwaka 1861, Bwana alisema hivi kupitia Bibi White kuhusu mfumo uliokuwa umekubaliwa na Waadventista Wasabato:
GSAM 349.2“Msimwibie Mungu kwa kumnyima zaka na sadaka zenu. Wajibu wa kwanza mtakatifu ni kumpa Mungu sehemu inayofaa. Msimruhusu mtu yeyote alete madai yake na kuwaongoza kumwibia Mungu. Msiwaruhusu watoto wenu kuiba sadaka zenu kutoka madhabahu ya Mungu kwa manufaa yao wenyewe.
GSAM 349Mfumo wa Zaka wa Kukuza Tabia
GSAM 349.3“Niliona kwamba mfumo huu wa zaka ungekuza tabia na kudhihirisha hali ya kweli ya moyo. Jambo hili likielezwa kwa watu kulingana na maana yake halisi, nao wakaachwa waamue wenyewe, wataona hekima na utaratibu katika mfumo wa zaka.”
GSAM 349.4Kwa namna hii mfumo wa fedha ulianzishwa miongoni mwa Waadventista wa Sabato kwa ajili ya kutegemeza kazi ya huduma, nao sasa unatumiwa na watu wetu ulimwenguni kote.
GSAM 350.1Katika Mapitio na Mbiu la Julai 21, 1859, kutokana na maagizo yaliyokuwa yametolewa hapo awali kupitia Shuhuda, ilipendekezwa kwa mara ya kwanza kwamba kila jimbo lifanye mkutano wa kila mwaka ambamo kazi ingepangiwa kwa uangalifu; hivyo kuepuka machafuko yaliyokuwa ya kawaida mno katika namna ya utendaji wa wachungaji, na kuhakikisha kwamba utaratibu na mpango vinafuatwa katika kazi yetu. Pendekezo hili kwa kweli lilielekea kwenye kuundwa kwa konferensi za majimbo.
GSAM 350Umiliki wa Mali za Kanisa
GSAM 350.2Kadiri ujumbe ulivyoenea na idadi ya waumini kuongezeka, mali nazo ziliongezeka kwa kawaida, jambo lililosababisha kuzingatiwa kwa umiliki halali wa mali za kanisa. Katika makala ya Mchungaji White iliyomo katika Mapitio na Mbiu la Februari 23, 1860, tunasoma yafuatayo:—
GSAM 350.3“Hata hivyo, tunatumaini kwamba wakati hauko mbali ambapo watu hawa watakuwa na hadhi inayohitajika ili waweze kukatia bima mali za kanisa na kumiliki nyumba zao za ibada kwa namna ifaayo, na kwamba wale wanaoandika wosia na kutaka kufanya hivyo waweze kutenga sehemu ya mali zao kwa idara ya uchapishaji. Tunawaomba wahubiri wetu na ndugu viongozi walizingatie jambo hili. Ikiwa yeyote anapinga mapendekezo yetu, je, atakuwa tayari kuandika mpango ambao sisi kama watu tunaweza kuufuata?”
GSAM 350Kuundwa kwa Taasisi Halali Kwaidhinishwa
GSAM 350.4Katika majira ya kiangazi ya mwaka huu, jambo hili lilijadiliwa kwa kiasi fulani katika hali ya kirafiki katika Mapitio na Mbiu. Na katika mkusanyiko mkuu wa wawakilishi wa watu wetu kutoka Michigan na majimbo mengine kadhaa, uliofanyika Battle Creek kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 1, jambo hili lilizingatiwa kwa unyoofu, na kulikuwa na majadiliano kamili na ya wazi kuhusu kuunda taasisi halali kwa kusudi la kumiliki ofisi ya uchapishaji na mali nyingine za kanisa—nyumba za ibada, na kadhalika. Majadiliano haya yanapatikana kwa kirefu katika Mapitio na Mbiu, Juzuu ya 16, Na. 21, 22, na 23, zilizotolewa Oktoba 9, 16, na 23, 1860.
GSAM 351.1Kutokana na mashauriano katika mkusanyiko huu, iliamuliwa kwa kura za wote kuunda kisheria chama cha uchapishaji, na ili taasisi hiyo iweze kuundwa upesi kadiri iwezekanavyo, mkutano uliokuwa umekusanyika ulichagua kamati ya watu watano.
GSAM 351Jina la Dhehebu
GSAM 351.2Mkutano huu pia ulizingatia suala la jina ambalo watu wetu wangeitwa. Hili tena lilizusha maoni mbalimbali, wengine wakitetea jina moja na wengine jingine. Jina “Kanisa la Mungu” lilipopendekezwa, lilipingwa kwa sababu halikuonyesha sifa zozote za pekee za imani yetu, ilhali jina “Waadventista wa Sabato” lingeonyesha imani yetu katika kukaribia kwa kuja kwa Kristo, na pia kuonyesha kwamba tulikuwa watunzaji wa Sabato ya siku ya saba. Mkusanyiko uliunga mkono jina hili la mwisho kwa umoja mkubwa kiasi kwamba lilipopigiwa kura, mtu mmoja tu alilipinga, naye muda mfupi baadaye aliondoa pingamizi lake.
GSAM 351Jina Laidhinishwa
GSAM 351.3Katika Ushuhuda Na. 6, tunasoma:
GSAM 351.3“Hakuna jina tunaloweza kuchukua litakalofaa isipokuwa lile linalopatana na kile tunachokiri, linaloeleza imani yetu, na kututambulisha kuwa watu wa pekee....
GSAM 351.4“Jina Mwadventista wa Sabato huweka wazi sifa za kweli za imani yetu, nalo litausadikisha moyo wa mtu anayetafuta kujua. Kama mshale kutoka katika podo la Bwana, litawachoma wavunjaji wa sheria ya Mungu, na kuwaongoza kumtubia Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.”
GSAM 351.4Matokeo ya ushuhuda huo yalikuwa kulimaliza suala hili milele katika mioyo ya waumini.
GSAM 351Kazi ya Karama ya Kweli
GSAM 351.5Je, hii si kazi maalumu ya udhihirisho wa karama za Roho wa Mungu? Paulo alisema kwamba ziliwekwa kanisani “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, kwa kazi ya huduma, kwa kuujenga mwili wa Kristo: hata sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani,” na kadhalika.11 Jinsi inavyofaa kwamba baada ya waumini kutafuta nuru kwa maombi na unyenyekevu, Roho aseme, “Hii ndiyo njia; maamuzi yenu ni sahihi;” na kisha “kulijenga” kanisa zaidi, kama katika jambo hili, kwa kuwaeleza jinsi suala hili linavyohusu matendo yao na baadhi ya matokeo mema yatakayotokana na maamuzi yao.
GSAM 352Muundo wa Kanisa
GSAM 352.1Katika hotuba iliyotolewa na Mchungaji White mbele ya Konferensi Kuu huko Battle Creek, Aprili 1861, na kuchapishwa katika Mapitio na Mbiu la Juni 11, 1861, alianzisha wazo la kuyapa makanisa yetu muundo kamili zaidi. Kwa mwaliko, wachungaji tisa walifanya somo la Biblia ili kutafuta nuru juu ya jambo hili, nao waliombwa na Konferensi wachapishe katika Mapitio na Mbiu matokeo ya uchunguzi huo. Baada ya kutoa ushuhuda wa Maandiko kuhusu utaratibu wa kanisa na maofisa wa kanisa, lilizingatiwa suala la uwakilishi sawa wa majimbo mbalimbali katika Konferensi Kuu, pamoja na uwakilishi ufaao na ulio sawa wa makanisa katika konferensi za majimbo. Kwa kweli huu ulikuwa mwanzo wa kutolewa kwa wazo la kuwa na wajumbe waliochaguliwa ipasavyo kwenye mikusanyiko mikuu kwa uwiano fulani ulio sawa ambao ungeweza kukubaliwa.
GSAM 352Konferensi ya Jimbo la Michigan Yaundwa
GSAM 352.2Oktoba 6, 1861, Konferensi ya Michigan iliundwa kwa kuchaguliwa kwa mwenyekiti, katibu, na kamati tendaji ya watu watatu. Kwa kura ya konferensi ilipendekezwa kwamba makanisa yaunde miundo yao, yakikubali yafuatayo kuwa agano la kanisa:—
GSAM 352.3“Sisi tuliotia sahihi hapa chini, kwa tamko hili tunaungana pamoja kama kanisa, tukichukua jina Waadventista wa Sabato; tukifanya agano la kuzishika amri za Mungu na imani ya Yesu Kristo.”
GSAM 353Hati za Uthibitisho wa Huduma za Wachungaji
GSAM 353.1Katika konferensi hii iliamuliwa kwa mara ya kwanza kwamba hati za uthibitisho wa huduma zitolewe kwa wachungaji wote Waadventista wa Sabato katika jimbo hili waliokuwa na mwenendo mwema, na kwamba wachungaji wabebe nyaraka zilizojumuisha cheti cha kuwekewa mikono na hati za uthibitisho wa huduma zilizotiwa sahihi na mwenyekiti na katibu wa konferensi, na kwamba hati hizo zifanywe upya kila mwaka.
GSAM 353.2Pia iliamuliwa kwa kura kwamba kamati ichaguliwe kuandaa ujumbe wa kuwaeleza watu wetu namna ya kufuata katika kuunda makanisa. Ujumbe huu ulichapishwa katika Mapitio na Mbiu la Oktoba 15, 1861.
GSAM 353Hati za Uwakilishi za Wajumbe
GSAM 353.3Katika mwezi wa Septemba 1862, Konferensi ya Michigan ilifanya kikao chake cha kwanza huko Monterey. Hapa kwa mara ya kwanza lilitolewa wazo la kuyapokea makanisa katika konferensi kama vile washiriki walivyopokelewa makanisani kwa kura. Kwa kuwa makanisa kumi na saba katika jimbo yalikuwa tayari yameundwa, yalipokelewa katika konferensi kwa kura; na washiriki wote wa makanisa haya waliokuwapo walikubaliwa kuwa wajumbe.
GSAM 353Mishahara ya Wachungaji
GSAM 353.4Ilikuwa pia katika konferensi hii ambapo mpango wa kuwalipa wachungaji kiasi fulani kwa juma kwa huduma walizotoa ulikubaliwa. Wachungaji kwa upande wao walitakiwa kutoa taarifa ya muda waliotumia kufanya kazi katika konferensi, pamoja na mapato na matumizi yao; na konferensi iliyopokea taarifa hii ilipaswa kukamilisha hesabu na malipo ipasavyo.
GSAM 353Wajumbe Wawasilisha Hati za Uwakilishi kwa Mara ya Kwanza
GSAM 353.5Mei 20, 1863, Konferensi Kuu ilifanyika Battle Creek, Michigan. Hiki kilikuwa kikao cha kwanza cha chombo hicho ambamo wajumbe walibeba hati za uwakilishi kutoka majimbo yao. Hata hivyo, uwakilishi haukutegemea idadi ya washiriki. Majimbo yaliyowakilishwa katika tukio hili yalikuwa Michigan, Wisconsin, Iowa, Minnesota, New York, na Ohio.
GSAM 354Katiba za Konferensi Kuu na Konferensi za Majimbo
GSAM 354.1Mei 21, katiba ilikubaliwa na Konferensi Kuu, na siku hiyo hiyo katiba ya jimbo ilipendekezwa kwa konferensi za majimbo. Ilikubaliwa katika kikao cha Konferensi ya Michigan. Katiba hizi ziliweka msingi wa uwakilishi wa wajumbe kwa kufuata idadi ya washiriki katika konferensi za majimbo na katika Konferensi Kuu. Katiba ya jimbo iliyopendekezwa hapo inafanana kwa kiasi kikubwa na ile inayotumiwa sasa na konferensi zetu sabini na mbili za maeneo mbalimbali ulimwenguni kote.
GSAM 354.2Wakati wa Konferensi Kuu, katika majira ya kuchipua ya 1864, kwa mara ya kwanza pendekezo lilitolewa kwa konferensi ya jimbo kwamba ichaguliwe Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu yenye washiriki wa kawaida ambao hawakuwa wameajiriwa na konferensi katika mwaka huo, ili ifanye kazi pamoja na kamati tendaji katika kukagua na kukamilisha hesabu na malipo ya wachungaji. Hivyo hatua kwa hatua, kadiri mahitaji yalivyotokea, utaratibu uliwekwa katika kazi na shughuli za Mungu.
GSAM 354.3Hivyo tumeeleza kwa ufupi hatua zilizoongoza kwenye kuwekwa kwa muundo rasmi wa kazi. Hili lilifanywa wakati dhehebu lilikuwa dogo sana likilinganishwa na lilivyo wakati huu.
GSAM 354.4Konferensi Kuu ilipoundwa kikamilifu mwaka 1863, jumla ya wajumbe haikuwa kubwa kama idadi tuliyo nayo sasa kila mwaka katika baadhi ya konferensi ndogo za maeneo mbalimbali.
GSAM 354Kusudi la Kuweka Muundo
GSAM 354.5Lengo la kuweka muundo lilikuwa kwamba mali za jumuiya ziweze kumilikiwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria; na kwamba watenda kazi waweze kutenda kwa umoja, bila machafuko, kwa kuwa hatua zao zilifuata mashauriano, na hivyo bila kuvurugika. Kanuni zilezile zilizokubaliwa katika muundo wetu hadi mwaka 1864 ziliingizwa katika kazi ilipopanuka na kuenea katika nchi na mataifa mengine.
GSAM 355Vyama Vikuu Vyaundwa
GSAM 355.1Kadiri ujumbe ulivyoenea, vyama vikuu vifuatavyo viliundwa, na maofisa wake walichaguliwa katika vikao vya kawaida vya Konferensi Kuu:—
GSAM 355.2Chama cha Konferensi Kuu—chombo halali chenye washiriki ishirini na mmoja, cha kushikilia hati za umiliki wa mali za taasisi mbalimbali katika Amerika na nchi nyingine.
GSAM 355.3Bodi ya Umishenari katika Nchi za Nje—ya kusimamia na kupanua kazi ya umishenari nje ya maeneo yenye konferensi zilizoundwa.
GSAM 355.4Chama cha Kimataifa cha Vijitabu—ambacho jukumu lake lilikuwa kugawanya maandiko ya kusoma na kuandikiana barua, kikitafuta kuanzisha vituo vipya vya umishenari.
GSAM 355.5Chama cha Uhuru wa Dini—kazi yake maalumu ikiwa kuwasaidia wale wanaoteswa kwa ajili ya dhamiri zao, na kusambaza maandiko kuhusu kanuni za uhuru wa dini.
GSAM 355.6Chama cha Kimataifa cha Shule ya Sabato—ambacho kusudi lake lilikuwa kuimarisha na kuendeleza kazi ya Shule ya Sabato katika maeneo yote ya kazi.
GSAM 355.7Chama cha Umishenari wa Kitabibu na Hisani—kazi yake ikihusu kuwafundisha madaktari na wauguzi, kuendesha taasisi za tiba na afya, makao ya yatima, wazee, na kadhalika.
GSAM 355Eneo la Kazi Hadi 1868
GSAM 355.8Hadi 1868, eneo letu la kazi lilijumuisha sehemu ya Marekani iliyoko mashariki mwa Mto Missouri na kaskazini mwa mstari wa latitudo unaolingana na mpaka wa kusini wa Missouri. Wakati huo Kamati ya Konferensi Kuu ilikuwa na wajumbe watatu tu, rais wa konferensi akiwa mmoja wao. Konferensi nane za maeneo mbalimbali zote zilikuwa chini ya usimamizi wa Konferensi Kuu, iliyokuwa na makao yake makuu Battle Creek, Michigan.
GSAM 356Kwa Nini Ilikuwa Lazima Kupanga Upya Muundo
GSAM 356.1Kadiri ujumbe ulivyoenea katika nchi nyingine, haja ilitokea ya kupanga upya muundo wa eneo lote la kazi. Kwa hiyo, hatua zilichukuliwa mwaka 1897 kuelekea kusudi hilo; lakini kazi ya kupanga upya imefanywa kwa kina zaidi katika miaka minne iliyopita, ambapo Konferensi Kuu ya Ulaya imeundwa, ikiwa na kamati tendaji yenye wajumbe kumi na wanne; nayo Konferensi Kuu ya awali, yenye makao yake makuu Washington, D.C., ina kamati tendaji yenye wajumbe ishirini na wanane, wanaowakilisha shughuli zote mbalimbali za ujumbe, na kuchukua nafasi ya baadhi ya vyama vikuu ambavyo vimekomeshwa.
GSAM 356Hali ya Muundo Januari 1, 1903
GSAM 356.2Yafuatayo kutoka katika Kitabu cha Mwaka cha Konferensi Kuu cha 1904 yanatoa takwimu zenye kuvutia hadi Januari 1, 1903:—
GSAM 356.3Wakati huo kazi yetu iliyokuwa na muundo ilijumuisha Konferensi Kuu mbili, zenye Konferensi za Muungano kumi na nne, konferensi sabini na mbili za maeneo mbalimbali, na misheni arobaini na mbili. Zimegawanywa kama ifuatavyo: konferensi za maeneo mbalimbali katika Amerika ya Kaskazini, arobaini na tisa; nje ya Amerika ya Kaskazini, ishirini na tatu. Konferensi za Muungano katika Amerika, nane; katika nchi nyingine, sita. Maeneo ya umishenari katika Amerika, pamoja na Alaska, Hawaii, na Newfoundland, matano; misheni nje ya Amerika, thelathini na saba, zikiwa katika maeneo yafuatayo: kumi na mbili Ulaya; nne Afrika; tatu Asia; mbili Amerika ya Kusini; mbili Afrika Kusini; na zilizobaki Amerika ya Kati, Meksiko, visiwa vya Karibi, na Visiwa vya Pasifiki. Wanaohusishwa na misheni hizi ni wachungaji sitini na saba, wakiwemo waliowekewa mikono na wenye leseni za huduma, pamoja na makanisa mia moja na thelathini na moja.
GSAM 356Umoja Katika Tofauti
GSAM 356.4Inatia moyo kujua kwamba vyama hivi tofauti katika nchi na mataifa mbalimbali vyote vimeungana katika kuendeleza kazi moja kuu ya ukweli na wokovu wa wanadamu. Hatuutumainii mpangilio rasmi wa muundo, bali tunamtumaini Mungu, mwanzilishi wa utaratibu. Kwa baraka zake juu ya matendo ya watenda kazi wake yaliyo na umoja na upatano, tunaweza kutambua jinsi ilivyo vema na kupendeza kuona “mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.”
Maelezo ya chini ya ukurasa
- Tito 1:5. ↩
- Kilio cha Usiku wa Manane, Februari 15, 1844. ↩
- Tito 1:5-9. ↩
- 1 Timotheo 3:1-15. ↩
- 1 Petro 5:1-6. ↩
- Mathayo 23:11. ↩
- Shuhuda kwa Kanisa, Juz. 1, uk. 210. ↩
- Kitabu hicho hicho, kur. 649, 653. ↩
- Shuhuda kwa Kanisa, Juz. 5, kur. 236, 237. ↩
- Kitabu hicho hicho, uk. 534 (mkazo umeongezwa). ↩
- Waefeso 4:12, 13. ↩